Duniani kote upinzani huwa una tabia ya kuchokonoa upungufu wa hoja na kisha kuonyesha vipi maboresho yangekuja kama wao wangeongoza Serikali. Hii maana yake bungeni unakuwapo ukosoaji wa aina mbili.

Ukosoaji endelevu (constructive criticisms) ambao unalenga kuboresha mada kwa faida ya Taifa. Tena upo ukosoaji bomoa (destructive criticisms) ambao daima hauoni jema upande wa waleta mada bali ni kukashifu, kubeza na kuchimbua (unearth) yaliyopita, hivyo kutokutumia muda wa kuchambua mada vizuri.

 

Malalamiko kwa Bunge hili huwa yanatolewa katika magazeti kwa imani kuwa waheshimiwa watasoma na kutusaidia wananchi kama walivyotuahidi. Hivi juzi tu imetolewa makala katika gazeti la HabariLeo Jumapili toleo No. 02026 Julai 8, 2012 uk. 23 kwenye “Haya ndiyo maisha”.

 

Makala yale yaliyoandikwa na Angela Semaya yalikuwa na kichwa cha habari ‘Bunge lisiwe sehemu ya kuonyeshana ubabe, kusanifiana’ pia katika makala yale yapo malalamiko kama vile, “Bunge siyo uwanja wa kuonyeshana nani anafahamu siasa na nani hafamu.”

 

Aidha, Bunge si sehemu ya kuonyeshana ubabe na kusanifiana. Hayo si mambo yatakayowasaidia wananchi kujiinua kiuchumi na kuondokana na umasikini. Wabunge wetu, vyema basi mkabadilika, fanyeni kile ambacho mmewaahidi wapiga kura wenu. Utamaduni uliojengeka ulimwenguni ni kambi ya upinzani kuonyesha upungufu wa Serikali na hivyo kuiamsha itambue upungufu wake na kujibadili kwa manufaa ya Taifa.

 

Mimi nafananisha upinzani na kichocheo (catalyst) katika kemia) kuharakisha maendeleo, lakini wenyewe haubadiliki kamwe (accelerate the development but itself does not change). Ni ufahamu wangu, kuwa upinzani unaleta hoja zenye nguvu kuonyesha uwezo wao.

 

Sijasikia popote upinzani unachochea (instigate) fujo na uvunjaji wa sheria. Huo upungufu mkubwa kwa upinzani katika nchi za ulimwengu wa tatu na ni hulka ya kutamani madaraka. Nami naongezea kuwa waheshimiwa wabunge wetu wote kwa ujumla wenu mjitahidi kuepuka upotoshaji wa hali ya maendeleo katika nchi yetu hii.

 

Kuna baadhi ya matamko kwa wananchi kama vile, “Serikali haijafanya lolote kuendeleza wananchi kwa miaka yote ya utawala wa chama tawala”, “Hakuna maendeleo, bali hali za wananchi bado ni duni tu!” “Serikali iliyopo madarakani imeshindwa kuwaletea maendeleo kwa kipindi chote cha miaka 50 ya utawala wake”.

 

Matamshi ya namna hii Waingereza wanayaita “Sweeping Statements” – matamko ya jumla jumla tu ni matamko ya kupotosha kabisa hali ya ukweli. Ningependa angalau kwa uzoefu wangu kama mwalimu wa darasani tangu mwaka 1954 kabla hata vuguvugu la siasa halijaanza nipo katika utumishi, nionyeshe angalau nijuavyo hali halisi ilivyo leo 2012 ukilinganisha na pale tulipopata Uhuru mwaka 1961. Nilikuwa mwalimu wa shule ya sekondari ya Serikali (Government boys secondary school) kwa hiyo nitakaloliandika nimeliishi kihalisia.

 

Mwaka ule wa 1961 hali ya elimu katika nchi yetu ilikuwa tofauti kabisa na hali hii tuionayo sasa. Mambo yamebadilika sana. Angalia, mwaka 1961 zilikuwapo shule za msingi 3,238 na zilikuwa na watoto 486,470. Tuliposherehekea mwaka wa 50 wa Uhuru wetu mwaka 2011, shule za msingi nchini zilikuwa 16,011 zenye kusomesha watoto 8,363,386. (Tazama ripoti Elimu: Best 2007 – 2011 uk. 20).

 

Hali ya maendeleo namna hii imeonekana hata katika elimu ya sekondari. Mwaka 1961 zilikuwapo shule za sekondari 41 tu zilizosomesha watoto 11,832. Mwaka 2011 hapa nchini zilikuwapo shule za sekondari 4,367 zenye kujaza watoto 1,789,547. Na kwa elimu ya chuo kikuu sote tunavyojua Tanganyika haikuwa na chuo kikuu na ndiyo kwanza TANU ilianzisha elimu namna hiyo pale Lumumba na wakawa watoto wa mwaka wa kwanza 14 pekee (1st year law).

 

Lakini nje ya nchi, Tanganyika ilikuwa na watoto kadhaa wakipata hiyo elimu ya chuo kikuu. Chuo kikuu cha Afrika Mashariki (Makerere na Nairobi) walikuwapo wanafunzi 261; vyuo vikuu Uingereza walikuwapo watoto 462; kule Marekani walikuwapo watoto 53 na Urusi walisoma Watanganyika wawili, na Lumumba 14. Kwa ujumla wanafunzi wa elimu ya chuo kikuu mwaka 1961 walikuwa 790 tu.  (Tanganyika itajengwa na wenye moyo uk. 11).

 

Sasa mwaka 2012 humu nchini tuna vyuo vikuu 32 na vinasomesha wanafunzi 139,638 (Best: 2007-2011 uk. 141). Hapo sijui inaingia akilini mwa mtu kupotosha ukweli huo kwa kusema hakuna maendeleo yoyote waliyopata wananchi tangu tupate Uhuru mwaka 1961; angalau kwa huduma hii ya elimu ukweli uko wazi kabisa.

 

Baba wa Taifa katika kile kijitabu chake cha ‘Tujisahihishe’ aliandika hivi na nukuu; “Ukweli una tabia moja nzuri sana. Haujali mkubwa wala mdogo; haujali adui wala rafiki, kwake wote ni sawa. Ukweli haupendi kupuuzwa puuzwa.” (Tujisahihishe uk. 3 ibara ya kwanza).

 

Baada ya kuonyesha Serikali ya chama tawala hapa katika kumpiga adui ujinga, labda tuone kidogo ilivyofanikiwa kumshambulia adui ugonjwa. Tumefanikiwaje? Mwaka 1961 nchi hii ilikuwa na madaktari wazalendo (wakiitwa Waafrika) 12 tu. (Nyerere: Uhuru na Maendeleo uk. 293). Mwaka 2011, miaka 50 ya Uhuru wetu nchi imekuwa na madaktari wazalendo zaidi ya 3,500. Mwaka 1961 hapakuwa na Chuo Kikuu cha Tiba, waliosomea fani namna hiyo walikwenda Makerere, Uganda.

 

TANU kwa kuharakisha kupambana na adui maradhi ilijenga Chuo cha Tiba cha Muhimbili mwaka 1963 na hivi leo ndiyo mahali panapofunza madaktari wengi sana. Mwaka 2011 nchi ilikuwa na vyuo vikuu vya uganga wa binadamu vitano nivijuavyo mimi Muhimbili, Kariuki, IMTU, KCMC na Bugando. Vyuo vyote hivi mwaka 2011 vilikuwa na wanafunzi 5,149 (Best: 2007-2011 uk. 143).

 

Aidha, kujitawala ni pamoja na kuwa na wataalamu wanaoendesha wizara na mashirika mbalimbali katika nchi. Mwaka 1961 nafasi za kazi za madaraka ya juu nchini zilikuwa 3,282. Katika hizo, wazalendo waliokuwa katika nafasi za uandamizi walikuwa 346 tu (Nyerere: Uhuru na Maendeleo uk. 263) kati ya zile nafasi 3,282.

 

Leo hii kazi zote kuanzia utawala, uhadhiri wa vyuo vikuu, majeshi, mashirika ya umma ni wananchi tu. Hilo nalo vijana wetu waheshimiwa wabunge watasemaje? Kweli hakuna maendeleo katika Taifa letu?  Ni lazima tuwe wazalendo na tujivunie nchi na Taifa letu wala tusijidhalilishe kwa kutangaza hakuna kilichofanyika.  Itaendelea.

 

Brigedia Jenerali mstaafu Francis Mbenna anapatikana katika simu 0715 806758. Alikuwa mwalimu wa sekondari na Afisa wa JWTZ. Ni mwanahistoria na ameandika kitabu cha HISTORIA YA ELIMU TANZANIA toka 1892 hadi sasa (Dar es Salaam University Bookshop).

 

By Jamhuri