Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limefafanua tuhuma dhidi yake zilizoibuliwa na Gazeti la JAMHURI hivi karibuni kuhusiana na ajira za upendeleo, matumizi mabaya ya ofisi, muundo mbovu, kuajiri watoto wa vigogo na nyingine.

Mkurugenzi wa Ofisi ya Spika, ambaye pia ni Katibu wa Spika, Said Yakub, ameliambia JAMHURI kwa niaba ya Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilillah kuwa tuhuma karibu zote zilizotolewa kupitia gazeti hili zina majibu sahihi, bali zimeonekana ni kashfa kutokana na baadhi ya watu walioathirika uamuzi uliofanywa kutokuwa na taarifa za kutosha.

Hoja kwamba bunge wameajiri watoto wa vigogo, Yakub ameliambia JAMHURI kuwa watoto wa wakubwa waliopo wamefuata taratibu za kuomba ajira baada ya nafasi walizonazo kutangazwa. 

Anasema katika Jumuiya ya Madola, uwiano kati ya wabunge na watumishi unapaswa kuwa mbunge moja kwa watumishi watatu, lakini kwa Tanzania uwiano ni mbunge mmoja kwa watumishi 1.5.

“Tusiangalie kuwa ni watoto wa wakubwa. Kuwa watoto wa wakubwa hakuwaondolei haki yao ya kikatiba ya kupata nafasi za kuajiriwa. Hao wanaotajwa kuwa watoto wa wakubwa, walipitia taratibu zote za ajira sawa na watumishi wengine.

“Tulitoa tangazo, wakaomba watu 332, kati yao tukachagua watu 156. Hawa walifanya usaili, tukapata watumishi 30. Nafasi nne zilibaki, baada ya kuonekana kati ya waliomba hawakuwa na sifa na taratibu za kuzitangaza kuitisha maombi upya zifanyika wakati ukifika,” anasema Yakub.

Yakub anasisitiza: “Si kosa mtoto wa waziri kufanya kazi ya utumishi wa umma. Inawezekana wapo, lakini walifuata taratibu.” 

Sambamba na hilo, anasema hoja kwamba baadhi ya Idara za Bunge watumishi wamefurika si ya kweli kwani mfano wa Idara ya Hansard wanaweza kuonekana wapo watumishi wengi wakati Bunge linapokuwa vikao haviendelei na ndiyo maana katika idara hiyo wanafanya kazi kwa mikataba ya muda maalum.

Kuhusu muundo wa utumishi wa Bunge uliotajwa kuwa umeongeza gharama za uendeshaji na watendaji kujiundia vyeo, Yakub amesema muundo mpya ulianzishwa na Spika wa Bunge la 9, Samuel Sitta baada ya kukabidhi kazi hiyo kwa taasisi ya Serikali ya National Institute of Productivity (NIP) iliyopendekeza namna bora ya muundo wa utumishi wa Bunge. Spika Anne Makinda ndiye aliridhia utekelezaji wa muundo mpya.

Anasema chini ya Muundo huo, Mtendaji Mkuu wa Bunge, ambaye ni Katibu wa Bunge, anakuwa na Manaibu Katibu wawili, ambao Mmoja anashughulika na Utawala na mwingine Shughuli za Bunge. 

Pia katika kurahisha utendaji, Katibu wa Katibu wa Bunge amepewa cheo cha ukurugenzi kumwezesha kufanya uamuzi katika baadhi ya masuala hali iliyoimarisha utendaji wa ofisi ya Katibu wa Bunge.

“Hata hivyo, tunafahamu kuwa baadhi ya watu waliozoea kwenda kwa Katibu wa Bunge moja kwa moja, wanaona kama mfumo huu unawanyima fursa ya kukutana na Katibu. Ila chini ya mfumo huu, kuna ufanisi mkubwa zaidi. Barua nyingine kulingana na uzito hazimsubiri Katibu wa Bunge pekee ndiye azipitishe au kuzitolea uamuzi. Huyu Katibu wa Katibu wa Bunge aliyepewa ngazi ya ukurugenzi katika muundo mpya, anakuwa mwanasheria kwa taaluma na ni mtu mwenye weledi wa kutosha,” anasema Yakub.

Taarifa za uhakika zinaonyesha kuwa baada ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais, John Pombe Magufuli kuingia madarakani, iliitaka ofisi ya Katibu wa Bunge kupunguza idadi ya watumishi wa Bunge, ambapo baadhi ya wakurugenzi waliokuwa wameteuliwa idara zao zilifutwa na nafasi moja ya Naibu Katibu wa Bunge (Jinsia) ilifutwa.

Awali, Bunge liliomba kupatiwa kibali cha kuajiri wafanyakazi 280, lakini wakapata kibali cha kuajiri wafanyakazi 34, ambao kati ya hao waliajiri 30 tu. Pia, Utumishi iliwambia Bunge kuwa pengo la wafanyakazi linalobaki lingejazwa kwa kufanya uhamisho wa ndani kutoka serikalini kwenda Bunge, utaratibu unaoendelea hadi sasa.

 

Ununuzi wa magari

Yakub anakiri kuwa yalikuwapo mabadiliko katika ununuzi wa magari, kwani Novemba, mwaka jana walipokwenda kununua magari nje ya nchi, walikuta aina ya magari yaliyokuwa yamepitishwa Toyata Land Cruiser VXL hakukuwapo idadi inayotosha, ikabidi wanunue Toyota Prado TXL. Kila gari moja la VX lilikuwa limepangiwa Sh milioni 168 kwa ajili ya ununuzi wa magari 14.

Hata hivyo, Ofisi ya Bunge ilinunua magari 10 tu aina ya TXL badala ya 14, na kati ya hayo 10 Yakub anasema Bunge limeweza kuokoa zaidi ya Sh milioni 300, huku akisema kuwa fedha zilizobaki ziko salama katika akaunti za Bunge.

Anasema baada ya kununua Toyota Prado TXL badala ya magari 10, zilizonunuliwa Sh milioni 149.1 kwa kila gari la automatic na Sh milioni 136.9 kwa kila gari la manual. “Kimsingi tulipaswa kupongezwa kwa kuokoa fedha zinazotosha kupata magari ya ziada, badala ya kushutumiwa,” anasema Yakub. Bunge ilikuwa halijanunua magari tangu mwaka 2000/2001.

 Tiketi za ndege na hoteli

Yakub amesema wafanyakazi wa Bunge wanaposafiri nje ya nchi huwa hawalipiwi hoteli isipokuwa viongozi wawili pekee ndiyo hulipiwa tiketi za ndege na hoteli kwa pamoja. Viongozi hao ni Spika na Naibu Spika wa Bunge.

Hata hivyo, anasema kwa nia ya kurahisisha utendaji au gharama za hoteli katika baadhi ya nchi mara kadhaa wafanyakazi wengine hulipa nusu posho (half board) na kulipiwa hoteli, chai na chakula cha mchana. 

 

“Unakuta mimi Katibu wa Spika nimesafiri na Spika inabidi tukae hoteli moja. Ikiwa Spika atalala Kilimanjaro Kempinski mimi nikaenda kulala Manzese, ukitokea ananihitaji nitachelewa kufika na shughuli zitakwama. Nikatika misingi hiyo huwa tunalipwa half board, kisha tunalala hoteli moja na viongozi,” anasisitiza Yakub.

 

Watumishi kuongezewa muda

 Yakub anasema baadhi ya watumishi wameongezwa muda kutokana na mahitaji maalum au mahitaji ya viongozi. “Mfano Tume ilimwongezea muda Abdallah Selemani aliyefanya kazi bungeni kwa miaka 42 ikitaka amalize kazi na Bunge la 10 kwa nia ya kuwapa mafunzo watumishi wengine. 

Unakuta dereva kwa mfano wa Mhe. Spika au Kiongozi wa Upinzani Bunge (KUB ), ameongezewa muda kwa maombi ya kiongozi anayemwendesha kutokana na umakini katika kazi yake,” anafafanua.

 

Bima ya afya kwa wabunge

 Kuhusu Bunge kulipa Sh bilioni 9 kwa ajili ya Bima za wabunge kwa kampuni binafsi, anasema Sheria ya Uongozi wa Bunge (National Assembly Administration Act ya Mwaka 2008), inataka wabunge kupewa huduma zenye hadhi ya kibunge ambazo zilikuwa hazitolewe na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), hivyo ikabidi watangaze huduma hii.

Baada ya kuitangaza, kampuni ya udalali ya Astra Isurance, iliomba kazi hiyo ikaipata na kuipeleka kwa Kampuni ya Bima ya Jubilee, ambayo ni sehemu ya mtadao wa Hospitali za Aga Khan, iliyolipwa Sh bilioni 9 katika mwaka wa 2014/2015, lakini tangu Novemba, mwaka jana, huduma hiyo imehamishiwa kwa NHIF, inayolitoza Bunge wastani wa Sh bilioni 6.

Awali, gazeti la JAMHURI liliripoti kuwa kabla ya kutumia utaratibu huu wa Bima, gharama halisi ya matibabu ya wabunge ilikuwa ni Sh bilioni 3 kwa mwaka. Sheria hiyo, inataka mbunge, mwenzi wake wa ndoa, watoto walio chini ya umri wa miaka 18 na wategemezi wapewa huduma za hadi ya kibunge wanapougua.

 

Wafanyakazi kutokwenda mafunzoni

Gazeti la JAMHURI lilichapisha habari kuwa wafanyazi wawili wa Bunge, Raphael Nombo na Mkurugenzi Msaidizi (Utawala), Ndofi Merkion walilipwa fedha za kwenda masomoni nchini Isarael, lakini baada ya kupokea wastani wa Sh milioni 103 kwa ujumla, walitia fedha hizo mfukoni na hawakwenda kwenye mafunzo. Nombo alitakiwa kurejesha wastani wa Sh milioni 32.2 na Mpanda, alitakiwa kurejesha Sh milioni 71.2.

Yakub amelionyesha JAMHURI, visa za kusafiria kwenda nchini Israel na hati za kusafiria za wafanyakazi hao, na akasema wanavyo vyeti vya kuhitimu mafunzo, ingawa nakala za vyeti hivyo au kikonyo za pasi ya kupandia ndege kwenda au kurejea kutoka nchini Israel hakuwa navyo mikononi akaahidi kuwa atawaonyesha waandishi wa gazeti hili mara tu vitakapokabidhiwa kwake na watumishi husika.

Amesisitiza kuwa watumishi hao walikwenda masomoni kati ya Juni 23 na Julai 13, 2015 baada ya awali kuwa wameaihirisha masomo yao, ambapo mtumishi mwingine Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Bajeti, ambaye sasa ni Mratibu wa Mafunzo ya Wabunge, Elisa Mbise yeye alikwenda kwenye mafunzo hayo bila kuahirisha.

 

Posho ya Sh 250,000 kwa siku

JAMHURI liliripoti kuwa watumishi wa ofisi ya Bunge wanalipwa posho ya Sh 150,000 hadi Sh 250,000 kila siku bila kujali wapo ofisini au wamesafiri. Yakub amesema posho hii iliwahi kulipwa ila ililipwa au inalipwa katika mazingira maalum tu. “Unakuta kwa mfano Mhe Spika yupo Marekani, wakati kule ni mchana, huku inakuwa usiku, inamlazimu mfanyakazi kulala ofisini akiwezesha mawasiliano kutoka Tanzania kwenda Marekani… hivyo posho hii inalipwa katika mazingira maalum tu si wakati wote,” anasema Yakub.

Mwisho, Yakub amesema wapo wafanyazi walikwisha katika baadhi ya kurugenzi na ukurugenzi wao umetenguliwa baada ya hoja ya kubana matumizi na kupunguza ukubwa wa muundo hivyo hao wameendelea kulalamika wakidhani wameonewa, lakini uhalisia ingependeza kama wangekubali mabadiliko hali itakayorahisisha utendaji na kuongeza ufanisi wa Bunge badala ya kupambana.

2352 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!