Hivi karibuni Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Angelina Mabula, ameonyesha ujasiri zaidi katika kuzibana taasisi na kampuni zenye madeni makubwa ya kodi ya pango la ardhi. Mpita Njia ama MN anatambua ukubwa wa tatizo hilo. Kwa mfano, Mwanza tu, kampuni na taasisi nane zinadaiwa zaidi ya Sh milioni 900.

Na katika ziara yake, Naibu Waziri Mabula alifika katika kampuni na taasisi kadhaa ambazo ni pamoja na Synergy Tanzania Ltd, Ideal Development Ltd, Birchard Oil Ltd, shule za Musabe, Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Ndamavyo Auto Spares, Jesse & Company Ltd na Maabara ya Taifa ya Udhibiti wa Samaki na Mazao ya Uvuvi.

MN akiwa katika shughuli zake za kawaida alimshuhudia naibu waziri huyo. MN alishuhudia mmiliki wa shule za Musabe ambazo ni za chekechea, msingi na sekondari akimweleza Dk. Mabula kuwa yuko tayari kulipa deni la kodi ya pango la ardhi lakini alishindwa kufanya hivyo kutokana na changamoto za kibiashara. Huyu ameahidi kulipa kiasi anachodaiwa kuanzia Agosti 2019 na kumaliza deni lote ifikapo Desemba 2019.

Akiwa katika Kampuni ya Birchard Oil Limited, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Mabula aliitaka kampuni hiyo kulipa kiasi inachodaiwa cha kodi ya pango la ardhi inayofikia Sh 85,235,050 ikiwa ni pamoja na malimbikizo ya kodi za miaka ya nyuma.

Meneja Uhusiano wa kampuni hiyo inayojishughulisha na uzalishaji wa mafuta na marobota ya pamba, Arshad Jetha, alimweleza Naibu Waziri wa Ardhi kuwa kampuni yake pamoja na kudaiwa kodi ya pango la ardhi kwa baadhi ya viwanja inavyomiliki lakini ilikwishalipa sehemu ya deni, kwa hiyo aliomba kuhakikiwa madeni yake ili kupata deni halisi.

Ideal Development Ltd kupitia Meneja wake Burnanuddin Rajbhai alikiri deni la kodi ya pango la ardhi linalofikia Sh milioni 79 na kuomba kupewa muda wa kulipa katika awamu tatu tofauti.

MN anakubaliana na uamuzi wa Naibu Waziri wa Ardhi kama alivyomshuhudia wa kuzitaka kampuni na taasisi zilizokubali kulipa madeni  kuandika barua ya kueleza namna zitakavyolipa na muda wa mwisho wa kulipa madeni yao katika ofisi za ardhi za halmashauri husika na nakala za barua hizo ziende Ofisi ya Kamishna Msaidizi wa Ardhi wa Kanda ya Ziwa.

Jambo moja la kiungwana ni kwamba serikali iwe na uvumilivu kwa wadaiwa hawa wanaokiri madeni yao na kuonyesha utayari wa kuyalipa kwa amani. MN anaamini ni busara zaidi serikali kuhakikisha wawekezaji wa aina hii wanaendelea na biashara zao ili kwanza iendelee kupata kodi, lakini pia mhusika apate uwezo wa kulipa deni la zamani. Huu ni uamuzi mzuri zaidi kuliko ule wa kufunga biashara.

713 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!