CCM chama tawala kilichoshindwa kutawala

Majuzi, aliyekuwa Spika wa Bunge la kumi la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Anne Makinda, alisema kwamba ushindi wa Rais Dk John Magufuli katika Uchaguzi Mkuu 2015 umenusuru Watanzania na machafuko.

Amesema kwamba machafuko yangeweza kutokea kutokana na tofauti kubwa ya kipato kati ya matajiri na maskini.

“Kuna watu walikuwa haifahamiki wanafanya kazi gani lakini mamilionea.” Hakuna asiyekubali kwamba Dk. Magufuli amelinusuru Taifa hili na machafuko. 

Kwa kweli, Spika mstaafu Anne Makinda ni mtu wa kupongezwa kwa kuona ukweli. Angesema kwamba ni Chama Cha Mapinduzi kilichonusuru  Taifa hili na machafuko, tungemwona Spika huyu mstaafu kuwa ni mtu asiyependa ukweli.

Si jambo zuri lakini ndiyo ukweli wa mambo. Usalama wa Taifa hili hautegemei chama tawala cha CCM. Unategemea kiongozi aliyepo madarakani. Akiwa mzuri Taifa linapona, akiwa mbovu Taifa linatafunwa.

Hii ni kusema kwamba Taifa la Tanzania haliongozwi kwa uongozi wa pamoja, kwa kifupi katika uongozi wetu kuna ombwe.

Ukifuatilia kwa karibu kazi ya utumbuaji majipu inavyofanywa na Dk. Magufuli utakubali kwamba Tanzania ilikuwa imeoza. Kwa kuwa ndani ya chama tawala hakuna uongozi wa pamoja, baadhi ya viongozi walikuwa wakilalamika kwenye majukwaa huku malalamiko yao yakipondwa na wenyeviti wao.

Tazama, tulikuwa na suala la mawaziri mizigo ambao Katibu Mkuu wa CCM na Katibu wake Mwenezi waliendelea kuwazungumzia mawaziri mizigo. Lakini Ikulu kwa niaba ya Rais ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa CCM, iliendelea kuwatetea.

Kwa kweli, CCM ya leo ni tofauti kabisa na CCM ya Mwalimu Nyerere – Mwenyekiti wa kwanza wa CCM. Kamati ya CCM ikikutana ilikuwa inazungumzia masuala muhimu ya Taifa yakiwamo elimu, afya, uchumi, siasa na kadhalika.

Katika vikao hivyo, CCM ilikuwa inatoka na sera na uamuzi wenye manufaa ya Taifa, huo ulikuwa uongozi wa pamoja. Lakini CCM ya leo ikikutana inazungumzia siasa tu hasa mapambano dhidi ya vyama vya upinzani.

Kwa hiyo, shule zimeendelea kukosa madawati, hospitali zimeendelea kukosa dawa na vitanda, mapigano yanaendelea kati ya wakulima na wafugaji, wanavijiji wameendelea kuporwa ardhi yao na wawekezaji, fedha za halmashauri zimeendelea kuliwa, na wachache wameendelea kugeuza fedha za umma kuwa fedha yao ya mfukoni.

Hayo yote yamekuwa matokeo ya kukosekana mfumo mzuri wa utawala wenye kutoa uamuzi wa pamoja. Kwa hiyo, usalama na ustawi wa Taifa hautegemei viongozi wa pamoja ndani ya chama tawala, unategemea una Rais wa namna gani.

Kwa kweli, mambo yanayotokea leo hayamwaminishi mtu yeyote kwamba bado chama tawala ni CCM. Utadhani kwamba hizi ni sera mpya za chama kipya cha upinzani.

Hakika ushindi wa Dk. Magufuli umenusuru Tanzania na machafuko. Si ushindi wa CCM ulionusuru Taifa letu. CCM imekuwako wakati wote huu wa Tanzania kuwa katika hali mbaya.

Lakini hapa tunalazimika kwenda mbele na mbali zaidi. Kinachoendelea kunusuru Taifa hili na machafuko ni upole na uvumilivu wa Watanzania ambao wameendelea kuwa wapenda amani. Watu wanasema ‘usione vyaelea, vimeundwa.’

Amani hii inayonusuru Taifa na machafuko, chimbuko lake ni Baba wa Taifa hili, Mwalimu Julius Nyerere. Tangu enzi za kupigania Uhuru wa Tanganyika, Mwalimu Nyerere aliwataka watu wa nchi hii wafanye mambo yao kwa kuzingatia amani. Tukafika mahali ambako Tanzania iliitwa kisiwa cha amani.

Katika nchi nyingine wapinzani wanapoona wanaporwa ushindi katika uchaguzi, kinachofuata ni machafuko. Lakini Tanzania ni jambo la kawaida Tume ya Uchaguzi kutumiwa kupora ushindi wa upinzani.

Tumefika mahali ambapo matokeo ya uchaguzi yaliyowapa ushindi wapinzani, yanafutwa hivi hivi na nchi inaendelea kuwa na amani.

Sasa basi, kwa kuwa usalama wa nchi yetu hautegemei uongozi wa pamoja wa chama tawala bali unategemea Rais aliyepo madarakani, kuna mambo ambayo lazima tufanye ili kuliokoa Taifa letu.

Kwanza kuboresha Katiba ya nchi yetu kwa lengo la kupunguza madaraka na uwezo wa Rais ili nchi iwe na uongozi wa pamoja. Pili, Rais asiishie kwenye kutumbua majipu ya kiuchumi tu. Pia atumbue majipu yanayohusiana na masuala ya siasa.

Tume ya Uchaguzi itumbuliwe na uongozi wa Rais Magufuli ili kauli kwamba ni Rais aliyepania kuliokoa Taifa letu iwe na maana. 

Taifa letu likiwa na uongozi wa pamoja na mfumo wa utawala wenye manufaa kwa Taifa zima, si kama tu tutanusuru Taifa letu na machafuko, bali pia Taifa letu litastawi.

Mwisho, nakumbusha kwamba kutawala ni kuwapa wananchi mahitaji yao muhimu kama maji na dawa. Pia kutawala ni kudhibiti uhalifu wa aina zozote. Kwa kuwa CCM imeshindwa kuwapa wananchi mahitaji yao muhimu pia imeshindwa kudhibiti uhalifu, basi CCM imekuwa chama tawala kilichoshindwa kutawala.