CCM iruhusu ushindani wa haki urais

4.+Nape+akihamasisha+kwenye+mkutano+huo,+Kushoto+ni+Mlezi+wa+mkoa+wa+Dar,+Abdulrahman+KinanaKwa wiki takribani nne hivi, sijaonekana katika safu hii. Sikuonekana kutokana na matatizo ya msiba, lakini pia nikalazimika kufanya kazi mikoani. Huku niliko nakumbana na tunachopaswa kupambana kukiondosha.
Sehemu nyingi za mikoani hakuna huduma ya data (Internet), simu zipo ila ukitaka kuingia kwenye Internet ili utume barua pepe ni sawa na kushuka mchongoma.
Yapo baadhi ya maeneo kuna mtandao, lakini hakuna umeme. Katika baadhi ya wilaya za Mkoa wa Kagera ninapokuwa vijijini kama Mfundize, Kilimilile, Rwambaizi Karagwe au Ihyolo Nyanga Bukoba Mjini najikuta simu yangu inatumika kwa wastani wa saa 12, nyingine nahemea umeme. Nashukuru nia njema ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera, John Mongela, na ufuatiliaji wake wa dhati, hali imeanza kubadilika.


 Nasema imeanza kubadilika kwani kwa muda mfupi aliofika mkoani hapa, ametoa mfano wa kuigwa kiutendaji. Mfano huu ninaoutoa ni halisi. Mwezi Januari mwaka huu, Mongela alikwenda Kata ya Nyanga kwenye chanzo cha maji Kanyamata. Alipofika akakuta nguzo za Wakala wa Umeme Vijijini (REA) zimesimamishwa na kutandazwa nyaya, lakini wakadai wananchi wa Nyanga hawawezi kupata maji kwani transfoma waliyopaswa kufungiwa imepelekwa Biharamulo.
Mongela alisimama kidete, akaamua kukaa eneo linaloitwa Darajani-Kilyabagole, akaagiza hiyo transfoma isafirishwe kutoka Biharamulo na kurejeshwa Bukoba kwa ajili ya kufungwa. Aliitisha kikao cha dharura hapo mtoni, akakaa kwa zaidi ya saa 4. Watendaji walipoona Mongela amedhamiria, wakaagiza transfoma hiyo iletwe, ikaletwa na kufungwa ndani ya siku mbili. Wananchi wa Nyanga wakaanza kupata maji na umeme.


Ni kwa bahati mbaya tu, kuwa umeme ule umepita Mtaa mmoja wa Nyarubanja, lakini Mtaa wa Ihyolo bado uko gizani. Nimepata kauli ya Mongela na hasa baada ya ujio wa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, kuwa anafanya juhudi kuhakikisha Mtaa wa Ihyolo nao unapata umeme.
  Nimetoa mfano huo mmoja tu, lakini ipo mingi ambayo Mongela anadhihirisha uongozi unaotaka kuona matokeo na si kauli za kuchakata michakato.
  Sitanii, kwa dhati kabisa nampongeza Mongela na nataraji hiyo nia yake ya kufikisha umeme Ihyolo, nayo itatekelezeka ndani ya muda mwafaka. Mara zote nchi hii imeelezwa kuwa maendeleo yanachelewa kutokana na usimamizi usio wa kuridhisha. Wakitokea akina Mongela wengi kama alivyosimamia maendeleo ya wananchi Kigoma na Arusha, nchi hii itakuwa katika nafasi nzuri ya kupiga hatua kubwa kimaendeleo.


  Nimelazimika kuanza na hoja ya Mongela ili kuweka msingi katika makala hii inayohusu urais. Utaniwia radhi msomaji wangu, orodha ya wataka urais imekuwa ndefu mno. Kwa wingi wao niruhusu niwaandike kwa jina moja tu kuokoa nafasi.   
  Nimesikia sasa wamefikia 28 wakiongozwa na Monica, Mahiga na Chikawe. Wapo pia Magufuli, Makongoro, Muhongo, Sumaye, Mwigulu, Membe, Mwandosya, Wasira, Sitta, Lowassa, Pinda, Ngeleja, Nyalandu, Kamani, January, Karume, Kigwangalla, Amina, Mpina, Bilali… orodha ni ndefu na pengine wakati tunakwenda mitamboni wataongezeka wengine. Hii ni rekodi ya aina yake.
 Sitanii, binafsi nimepata wasiwasi. Nimepata shida kuwa huenda kazi ya urais imeanza kuwa rahisi. Kwamba mwaka 1995 walijitokeza 12, mwaka 2005 wakajitokeza 11 ndani ya CCM na mwaka huu taarifa nilizonazo watangaza nia watafikia 32. Napata taabu kama waliojitokeza wote wanafahamu kuwa kazi ya urais ni utumishi kwa wananchi.


  Napata shida kwa sababu hata baadhi ya wanafunzi nasikia wanatangaza nia. Nakubaliana na hoja kwamba urais hauna chuo, lakini uzoefu na maarifa ni vya msingi. Mawili hayo yanaweza kupatikana kupitia darasani au utumishi wa muda mrefu. Huhitaji kuwa na mambo hayo kama unatokea msituni. Na hatutakuwa na muda mrefu kushuhudia yanayotokea Burundi, ambako Pierre Nkurunziza aliingia madarakani akiwa na miaka 40.
  Wapo wanaosema alikuwa anafundisha chuoni, ndiyo, lakini la pili maarifa yaliyoambatana na uzoefu wa uendeshaji wa serikali kwake ilikuwa sifuri. Zipo hoja kuwa Rais Barak Obama wa Marekani alikuwa hajapata kuwa hata waziri, lakini wanasahau kuwa alikuwa Seneta wa Illinois, cheo ambacho ni kikubwa pengine kuliko marais wengi wa Bara la Afrika.


Sitanii, kwa utitiri wa wagombea napata shaka kama haudhalilishi taasisi ya urais. Nimeanza kusikia mawazo ya hatari. Wapo watangaza nia wanaokiri kuwa wao kama wao hawana uwezo, ila wanasema urais ni taasisi. Wameanza kutoa kauli za kwamba ukigombea urais vipo vyombo vya dola unavyoshirikiana navyo kuongoza nchi, hivyo unahitaji tu kuwa rais, mambo mengine yatakwenda.
Kuna kauli nisizoweza kuzisahau maishani mwangu. Mwanasheria Mwandamizi, Mabere Marando, alipata kutoa kauli kuwa “Tanzania ni nchi yenye bahati na Mwenyezi Mungu anaipenda.” Akaongeza kuwa “Ni nchi pekee duniani inayoweza kujiongoza bila rais kwa kipindi kirefu.”
  Mimi sitaki kushiriki kauli hii na wala sijui Marando alifikiri nini kutoa kauli kama hii wakati muda wote tunaye rais aliyechaguliwa kwa awamu ya nne sasa. Lakini nikiwaza kwa sauti (loud thinking) naweza kuona mantiki katika kauli ya Marando. Naiona mantiki kwa maana kwamba nchi hii haitendewi haki kuwa na rais ambaye wizara au mkoa unaweza kupangiwa bajeti ya Sh bilioni 10 ukaishia kupata asilimia 20, yaani bilioni 2 katika mwaka wote wa fedha.
Tunahitaji rais ambaye atafika mahala tukajenga viwanda vya kuzalisha dawa za msingi za magonjwa tunayofahamu kuwa tunayo kwa muda mrefu, na yataendelea kuwapo, kama malaria, badala ya kutegemea fedha za wafadhili kutulipia dawa za magonjwa karibu yote hapa nchini. Ndugu zangu, inawezekana hamlijui hili. Leo, Tanzania inategemea wafadhili kwa karibu asilimia 98 kwa dawa zote tunazotumia katika hospitali zetu.


Tunahitaji rais atakayeona soko la bidhaa kama pikipiki kuwa badala ya kuendelea kununuliwa kutoka China, basi tuwalete Wachina wajenge kiwanda hapa nchini, vijana wetu wanunue pikipiki kwa shilingi za Kitanzania na ikibidi tuuze nje ya nchi pikipiki kama wafanyavyo Wachina.
Sitanii, tunao uwezo wa kuondokana na unyonge wa kutegemea wafadhili katika mambo yaliyo ndani ya uwezo wetu. Naona aibu kuona miti yote tuliyojaaliwa nayo hapa nchini, bado Serikali inatembeza bakuli kwa wafadhili kuomba madawati na kuchimbiwa vyoo shuleni. Tunahitaji rais anayeweza kuagiza, utekelezaji ukawapo kwa kujenga shule au kutengeneza madawati, tena kwa bei za kiungwana.


Wiki iliyopita, nilikuwa nazungumza na mtendaji mmoja. Akaniambia ujenzi wa chumba cha maabara unagharimu Sh milioni 56. Nikamuuliza nyumba yake ameijenga kwa shilingi ngapi? Akasema bei ya chumba cha maabara ni kwa mujibu wa ‘BOQ’ ya Halmashauri ya Mji wake. Nikakumbuka, sisi tulisomba matofali kujenga shule ya msingi nilikosomea, na madarasa tuliyojenga tangu mwaka 1979 hadi leo yapo na hayana nyufa. Nenda kwenye hayo yaliyojengwa kwa ‘BOQ’ uyaangalie na uniambie kama yatakuwapo miaka miwili ijayo.
Narudia, tunahitaji rais atakayesimamia thamani bora ya matumizi ya fedha zetu. Tunahitaji rais atakayefikiria na kurejesha uchumi wa viwanda vidogo vidogo, viwanda vya kati na vikubwa. Tunahitaji kurejea katika fikra za kuwezesha wazawa. Si aibu Tanzania kuanzisha mpango mahususi wa kuwezesha wazawa kwa kuwapa mitaji.


Bila rais kuanzisha mchakamchaka wa kujenga uchumi kwa kuwezesha wazawa kumiliki viwanda, wakazalisha bidhaa zenye thamani na kuuza nje, tena wa dola, tutaishia kwenye majungu.  Tatizo la ajira lilivyogeuka wimbo wa Taifa… kama hatuna ndoto za kuwekeza katika viwanda hata tukijenga vyuo vya ufundi na kuanzisha vyuo vikuu, hawa hawatakuwa na pa kwenda kufanya kazi baada ya kuhitimu.
  Uchumi wa Japan ulikua baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia pale walipoamua kuwekeza katika viwanda vidogo vidogo na vya kati. Kila aliyekwenda na wazo, serikali ilimwezesha kifedha na kumwekea usimamizi kwa utaratibu wa kukagua utendaji wake mwaka hadi mwaka. Kinachotakiwa si kuwapa mikopo wajasiriamali halafu kusiwe na ufuatiliani wa ‘wapo wapi na wanafanya nini’.


  Chini ya uongozi wa Awamu ya Kwanza wa Mwalimu Nyerere walikuwapo maafisa mifugo na maafisa ugani (kilimo), hawa walipita katika mashamba ya wananchi vijijini kuwashauri nini waongeze au wapunguze katika mashamba na mifugo yao. Matokeo ni kuwa mazao bora yaliongezeka, na mauzo nje ya nchi yakaongezeka pia. Leo, kila mtu anakwenda kivyake.
Sitanii, kwenye kichwa cha makala hii napendekeza uwanja sawa wa ushindani katika mbio za urais. Nimeanza kusoma alama za nyakati. Kuna maandalizi ya mizengwe katika uchaguzi lakini si kupitia CCM pekee bali hata kwa vyama vya upinzani. Nimeanza kusikia UKAWA wanavyoparurana kwenye makundi ya WhatsApp. Hawaridhiki nani achukue jimbo lipi. Hofu yangu ni kuwa wanaweza kuamua kugawana mbao wakati wapo katikati ya Bahari ya Mamba!
Kwa CCM napata shida kama watapata mgombea mzuri. Badala ya kuwapima wagombea wao kwa mikakati yao ya kukuza uchumi wa Taifa letu, kigezo sasa kimekuwa ufisadi, rushwa na historia za ‘kubumba’ za watu. Wanachafuana kwenye mitandao ya kijamii usipime. Wenye historia za kweli za kula (kutoa au kupokea) rushwa kama Stephen Wasira wanajifanya ni malaika.


Kibaya zaidi, wengi wameonesha nia wakiwa bado kwenye vikao vya uamuzi. Mfano ni Wasira, Dk. Bilal, Pinda na wengine. Hawa sijajua ushiriki wao utakuwaje wakifikia ajenda za kujadili wagombea. Mwigulu Nchemba anastahili pongezi katika hili. Amejiuzulu unaibu katibu mkuu kuepuka mgongano wa maslahi katika vikao vya Kamati Kuu. Wengine msamiati huu hauwahusu?
  Narudia, ushindani wa haki utafuta mizengwe. Utaepusha nchi yetu na balaa la chuki. Makundi na ushabiki wakati wa uchaguzi si jambo baya. Huwezi kuchagua au kuchaguliwa kama huna wanaokuunga mkono, mnaozungumza lugha moja na hayo ndiyo makundi. Tatizo ni pale baadhi ya wachezeshaji (refarii) wanapokuwa sehemu ya makundi hayo. Mchezo unanoga pale timu mbili au zaidi zinapopambana na marefarii wakabaki kufanya kazi ya urefarii.


  Sitanii, safari ya mwezi mmoja na zaidi kabla ya kufikia Julai 12 atakapotangazwa mgombea wa CCM, tuandae masikio na macho yetu kushuhudia mengi. Kikubwa ninachosema ni kuwa kila atakayekwambia ubaya au uzuri wa mgombea usisite kumuuliza sababu. Inawezekana mtu anakuelekeza kwa mgombea fulani, kwa sababu tu amepewa doti ya khanga, hivyo anataka nawe ushiriki rushwa yake.


Mimi nasema vyama vyetu vinapotaka kutuletea wagombea, vituletee wagombea watakaozungumzia uchumi wetu. Kauli tamu tumezichoka. Tunahitaji kiongozi anayeishi maneno yake. Utekelezaji ni lazima uwe na muda, si sisi kuelezwa kauli ya mchakato unaendelea hadi siku ya kiama.
Tunahitaji rais shupavu, anayeweza kujenga uchumi na ambaye kauli yake inatekelezeka. Tusiidharau historia. Kama mtu alipewa fursa akashindwa kutenda lolote, tusitaraji kuwa akipewa urais malaika watamshukia kutoka mbinguni. Ni lazima tumpime kwa kigezo cha ‘aliwahi kufanya nini?’ Huu si wakati wa kufanya majaribio ya uongozi Ikulu. Mungu ibariki Tanzania.