Mbunge wa Mbozi Magharibi, David Silinde (Chadema) mwanzoni mwa mkutano wa Bunge unaoendelea sasa, alizungumza maneno ya hekima.

 

Akieleza safari ya kifo cha Chama Cha Mapinduzi (CCM) alifananisha hali hiyo na tajiri anayefilisika. Akasema tajiri anayefilisika huwa hajitambui, na kwamba akijitambua kuwa anafilisika, kamwe hatafilisika. Hatafilisika kwa sababu atajitahidi kutafuta mbinu za kujikwamua. Akasema kwa hali ya mambo ilivyo, CCM haijitambui kama inakufa, na kwa sababu hiyo, inakufa!

Maneno haya ni mazito. Wana-CCM wa kweli wanapaswa kuyatumia kama maono wanayopewa na mmoja wa watu wanaoona mwenendo wa CCM kuwa si mzuri. Unaweza usikubaliane na Silinde kwa sababu ni mwana-Chadema. Unaweza usikubaline naye kwa sababu una umri mkubwa kumzidi, na kwa tabia ya Mwafrika kuikubali busara ya mtoto mdogo wa rika la Silinde ni jambo gumu kweli kweli.

 

Nikitazama mijadala inayoendelea ndani ya Bunge, huwezi kuwa mbali na ukweli aliousema Silinde. Kwa bahati mbaya ni kwamba anayekuwa na mtazamo tofauti, daima ameitwa mpinzani wa CCM.

 

Hoja za wabunge wa upinzani: Wabunge hawa wameibua hoja nyingi na za kufikirisha sana. Pamoja na uzito wake, bado wabunge wa CCM na Serikali ya chama hicho wameendelea kuzipuuza. Nitajaribu kuziainisha kwa uchache sana.

 

Kuliibuliwa hoja ya mfanyabiashara Mohsin Abdallah kukaribisha kampuni ya kuendesha utafiti na hatimaye kuchimba madini ya urani katika vitalu alivyopewa kwa ajili ya uwindaji wa kitalii. Hoja hiyo ilitolewa na Halima Mdee (Chadema).

 

Mfanyabiashara huyo ambaye ni mmoja wa wafadhili wakuu wa CCM, kwenye mkataba wake na kampuni ya utafiti wa urani, wamekubaliana alipwe dola milioni sita. Dola moja ya Marekani ni wastani wa Sh 1,580. Malipo hayo ni mbali kabisa na mengine manono. Wakati akilipwa hivyo, masikini wanavijiji wenye eneo la uwindaji kwa wingi wao wanaambulia dola 10,000 tu. Dhulma iliyoje!

 

Kwa namna yoyote ile, hoja hii ilipaswa iitikise Serikali. Ilipaswa iwafumbue macho viongozi wetu. Lakini hata wakati wa kuhitimisha hoja, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, hakuigusa kabisa hadi pale alipokumbushwa na Mdee. Fikiria, madini hatari ya urani yanachimbwa na kampuni iliyoingia mkataba na mtu binafsi, Serikali inaambiwa haishituki! Nani kawaloga hawa viongozi wetu?

 

Hoja ya pili. Hoja hii ni ile iliyotolewa na Mbunge wa Musoma Mjini, Vincent Nyerere (Chadema). Ilihusu dola zaidi ya milioni 700 zilizotolewa na Benki ya Dunia kwa Wizara ya Maji. Mtandao wa Benki hiyo unaonyesha kuwa fedha hizo zilishaanza kutolewa tangu mwaka 2007 (dola milioni 200), lakini hakuna mahali zinapoonekana kwenye vitabu vya Serikali. Fikiria, dola milioni 700! Hizi ni fedha nyingi mno. Tulitarajia kuwa Serikali yenye watu ambao bongo zao zinafanya kazi vizuri, wangeshitushwa na habari hizi, kisha wakachukua hatua.

 

Hoja ya tatu. Spika Anna Makinda ambaye ni kada wa CCM, pamoja na Naibu Spika, Job Ndugai, pamoja na wenyeviti wote wa Bunge, wanaonekana wazi kuwabana wapinzani – hawa ni wale wa vyama vya upinzani na hata kutoka ndani ya CCM. Sasa wanasaidiwa sana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye kimsingi wajibu wake ni kusaidia kutoa mwongozo/ufafanuzi wa kisheria bungeni, lakini sasa amekuwa kada wa CCM mwenye kuwabeza wapinzani!

 

Hoja za wapinzani hazipewi nafasi hata pale ambako kwa akili ya kawaida kabisa mtu unaweza kuona mashiko ya hoja hizo. Kwa mfano, kuzuiwa kwa nguvu zote kujadiliwa kwa suala la Dk. Stephen Ulimboka, kabla hata ya jambo hilo kufikishwa mahakamani, kumeuthibitishia umma kuwa CCM hawako karibu na wananchi.

 

Kuzuia suala la madaktari kujadiliwa bungeni, huku wananchi makabwela wakiendelea kukata roho kutokana na mgomo wa madaktari, ni jamho jingine ambalo utake usitake utakubaliana na Silinde kwamba CCM inayokufa haijitambui kuwa inakufa!

 

CCM hawana hatimiliki ya kuliongoza taifa hili milele. Mara zote ilijihami kwa kutumia nguvu za dola, lakini matokeo ya uchaguzi unaohusisha jamii nzima unaonyesha kuwa hata huko kwenye vyombo hivyo, CCM watu wameichoka. Matokeo ya kura kwenye kambi za Jeshi, Polisi, Magereza na kadhalika, ni mabaya kwa CCM. Hili si jambo la kificho.

 

Hoja ya nne: Kitendo cha viongozi wa Bunge wiki iliyopita kusita kuahirisha Bunge baada ya taarifa za msiba mkubwa uliosababishwa na ajali ya meli Visiwani Zanzibar, kimewafanya wenzetu wa upande wa pili waamini kuwa kweli Muungano huu inawezekana ukawa hauna umuhimu tena. CCM wamerahisisha safari ya kuua Muungano kwa kukataa kujiona sehemu ya waliofikwa msiba!

 

Wabunge wakaomba muda kujadili ajali hiyo, wakakataliwa. Kibaya zaidi walikataliwa kwa utetezi dhaifu kutoka kwa viongozi wa Bunge. Wabunge wanasema jamani tuna msiba, tuahirishe walau kwa siku zaidi ya moja vikao vya Bunge ili tushiriki pamoja majonzi na ndugu zetu wa Zanzibar. Kiti cha Spika kinazuia maombi halali ya aina hii. Hii ni petroli katika hoja ya Uamsho ya kuuvunjilia mbali Muungano huu.

 

Hoja ya tano: Kambi ya Upinzani imeibua ufisadi wa kushangaza unaomhusu Mbunge wa Viti Maalumu, Mama Anna Abdallah (Mwenyekiti wa Bodi ya Korosho) na wajumbe wenzake wa Bodi hiyo kujilipa Sh milioni 7 kwa siku moja.

 

Malipo hayo si hoja. Hoja ipo kwenye aina ya malipo. Mbunge mwingine Jerome Bwanausi kalipwa mara mbili kwa kutumia majina, “Jerome Bwanausi, na J. Bwanausi”. Amechotewa mamilioni ya shilingi. Mjumbe mwingine wa Bodi kalipwa sawa sawa na mkewe ambaye si mjumbe wa Bodi.

 

Mama Anna akajitetea bungeni kwa kusema yule mama (ambaye ni mjumbe wa bodi), alilipwa kama msaidizi wa mmoja wa wajumbe ambaye ni mlemavu! Je, huu kweli ndiyo utetezi wa mtu mzito kama huyu kwa matumizi ya fedha za umma? Kama Mama Anna ambaye amelitumikia taifa hili kwa muda mrefu anaweza kubariki mambo ya aina hii, hivi kuna sababu ya kuendelea kuwaheshimu watu wa aina hii?

 

Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika alipojibu hoja, hakugusia kabisa wizi huo. Akajifanya hayamhusu. Jambo kubwa na zito kama hili, kashfa nene kiasi hiki inaachwa ipite hivi hivi tu! Je, ni kwa sababu waliokula fedha hizo wote ni wana-CCM? Je, ni kwa kuwa Mama Anna ni mke wa Mzee Msekwa ambaye anakalia kiti kizito ndani ya CCM? Kwa matukio haya, mwananchi gani ataiamini CCM kwamba inaipiku Chadema katika mapambano dhidi ya ufisadi?

 

Ndugu zangu, Mbunge wa Kigamboni, Dk. Faustine Ndungulile, alifukuzwa bungeni kwa sababu ya msimamo wa kutetea wananchi wake wanaopokwa ardhi kinyume cha sheria. Alijaribu kuonyesha namna sheria ilivyokiukwa kwa mradi huo. Kweli madudu mengi hayakufanywa na Profesa Tibaijuka wala Katibu Mkuu, Patrick Rutabanzibwa. Yalifanywa na watangulizi wao.

 

Pamoja na ukweli huo, bado dhima ya viongozi hao wapya katika kurekebisha kasoro inabaki pale pale. Kukiri udhaifu wakati mwingine ni jambo la kiungwana. Lakini Ndugai kwa kuona Dk. Ndungulile ataleta shida wakati wa upitishaji bajeti, akaamua kumfukuza asihudhurie vikao vitatu vya Bunge! Uamuzi ule ulitazamwa na wananchi wa Kigamboni na kwingineko ambako dhuluma za ardhi zimefanywa. Hakika, wananchi hao hawawezi kuwa wafuasi wa CCM.

 

Nimejaribu kuainisha haya machache katika kuonyesha kuwa kauli ya Silinde ina maana kubwa sana kwa CCM. Wanaokipenda chama hiki wanapaswa kuamka na kutafakari mwenendo wao kama kweli una mbolea katika uhai mzima wa chama hicho.

 

Lakini Waswahili walisema sikio la kufa halisikii dawa. Siku ya kifo cha nyani kila mti huteleza. La kufunda halina ubani. Kuna dalili zote kwamba CCM inajimaliza yenyewe. Hoja nzito zinazolihusu taifa zinapopuuzwa na viongozi wa CCM, hiyo inakuwa tija kubwa kwa wanasiasa wa kambi ya upinzani.

 

Kuna hadithi ya kwamba chunusi – yule kiumbe wa baharini – akimhitaji mtu, huyo mtu analazimisha kujipeleka mwenyewe baharini. Hata kama atazuiwa au kuonywa kwa nguvu kiasi gani, mwisho wa siku huyo mtu atakwenda tu baharini. Na huko akishaenda atanaswa na huyo chunusi. Atakufa.

 

CCM ni kama wameitwa na chunusi. Kila wanapoonywa na kuhadharishwa, hawasikii wala hawaheshimu maonyo. Wameitwa. Wamenuia lazima waende, na kwa sababu hiyo ni lazima wafe! Lini watakufa? Hilo ni jambo la kusubiri tu. Tunayasema haya ili siku moja tusiwe upande wa watakaohukumiwa kwa kushindwa kuiamsha CCM inayokufa ili ijue inakufa na kwa sababu hiyo isiweze kufa!

1156 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!