CECILIA PETER: Mwanamke dereva jasiri wa bodaboda

* Akerwa na watekaji, waporaji wa pikipiki

Ni saa 11 jioni nawasili katika Kituo cha daladala cha Kibamba, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam. Ni umbali wa kilometa 30 kutoka katikati ya jiji hili. Hapa nakutana na mwanamke anayeitwa Cecelia Peter. Ninagundua haraka haraka kuwa mama huyu ni maarufu katika eneo hili na maeneo jirani.

Lakini kumbe umaarufu wake umetokana na shughuli anayoifanya ya kumwingizia kipato, ya udereva wa pikipiki ya abiria, maarufu kwa jina la bodaboda.

 

Ananipakia kwenye pikipiki yake hadi sehemu ya jirani panapoitwa Kibamba Hosipitali. Hapa sasa ndiyo kijiwe chake anapoegesha bodaboda katika harakati za kutega abiria.

 

Nakutana na vijana tofauti ambao pia ni madereva wa bodaboda. Wanampa sifa lukuki kutokana kile kinachoonekana kuwa ni ujasiri alionao wa kuamua kufanya kazi, ambayo ni nadra kukuta mwanamke anaifanya.

 

Sikutaka kusikia ya kuambiwa, nilimwambia anipakie kama abiria ili tutembee maeneo kadhaa jirani na kijiweni kwake huku tukipitia barabara kuu. Ama kweli kuna kila haja kwa wanawake wengine kujifunza kutoka kwa Cecilia.

 

Mwendo wake na hata jinsi anavyopishana na magari makubwa inadhihirisha kuwa mama huyu ana uwezo kuwazidi hata wanaume katika kumudu uendeshaji wa pikipiki.

 

Baada ya kushuhudia hayo machache kwa macho na kusikia mengi kutoka kwa baadhi ya watu pale maskani yake wakimpa sifa nyingi, nilitaka kujua kwa mapana zaidi kuhusu historia yake. Hali kadhalika kujua ujasiri huo aliupata wapi hadi kufikia alipo. Maongezi yetu yalikuwa kama ifuatavyo:

 

JAMHURI: Nipe historia fupi ya maisha yako.

Cecilia: Mimi nilizaliwa Arusha. Baba yangu ni Mnyaturu na mama yangu ni Mnyamwezi. Tulihamia hapa Dar es Salaam mwaka 2000 baada ya baba kufariki. Kutokana na kifo cha baba yangu pia nilishindwa kuendelea na elimu ya sekondari ambapo niliishia kidato cha pili.

 

Nina umri wa miaka 33 na nimeolewa. Mume wangu anaitwa Abuu Mkumba. Nina watoto wanne – Kelvin mwenye umri wa miaka 12, Emmanuel (9), Mapesa (7) na Shakira mwenye umri wa mwaka mmoja. Wote wanasoma isipokuwa wa mwisho ambaye bado mdogo.

 

JAMHURI: Ilikuwaje hadi ukawa dereva wa bodaboda?

Cecilia: Kwanza kabla ya hapo mume wangu alikuwa na bodaboda na ndiye aliyenifundisha kuendesha pikipiki. Baada ya muda mume wangu aliachana na biashara hiyo na kuanza kujishughulisha na kilimo. Mimi nikawa sasa napenda kuendesha pikipiki. Ukweli napenda kuendesha pikipiki.

 

Nakumbuka kipindi fulani niliendesha hadi mimba yangu ikafikia miezi sita, kila mtu akawa ananishangaa. Hadi sasa hapa unaponiona nachukua pikipiki kwa tajiri kila mwisho wa wiki nampelekea hesabu yake na mimi nabaki na changu, maisha yanasonga mbele.

 

JAMHURI: Hesabu ya tajiri ni shilingi ngapi kwa wiki?

Cecilia: Hesabu ya tajiri ni 50,000/- kwa wiki, lakini pia kwa wale wanaopeleka kwa siku huwa ni 7,000/-.

 

JAMHURI: Wewe ni mama wa familia, unawezaje kugawa muda wako na kazi hii?

Cecilia: Kwa kawaida naamka asubuhi mapema, nawaandaa watoto. Kuna wale wanaoenda shule asubuhi na wengine mchana. Kwa sababu biashara yangu ipo karibu na nyumbani, basi hata ikifika saa sita hivi narudi nyumbani napika haraka haraka alafu narudi kijiweni. Nafunga biashara saa 12 jioni.

 

JAMHURI: Kuna changamoto gani katika biashara hii ya bodaboda?

Cecilia: Changamoto ziko nyingi – nzuri na mbaya. Kwa mfano, kuna ile ya watu kunishangaa kila wanaponiona nikiendesha bodaboda. Lakini mshangao huu ni katika hali ya kunifurahia kwani ni akina mama wachache ambao wanaweza kuendesha bodaboda kama ninavyofanya. Nafikiri unakumbuka wakati nimekupakiza wewe kule barabarani watu walikuwa wananishangaa.

 

Lakini changamoto kubwa katika biashara hii ni hawa majambazi wanaowakaba vibaka na kuwanyang’anya pikipiki. Tena katika mitaa yetu huku wanauawa mchana kweupe. Nikifikiria hili kuna wakati natamani kuacha kazi hii ila maisha yenyewe hayajakaa vizuri.

 

JAMHURI: Wewe ukiwa dereva mzoefu wa bodaboda, unafikiri ni staili gani ambayo inatumiwa sana na hao wanaowateka nyie?

Cecilia: Siku hizi kuna staili ambayo inatumika sana. Anakuja dada mzuri anajifanya anaongea na simu pale mnapopaki pikipiki zenu. Kumbe anaangalia pikipiki mpya au nzuri. Anajifanya anaongea na simu kama vile kuna mtu anamuelekeza sehemu ili amfuate.

 

Baada ya hapo anakodi pikipiki, mkifika sehemu anajifanya pochi yake imedondoka. Ukisimama tu unaona jamaa wanatokezea na kukufanyia uhalifu wa kukudhuru na kukunyang’anya bodaboda na pengine kukuua. Wakigundua umewafahamu wanakuua.

 

JAMHURI: Una muda gani unafanya kazi hii? Je, uliwahi kupata ajali ya aina yoyote?

Cecilia: Huu ni mwaka wa tatu niko barabarani, sijawahi kupata ajali ya aina yoyote. Hii ni kutokana na umakini wangu ninapokuwa naendesha pikipiki. Japokuwa ajali haina kinga lakini kuna ajali nyingine za kujitakia. Utakuta mtu anashindana na magari makubwa eti anataka kulipita. Hivi injini ya gari na pikipiki ipi kubwa? Hivi ndiyo vyanzo vya ajali nyingi za bodaboda.

 

JAMHURI: Wateja wako ni wa aina gani?

Cecilia: Kusema ukweli, wateja wangu wengi ni wanaume, na hii inatokana na kuwa wanaume wengi wanaamini madereva wa kike hata katika magari.

 

JAMHURI: Nini matarajio yako ya baadaye?

Cecilia: Siku zote matarajio ni mengi lakini kuna changamoto nyingi ili kufikia matarajio. Mimi kuna wakati natamani kumiliki gari, na hasa natamani kufanya biashara ya teksi na kuachana na hii ya bodaboda. Lakini najua yote mipango tu, kuna siku Mungu atashusha baraka zake mambo yatakaa sawa.

 

JAMHURI: Ndugu zako, akiwamo mama yako mzazi wanakuchukuliaje?

Cecilia: Kawaida, ila wananiona kama mwanamke jasiri. Kuna dada yangu ambaye ninamfuata kwa kuzaliwa nilimfundisha na sasa anajua kuendesha. Mtoto wangu wa kwanza pia anapenda kuendesha pikipiki. Mara nyingi nikipaki huwa nakuta anadandiadandia, ila bado mdogo, akikua nitamfundisha.

 

JAMHURI: Je, unaweza kuendesha gari?

Cecilia: Ndiyo najua kuendesha gari na hata kama nikipata magari makubwa naweza pia kuendesha. Kuna wakati huwa nafikiria kutafuta kazi hata katika magari makubwa, sema kwa hali ya sasa hivi kama humjui mtu ni ngumu sana kupata kazi sehemu yoyote.

 

JAMHURI: Kitu gani kinakupa moyo hadi unajiaminisha kutaka hata kuendesha magari makubwa?

Cecilia: Jibu ni fupi, kujiamini na kitu ninachokifanya. Kwa kawaida sisi wanawake tumekuwa tukidharaulika katika jamii na kuonekana kuwa hatuwezi kufanya baadhi ya kazi. Ninaamini kuwa mwanamke akiamua kufanya kitu kwa nguvu moja anafanya na anaweza.

 

JAMHURI: Una ujumbe gani katika jamii?

Cecilia: Hawa jamaa wanaowateka madereva wa bodaboda wasakwe na kama ikiwezekana Serikali iimarishe ulinzi na hatimaye kukomesha tabia hizi ambazo ni tishio kwetu. Haya ndiyo maisha yetu na tunapata riziki kupitia kazi hii kwa hiyo wanaotuteka wadhibitiwe kwa nguvu ya hali ya juu.