CHADEMA: Tunataka Serikali tatu – 2

Wiki iliyopita tulichapisha sehemu ya kwanza ya maoni ya Chadema kwa Tume ya Marekebisho ya Katiba. Sehemu ya kwanza iliahidhi kuwa sehemu ya pili ya mapendekezo haya itaanzia kwenye mtazamo wa Chadema juu ya uwapo wa Serikali ya Tanganyika. Endelea…

D. SERIKALI YA TANGANYIKA

1. Kutakuwa na Rais wa Tanganyika ambaye atakuwa Mkuu wa nchi na Mkuu wa Serikali ya Tanganyika.

2. Rais wa Tanganyika atakuwa na mamlaka na atatekeleza madaraka yote ya Serikali ya Tanganyika juu ya mambo yote yanayohusu Tanganyika.

 

3. Madaraka ya Serikali ya Tanganyika yatatekelezwa ama na Rais mwenyewe moja kwa moja au kwa kukasimu madaraka hayo kwa mawaziri ambao hawatazidi kumi na nane na hawatapungua kumi na tano au kwa watu wengine wenye madaraka katika utumishi wa Serikali ya Tanganyika kama itakavyowekwa katika sheria iliyotungwa na Bunge.

 

4. Madaraka ya Serikali ya Tanganyika katika majimbo yatatekelezwa na Serikali za majimbo zilizochaguliwa na wananchi wa majimbo husika na halmashauri za Serikali za mitaa katika majimbo hayo.

 

5. Rais wa Tanganyika atakuwa na mamlaka ya kuteua mawaziri wasiopungua kumi na tano na wasiozidi kumi na nane pamoja na manaibu mawaziri lakini uteuzi huo utapaswa kuthibitishwa na Bunge la Tanganyika baada ya utaratibu wa wazi wa kusikiliza maoni ya wadau (confirmation hearings).

 

6. Rais wa Tanganyika atateua watu wengine katika utumishi wa Serikali ya Tanganyika katakana na mapendekezo atakayopelekewa na tume huru za kitaalamu kama itakavyoelekezwa na sheria mahsusi iliyotungwa na Bunge la Tanganyika lakini uteuzi huo utapaswa kuthibitishwa na Bunge la Tanganyika.

 

7. Rais wa Tanganyika atakuwa na mamlaka kutangaza hali ya hatari kutokana na matukio au maafa yasiyotokana na nchi ya Tanganyika kuwa au kuingia vitani na nchi nyingine au kikundi cha watu ndani ya nchi ya Tanganyika.

 

8. Rais wa Tanganyika atakuwa na uwezo wa kutoa msamaha kwa watu waliopatikana na hatia na kuadhibiwa na mamlaka za utoaji haki za Serikali ya Tanganyika lakini uwezo huo utatekelezwa baada ya kupokea mapendekezo ya mamlaka zenye madaraka ya kusimamia urekebishaji wa tabia za wahalifu za Serikali ya Tanganyika.

 

9. Rais wa Tanganyika hatakuwa na kinga dhidi ya mashtaka ya jinai na madai kwa kosa ama jambo lolote atakalolitenda wakati akiwa Rais wa Tanganyika lakini mashtaka ya jinai yataendeshwa dhidi ya Rais baada kwanza Bunge la Tanganyika kupitisha azimio la kumwondoa Rais madarakani na endapo hoja ya kumshtaki itatolewa na kupitishwa na Bunge hilo.

 

10. Rais wa Tanganyika hatakuwa na mamlaka ya kutangaza vita wala kutangaza hali ya hatari isipokuwa kutokana na majanga, maafa au matukio yasiyokuwa ya kijeshi.

E. TAWALA ZA MAJIMBO NA SERIKALI ZA MITAA

1. Nchi ya Tanganyika itagawanywa katika maeneo kumi ya kikanda yatakayojulikana kama Majimbo kama ifuatavyo:

 

(a) Jimbo la Nyanza Magharibi ambalo litaundwa na mikoa ya sasa ya Kagera, Geita na Shinyanga;

 

(b) Jimbo la Nyanza Mashariki litakaloundwa na mikoa ya sasa ya Mara, Mwanza na Simiyu;

 

(c) Jimbo la Ziwa Tanganyika litakalojumuisha mikoa ya sasa ya Kigoma, Katavi na Rukwa;

(d) Jimbo la Kati litakaloundwa na mikoa ya sasa ya Tabora, Singida, Dodoma na Iringa;

 

(e) Jimbo la Kaskazini litakaloundwa na mikoa ya sasa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara;

 

(f) Jimbo la Pwani ya Kaskazini litakaloundwa na mikoa ya sasa ya Tanga, Wilaya za Bagamoyo, Chalinze, Kibaha, Kisarawe na Mkuranga katika Mkoa wa sasa wa Pwani na Wilaya za Gairo, Kilosa, Mvomero, Morogoro na Kilombero katika Mkoa wa sasa wa Morogoro;

 

(g) Jimbo la Mji Mkuu wa Dar es Salaam;

 

(h) Jimbo la Pwani ya Kusini litakaloundwa na mikoa ya sasa Lindi, Mtwara na Wilaya za Rufiji na Mafia katika Mkoa wa sasa wa Pwani, na Wilaya ya Ulanga katika Mkoa wa sasa wa Morogoro;

 

(i) Jimbo la Nyanda za Juu Kusini litakaloundwa na mikoa ya sasa ya Mbeya, Njombe na Ruvuma;

2. Majimbo yataongozwa na Gavana atakayechaguliwa moja kwa moja na wananchi katika Jimbo husika.

 

3. Miji, manispaa na jiji ndani ya majimbo itaongozwa na Meya atakayechaguliwa moja kwa moja na Wananchi katika Mji husika;

 

4. Maeneo yasiyokuwa Miji, manispaa na majiji itaunda halmashauri za wilaya zitakazoongozwa na Mwenyekiti atakayechaguliwa moja kwa moja na Wananchi katika halmashauri husika;

 

5. Halmashauri za Wilaya, Miji, manispaa na majiji zitakuwa na mamlaka ya kuteua na kuajiri watendaji wakuu, watendaji na watumishi wote katika maeneo yao kwa kadri itakavyoonekana inafaa na mamlaka hizo.

 

6. Kila Jimbo litakuwa na Baraza la Kutunga Sheria la Jimbo (Provincial Legislative Assembly) litakalochaguliwa moja kwa moja na Wananchi kwa utaratibu utakaowekwa na sheria iliyotungwa na Bunge la Tanganyika.

 

7. Majimbo yatakuwa na mamlaka ya kutoza kodi za aina mbali mbali katika maeneo yao na vile vile yatakuwa na haki ya kupata sehemu ya kodi itakayotozwa na Serikali Kuu kutoka ndani ya eneo la mamlaka ya Jimbo kwa kiwango kisichopungua asilimia arobaini ya kodi yote itakayokusanywa na Serikali Kuu katika Jimbo.

Itaendelea