*Watangaza mkakati wa kumtoa jasho katika Bunge la Bajeti linaloanza leo

*Tundu Lissu: Hatutakubali kuzibwa midomo, asisitiza yeye, wenzake hawatahojiwa

*Ndugai: Sitarajii kuona fujo zinajirudia, Shibuda kutinga na hoja ya kuahirisha bajeti

 

Wakati Bunge la Bajeti linaanza leo mjini Dodoma, wabunge kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), wametamba kuwa kipindi hiki kiti cha Spika kitatambua makali yao.

Wamesisitiza kuwa wamejipanga kikamilifu kumdhibiti Spika ipasavyo, endapo atathubutu kuwazima wakati wa kuchangia mijadala yenye kutetea maslahi ya umma.


Wakizungumza na JAMHURI kwa nyakati tofauti hivi karibuni, wabunge kutoka Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni wameapa kuwa kipindi hiki hawatakubali kubanwa na Spika Anne Makinda na Naibu wake, Job Ndugai, kinyume cha Kanuni za Kudumu za Bunge.


Mnidhamu Mkuu wa Upinzani, Tundu Lissu, amesema siku zote wataendelea kupinga kwa nguvu kubwa, utamaduni wa kufanya uamuzi na kuendesha Bunge mithili ya mali ya mtu binafsi.


Lissu, ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki, ametaka hadhi ya Bunge ilindwe huku akisema, “Wakileta chochote ambacho kiko nje ya utaratibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge, hapo wasitegemee kwamba tutanyamaza hata kidogo, na wanalifahamu hilo.”


Akisisitiza zaidi, Lissu amesema, “Bunge la Tanzania siyo mali binafsi ya Anne Makinda, na si mali binafsi ya Chama Cha Mapinduzi au Serikali yake. Bunge ni mali ya Watanzania, inatakiwa liendeshwe kwa mujibu wa kanuni.


“Kama kanuni hazifuatwi, wasitarajie kabisa kwamba sisi tutawasaidia katika kuvunja kanuni. Hatutawasaidia na hatutanyamaza. Kama wanafikiria kwamba wanakuja kutubana, hatuna shida yoyote ilimradi tu kanuni ziwaunge mkono.


“Kama kanuni hazimuungi mkono [Spika], ubabe hautampeleka popote kabisa, na wala hawezi kutisha mbunge yeyote, hajatuleta sisi bungeni, tumechaguliwa na wananchi kama alivyochaguliwa yeye.” Kwa upande wake, Mbunge wa Karatu, Mchungaji Israel Natse (Chadema), amesisitiza kuwa Kiti cha Spika kinapaswa kutambua kukua kwa demokrasia katika Bunge linaloundwa na vyama vingi vya siasa.


“Sisi tutafuata kanuni na taratibu, hatutakubali vitisho,” amesema Mchungaji Natse ambaye pia ni Wazari Kivuli wa Wizara ya Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu).


Naibu Spika wa Bunge, akieleza jinsi Kiti cha Spika kilivyojipanga kukabiliana na nguvu ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kipindi hiki cha bajeti, ameiambia JAMHURI kuwa hatarajii kuona dosari zilizojitokeza katika mkutano wa Bunge uliopita zinajirudia.


“Siamini kama kuna mbunge yeyote ataleta fujo bungeni, nadhani aibu ile haitajirudia. Kwa hiyo hatujajipanga na niko jimboni kwangu nakula Pasaka, karibu kaka.”

Sakata la wabunge waliogoma kuhojiwa

Kuhusu kitendo cha wabunge kutoka Chadema kugoma kuhojiwa na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, Lissu amesema hawakuona haja ya kwenda kuhojiwa kwa sababu Kamati hiyo imekwishawahukumu.


“Kamati ilikwishamaliza kazi yake tangu Februari 8, mwaka huu, ilishafanya uchunguzi, ikagundua nani mkosaji, ikatusomea hukumu. Watanzania wanafahamu hivyo, wabunge wote wanafahamu hivyo, dunia nzima inafahamu hivyo,” amesema Lissu na kuendelea:


“Maamuzi hayo yalifikiwa kinyume cha Kanuni za Bunge. Kwanza hatukushtakiwa, halafu ili uitwe kwenye Kamati inabidi kwanza ushtakiwe, sisi hatukushtakiwa, hatukupewa hati za mashtaka (sermons), pili hatukuitwa kwenda kujitetea hata kidogo, maamuzi kwamba sisi tulifanya fujo, yalifikiwa bila hata kutusikiliza.


“Wanafahamu kwamba walivunja kanuni, wanachotaka sasa hivi ni sisi tuwasaidie kufunika hayo madhambi yao, tujipeleke kwenye Kamati, tuhojiwe, uamuzi unabaki papale lakini waje waseme tuliwaita wakajitetea…hatuwezi.

 

“Hukumu ilishatoka, [Brigedia Jenerali mstaafu Hassan] Ngwilizi atoe kile alichotoa hadharani tarehe nane mwezi wa pili, ili dunia nzima ifahamu tuliadhibiwa bila kusikilizwa, hatuwezi kwenda kwenye Kamati kwa sababu, kwenda kutamaanisha kwamba Kamati haikumaliza kazi yake wakati ilishamaliza kazi yake, ndiyo maana ilikuja kusoma uamuzi bungeni. Uamuzi wa Kamati huwa hausomwi kama Kamati haijamaliza kazi yake.”


Akizungumzia suala hilo, Mchungaji Natse yeye ametaka kama ni adhabu iwaangukie pia wabunge wanaotoka CCM waliowaunga mkono kwa kile kinachodaiwa kuwa ni kufanya fujo bungeni.


“Kama ni vurugu hata wabunge wa CCM waliwashangilia wabunge wa Chadema wanaodaiwa kufanya fujo,” amesema mbunge huyo.


Kwa upande wao, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, na Joshua Nassari wa Arumeru Mashariki (Chadema), hawakuwa tayari kuzungumzia suala hilo walipoulizwa na JAMHURI.


Wabunge kwa tiketi ya Chadema waliogoma kuhojiwa na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kujibu tuhuma za kuonesha utovu wa nidhamu, uliosababisha vurugu bungeni wakati wa Mkutano uliopita, ni Tundu Lissu (Singida Mashariki), Joshua Nassari (Arumeru Mashariki), John Mnyika (Ubungo) na Pauline Gekul (Viti Maalumu).


Kamati hiyo ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Brigedia Jenerali mstaafu Hassan Ngwilizi, ambaye ni Mbunge wa Mlalo (CCM), ilipewa kazi ya kuwahoji wabunge hao, lakini walikaidi.


Awali, akiwasilisha taarifa ya Kamati hiyo bungeni, Ngwilizi alieleza kwa kutumia ushahidi wa picha za video zilizopigwa na TBC na kumbukumbu za Bunge, kubaini wabunge waliokuwa wakisimama, kuwasha vipaza sauti na kujibizana na Kiti cha Spika kinyume cha Kanuni za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


Brigedia Jenerali Ngwilizi alipotakiwa na JAMHURI kueleza ni hatua gani za kinidhamu zitachukuliwa na Kamati yake dhidi ya wabunge hao, alijibu kwa kifupi:

“Hayo ni mambo ya Bunge na wabunge wake, siwezi kukujibu hilo bwana.”

Wazungumzia bajeti

Katika hatua nyingine, Mchungaji Natse amesema amejipanga kupambana kwa nguvu kubwa kuhakikisha Wizara za Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Afya na Ustawi wa Jamii zinatengewa bajeti inayokidhi mahitaji ya wananchi.


“Wizara ya Elimu ni nyeti sana, elimu ndiyo mazao yote yaliyopo sasa, inapaswa kuwa na mitaala inayokidhi mahitaji ya Watanzania. Kwenye Wizara ya Afya nako kuna kelele katika kuhudumia wagonjwa, nitapambana wizara hizi zipate bajeti zinazoridhisha,” amesisitiza.


Naye Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba (CCM), ameiambia JAMHURI kwamba yeye na wabunge wengine wa chama hicho, wamejipanga kupigania bajeti zitakazowaletea Watanzania maendeleo.

 

“Sisi wabunge wanaotokana na CCM tumejipanga kupigania bajeti ikidhi matakwa ya mpango wa maendeleo na Ilani ya Uchaguzi ili tuwaletee wananchi maendeleo,” amesema Nchemba.


Shibuda na hoja ya kuahirisha bajeti

Wakati wabunge wengine wakieleza mikakati hiyo, Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda (Chadema), yeye amejipanga kutinga bungeni na hoja binafsi ya kuwashawishi wabunge waahirishe kuunga mkono Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2013/2014.


“Nimetafakari, nataka nitoke na ajenda ya kuwaomba wabunge kuahirisha kuunga mkono bajeti, si kuikataa bali kuahirisha tu kuiunga mkono hadi Serikali itakapowasadikishia Watanzania kwamba bajeti hiyo ni kwa ustawi na maendeleo ya binadamu wa Tanzania,” amesema Shibuda na kuongeza:


“Ninataka kujua kama Tanzania kuna kundi la wabunge wangapi ambao ni sauti ya jamii na nuru ya matarajio ya jamii kwa ustawi na maendeleo ya jamii na taifa.


“Nataka kujua pia kama kuna kusigana kwa kimya kimya kwa kutojali maslahi ya jamii, kunakotekelezwa na kundi la kibinafsi.

 

“Lakini kujua pia kama pesa ipo ambayo ndiyo mbegu au mbolea ya kuzalisha hayo tunayotaka kuyapitisha bungeni.”


1167 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!