Chakula cha bure: Falsafa ya Pinda!

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ameiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kuhakikisha inaisimamia Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) ili igawe chakula cha bure kwa kaya 20,000 zinazoishi katika Tarafa ya Ngorongoro.

Alitoa agizo hilo alipozungumza na wakazi wa kata saba za Tarafa ya Ngorongoro katika mkutano wa hadhara uliofanyika Enduleni Madukani, Ngorongoro mkoani Arusha.

Kero kubwa iliyowasilishwa kwenye kikao cha Malaigwanan na kwenye mkutano wa hadhara wa Endulen, ililenga kuiomba Serikali iwape ruhusa ya kuwa na mashamba madogo ya kujikimu kwenye maboma ya wafugaji wanaoishi kwenye Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro. Kero nyingine zilihusu ukosefu wa maji, ajira kwa vijana, mitandao ya simu za mkononi na upatikanaji wa chakula cha msaada kwa haraka.

 

Alikataa ombi la kulima, lakini akaagiza chakula kilichonunuliwa na NCAA kigawanywe haraka, tena bure badala ya kuwauzia wakazi hao ilhali wakijua hawana uwezo wa kununua chakula hicho.

 

Unaweza kuamini kuwa kilichomsukuma Waziri Mkuu, hata akaamua kutoa agizo la kuwalisha bure wananchi wa Ngorongoro, ni huruma aliyonayo.

 

Ambacho hakukiweka wazi ni kama mgawo huo ni wa muda, au ni wa kudumu. Kama ni wa muda, hilo halina tatizo, lakini kama ni wa kudumu, Waziri Mkuu ajue amefanya jambo lisilokuwa la manufaa.

 

Wananchi wa Ngorongoro hawahitaji kupewa chakula cha bure. Kinachotakiwa ni kuwawezesha ili waweze kupata chakula na mahitaji mengine ya kibinadamu. Kulisha kaya 20,000 bure si jambo la mzaha. Hili ni jambo kubwa linalohitaji uwezo na ujasiri.

 

Athari ninazoziona kwa uamuzi wa Waziri Mkuu ni kwamba uamuzi wake wa kuzuia kilimo ndani ya Ngorongoro kunaweza kukawa hakuna maana sana kwa sababu wakati akiziba mwanya huo, amefungua mwanya mwingine wa kupokea watu wengi wenye mahitaji ya chakula cha bure! Sidhani kama anaweza kuwapo mtu mwenye asili ya Kimasai asiyependa kazi, akasikia kuna chakula cha bure kinasambazwa kwa amri ya Waziri Mkuu, halafu akahangaika kuishi nje ya Ngorongoro.

 

Uzito wa suala hili ni kama ule wa ombaomba walio mitaani. Mara kadhaa kumekuwapo mwito wa kiimani kwamba kumsaidia mtu mwenye mahitaji ni jambo la kumfurahisha Mungu. Lakini wakati mwingine kumwaga misaada mitaani kunachochea kuwavuta ombaomba zaidi. Hili ndilo litakalotokea Ngorongoro baada ya agizo la Waziri Mkuu.

 

Na hata kama msaada huo ni wa muda tu, sidhani kama wananchi hao watakuwa radhi kuona Serikali yao “sikivu”, ikiwambia kuwa haina uwezo wa kuendelea kuwahudumia chakula cha bure! Mara zote imeonekana kuwa uongozi wa Pinda ni wa matukio. Serikali imekuwa ikija na mambo ya msingi, lakini kwa namna ya kushangaza, mambo hayo yamekuwa yakizimwa na Serikali kupitia kwa Mheshimiwa Pinda.

 

Bado tunakumbuka namna Serikali ilivyoamua kuweka kodi kwenye bidhaa zinazoingizwa nchini na madhehebu mbalimbali. Baada ya makanisa na misikiti kumbana, Pinda akatangaza uamuzi wa kupangua jambo hilo la maana kabisa. Kigezo alichokitumia ni cha “Serikali hii ni sikivu”.

 

Matokeo yake baadhi ya watu wanaoendesha misikiti na makanisa yaliyochipuka kama uyoga wa msimu wanaingiza bidhaa na kufanya biashara bila kulipa kodi. Wanakusanya mabilioni ya fedha kutoka kwa waumini, wanaendesha miradi mingi kwa manufaa yao, lakini hawalipi kodi kwa kigezo kwamba mali hizo ni za makanisa na misikiti!

 

Haikushangaza kuona “usikivu” wa Mheshimiwa Pinda na Serikali ikiingia hadi kwenye suala la uhifadhi. Serikali hii hii, kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii ilimega eneo kwa ajili ya uhifadhi katika Pori Tengefu la Loliondo. Uamuzi huo ulilenga kuweka eneo maalumu kwa ajili ya kuhakikisha Loliondo inadumu na kwa hiyo Serengeti inaendelea kustawi.

 

Baada ya kubanwa na siasa na wanasiasa, na kwa vitisho vya CCM kupoteza kura, Pinda amekwenda Loliondo na kufuta msimamo wa awali wa Serikali wa kulinda eneo hilo! Ameruhusu wafugaji waingize mifugo yao ndani ya maeneo ya uhifadhi kwa kigezo kwamba kwa miaka yote wamekuwa wakifanya hivyo.

 

Lakini asichokijua Waziri Mkuu wetu ni kwamba kati ya aliowaruhusu kufanya hivyo, asilimia kubwa ni raia wa Kenya wanaoingiza mifugo ndani ya Loliondo. Huko kwao hawana malisho. Kila mita ya mraba ina mwenyewe. Sehemu pekee wanayoweza kuitumia kama shamba la bibi ni Loliondo. Kauli yake imepokewa kwa shangwe mno na Wakenya.

 

Mheshimiwa Pinda pengine hajui kuwa hata kilimo kinachoendelea kwa fujo Loliondo, wanaopeleka matrekta huko ni Wakenya na matrekta ni ya Wakenya.

 

Kwa kuwa Serikali imekuwa sikivu kwa wafugaji wa Loliondo, hata ikaweza kufuta mpango wake wa awali kwa kuwaruhusu wafugaji, basi haitashangaza kuwasikia Wakurya, Waikoma, Wanata, Waisenye na Wasukuma wakidai wamegewe eneo la Serengeti ili mifugo yao ipate maji na malisho!

 

Nimeshangaa kweli kweli kuona Serikali hii “sikivu” ikiwaondoa wafugaji ndani ya Bonde la Ihefu kwa madai kwamba wanaharibu eneo hilo ambalo ni oevu!

 

Serikali “sikivu” lazima iwaache wananchi wake waivuruge Kilombero yote kwa sababu ni haki yao kuwa na eneo la malisho bila kujali idadi ya mifugo waliyonayo.

 

Nitawashangaa wavuvi wanaotumia makokoro wakizuiwa kutumia zana hizo kuendesha uvuvi katika maziwa na bahari. Kama yanawawezesha kupata samaki wengi na kwa haraka, kwanini wazuiwe na Serikali yao “sikivu”?

 

Kwa utaratibu huu wa kushindwa kusimamia inachokiamini, Serikali itawezaje kulinda maelfu ya hekta za misitu asili inayokatwa na kuchomwa mkaa kila siku? Serikali isiyotaka kusimamia sheria, itawezaje kuwazuia wavuvi wanaotumia baruti, tena wengine wakivua karibu na Ikulu bila woga?

 

Waziri Mkuu huyu huyu ndiye aliyemfuata John Magufuli jimboni kwake, kukawa na mkutano wa hadhara. Kwenye mkutano huo akamfunga “gavana” Waziri Magufuli juu ya bomoabomoa kwa watu waliojenga ndani ya hifadhi ya barabara. Nchi inahitaji maendeleo, nchi inahitaji barabara, miji mikubwa inahitaji flyover, kiongozi wa kusimamia kazi hiyo yupo, lakini kwa namna ya kushangaza, anapigwa marufuku kuwaondoa wavamizi! Nchi hii itapiga hatua kimaendeleo? Tutawafikia Wakenya kweli?

 

Ripoti za wataalamu wote wa wanyamapori zimeeleza umuhimu wa kulinda ushoroba (mapitio ya wanyamapori) kule Lolindo. Wameeleza faida na hasara za kupuuzwa kwa jambo hilo. Hawa ni wataalamu. Imeingia presha kidogo tu ya wananchi kutishia kujitoa CCM, Waziri Mkuu anakwenda kutangaza kutengua jambo jema kama hilo!

 

Nchi hii hatuna utaratibu wa kuheshimu ushauri wa wataalamu. Haishangazi kuona madiwani ambao wanajua kusoma na kuandika, ndiyo wanaoamua miji ipangwe vipi, nini kijengwe wapi, na nani asikilizwe na kwa manufaa gani. Madiwani wasio na weledi wa kutosha ndiyo wanaowaburuza mainjinia na mabingwa wa mipango miji.

 

Mahali ambako kumetengwa kuwe uwanja wa wazi kwa ajili ya jamii, wanasiasa wasiojua faida zake ndiyo wa kwanza kupitisha uamuzi wa kubadili matumizi yake. Hoja yao mara zote imekuwa, “Msifanye mambo ya kuwachukiza wananchi na kuwafanya wainyime kura CCM.”

 

Hawa ndiyo wako radhi kuhakikisha kuwa wakati wa uchaguzi wachuuzi wanasambaa hadi kwenye kuta za ofisi nyeti. Uchaguzi ukishamalizika, inakuwa vita kati yao na mgambo au polisi wanaotumwa kuwaondoa.

 

Wakati wa ujio wa Rais Barack Obama wa Marekani tuliona Dar es Salaam ilivyopendeza ndani ya wiki moja. Jiji lilipendeza. Jiji lilipumua. Barabara zilisafishwa kwa maji na sabuni. Waenda kwa miguu walipata fursa ya kutembea kwa raha mustarehe. Bwana mkubwa alipoondoka, vyombo vya kusimamia usafi na mpangilio wa jiji navyo vinaondoka! Jiji limerejea kule kule!

 

Ukiwa angani, ukitazama Jiji la Dar es Salaam, unaweza kuamini kabisa kuwa nchi hii hatuna wataalamu wa mipango miji. Ukweli ni kuwa wapo, lakini wamelemewa na wanasiasa. Wasomi katika nchi yetu ndiyo watu wachovu kabisa waliokubali kushindwa kirahisi na wanasiasa.

 

Kama wangekuwa shupavu, uamuzi wa Waziri Mkuu wa kufuta msimamo wa awali wa Serikali kule Loliondo ungekuwa chachu ya kuwafanya wanamazingira na wahifadhi wakusanyike kumjadili. Kwa kuwa hawana ubavu wa kuhoji uamuzi wa kisiasa na wanasiasa, wamejikalia kimya wakishuhudia mambo yakiharibika.

 

Si kila kinachotakiwa na mtu au kundi fulani la watu, lazima kitimizwe. Sasa kuna hatari ya kuigawa nchi. Kwa mfano, Wasonjo walimwambia wanataka jimbo na mbunge wao Msonjo kwa sababu wanaonewa na Wamasai! Wilaya ya Butiama kuna watu wanaoendesha harakati za kuwa na halmashauri na wilaya yao yenye mwelekeo wa kikabila! Mbeya vivyo hivyo. Maombi mengi ya kugawa majimbo ya uchaguzi yanalenga kuwa na mipaka ya kikabila. Hii ni hatari. Lakini kwa hii Serikali “sikivu”, hilo linawezekana kwa kigezo cha kusogeza karibu huduma za kijamii. Wanachotazama ni huduma za kijamii, lakini si athari za kabila fulani kuwa na eneo lake la utawala! Hili ni balaa kwa umoja wetu kama taifa.

 

Tumeambiwa kuwa Waziri Mkuu ni msomaji mzuri wa magazeti. Kama hivyo ndivyo, basi ajitokeze atusaidie majibu ya maswali haya. Mosi, uamuzi uliotangazwa na Waziri wa Maliasili na Utalii haukupita kwenye Baraza la Mawaziri? Kama ulipita ukiwa hauna ‘maana’, anataka kuueleza umma kuwa Baraza limekosa umakini?

 

Pili, alipoenda kutengua uamuzi huo, alipata baraka za Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri ambaye ni Rais Jakaya Kikwete? Kama ulikuwa uamuzi wa maana, yeye kama mshauri wa Rais anajisikiaje kumshauri Rais jambo lisilofanyiwa utafiti?

 

Tatu, kwa kuwa hii ni Serikali sikivu, ofa hii aliyoitoa ni kwa wana Loliondo tu? Wafugaji wengine kama kule Mugumu wakitaka wamegewe eneo ndani ya Serengeti wataruhusiwa?

 

Nne, hiki chakula cha bure kwa watu wanaoweza kujilisha wenyewe, ni mpango wa muda au wa kudumu? Kama ni wa kudumu, atawazuiaje walio nje wasiingie Ngorongoro kwenda kupata hicho chakula cha bure?

 

Mwisho, natoa wito kwa Serikali kusimama imara kutekeleza kile inachoamini, kwa ushauri wa wataalamu kuwa kina manufaa kwa sasa na kwa siku zijazo. Tunapaswa kuwaheshimu na kuwatumia wataalamu kwa mujibu wa taaluma zao. Tukikubali nchi hii kila kitu kiendeshwe kisiasa, kamwe hatutafanikiwa kusonga mbele.

 

Waziri Mkuu wa zamani, Edward Moringe Sokoine ni mmoja wa viongozi wachache sana katika nchi yetu waliopendwa mno na wananchi. Sokoine alifariki nikiwa na akili timamu. Niliwaona maelfu ya wananchi Dar es Salaam jinsi walivyomlilia.

 

Sokoine hakupendwa kwa sababu ya kuongozwa na utashi wa kisiasa. Sokoine alikuwa kiongozi. Alitenda katika yale aliyoyaamini. Alisimama kidete kulinda heshima na taratibu. Hakutaka kumfurahisha mtu kwa sababu tu ya kutaka apendwe. Kupendwa kwake kulitokana na mambo makubwa na mazito aliyoyatenda kwa mujibu wa sheria.

 

Sokoine hakupendwa kwa sababu aliruhusu wafugaji kuvamia maeneo oevu, mapori tengefu, mapori ya akiba au hifadhi za taifa. Hakupendwa kwa sababu aliruhusu watu kuuza bidhaa popote wanapotaka. Hakupendwa kwa sababu ya kuwabeba waliovamia maeneo ya wazi na wavamizi wa hifadhi za barabara.

 

Sokoine hakupendwa kwa sababu ya kuacha mambo yajiendeshe yenyewe kama tanga linalosukumwa na upepo kwa kumkosa nahodha. Hakupendwa kwa sababu ya hotuba zake tamu za kutoa matumaini ya bure kwa wananchi. Hakupendwa kwa sababu ya kuwabeba maskini waliovunja sheria au matajiri waliokichangia chama!

 

Sokoine alipendwa kwa sababu ya kusimamia uamuzi sahihi wa Serikali, kwa sababu ya kusimamia sheria na taratibu na kwa sababu ya kuwa na msimamo usioteteleka wala kutiliwa shaka juu ya uzalendo na kiu yake ya kuona Tanzania na Watanzania wanakuwa na maendeleo ya kupigiwa mfano. Mheshimiwa Pinda anaweza kujifunza kutoka kwa Sokoine.