Kwenye Mkutano wa 18 wa Bunge uliopita, Mchungaji Peter Msigwa, Mbunge wa Iringa Mjini (CHADEMA) aliongea bungeni na kuhoji uamuzi wa Wizara ya Maliasili na Utalii kutumia wasanii Watanzania kutangaza vivutio vya utalii nchini. Mchungaji Msigwa alisema kuwa wasanii hao hawajulikani na ingefaa kutumia wasanii wa nje wanaofahamika zaidi.

Katika kusisitiza hoja yake, alimtaja msanii Steven Mengele (anayejulikana zaidi kama Steve Nyerere) na kudai kuwa Mengele hana umaarufu wowote. Mengele amejibu na hakufurahishwa na kauli za Mchungaji Msigwa. Alikasirika sana.

Alianza kwa kueleza mchango mkubwa ambao wasanii mbalimbali wanatoa katika masuala muhimu ya kijamii, pamoja na kutetea uamuzi wa kutumika wasanii Watanzania kuhimiza Watanzania kutembelea vivutio vya utalii nchini.

Halafu akashusha ‘kombora’. Alisema kuwa tatizo kubwa kati yake na Mchungaji Msigwa ni kuwa wanagombea mwanamke ambaye Steven anasema anaishi Sinza na ambaye yeye amempokonya Mchuganji Msigwa.

Sifahamu ukweli wa hiyo ‘kesi’ ya Sinza, na sikuona kama suala linalojadiliwa ni kubwa sana kiasi cha kufunika mijadala mingine ambayo ingeibukia bungeni na kufanya tusahau ya Msigwa na Steven mpaka niliposikia maoni ya mtu mmoja akizungumzia uwezekano wa ugomvi huo kuwa chanzo cha kichwa cha habari kinachoarifu: “Nyerere na Msigwa wagombea mwanamke Sinza.”

Steven alianza kupata umaarufu kwa kuanza kumuigiza Mwalimu Nyerere kwenye filamu na kuanza kujiita “Steve Nyerere”. Sasa hivi ni wachache wanaomfahamu kwa jina lake halisi. Kwa hali hiyo si ajabu kuwa wapo watu sasa hivi wamebaki na kumbukumbu kuwa Nyerere amempokonya Msigwa kimada wa Sinza.

Kwa desturi, kutumia jina la mtu mwingine ni kielelezo cha heshima kubwa ambayo muazimaji anampa mwenye jina; ni kielelezo pia cha umaarufu wa mtu ambaye jina lake linatumika.

Katika uzinduzi wa mradi mkubwa wa kufua umeme wa Bonde la Stiegler, Rais John Pombe Magufuli, aliamua kuwa bwawa la maji litakalotokana na mradi huo liitwe Bwawa la Nyerere. Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam, pamoja na maeneo mengi umepewa jina lake kwa sababu ya heshima hiyo ambayo taifa inampa.

Akijitokeza mjasiriamali akapata wazo la kuanzisha “Nyerere Bar na Nyumba ya Kulala Wageni” atahangaika sana kupata ruhusa ya kusajili rasmi biashara hiyo kwa sababu naamini wenye mamlaka hiyo wataona kuwa kumbukumbu ambazo zinapaswa kuhusishwa na Mwalimu Nyerere hazifanani na mienendo ya baa na nyumba za kulala wageni. Kwa misingi hiyo hiyo, si busara hata kidogo kulihusisha jina hilo na kugombea wanawake.

Kuwa na unasibu na jina hilo hakumkingi mtu na ugomvi wa aina hiyo. Lakini ipo tofauti kubwa kati ya kutumbukia ndani ya ugomvi wa aina hiyo na ukakaa kimya, na kuwapo ndani ya ugomvi huo halafu ukaamua kuwa ni busara kukusanya waandishi wa habari na kuutangazia umma, bila kupepesa macho, kuwa ugomvi wako chimbuko lake ni mrembo wa Sinza Mori.

Yaliyotokea yangeyafanywa na Steven Mengele yangeishia kuwa mazungumzo kama mengine, lakini akiyafanya “Steve Nyerere” yanaibua mjadala mwingine wa ziada.

Si kila mara kuwa tunaotumia jina hilo tunafanikiwa kulinda heshima ya jina. Suala muhimu ni kuweka jitihada wakati wote ya kulinda hadhi ya mtu ambaye bado anaheshimika na watu wengi nchini na nje ya mipaka yetu.

Wanajamii tunakubali kuwa tabia mbovu ni kionjo cha kawaida kabisa cha jamii. Lakini jambo ambalo halikubaliki ni kushuhudia watu wenye majina mashuhuri kuwa na tabia mbovu. Watu mashuhuri wanapimwa kwa vigezo tofauti kabisa.

Hivi karibuni nimeandika makala nikitaja tuhuma za ufisadi uliyotukuka zinazomkabili Isabela Dos Santos, binti wa aliyekuwa Rais wa Angola, Jose Dos Santos. Kuna msululu watu wanaotuhumiwa pamoja naye huko Angola, lakini mimi pamoja na watu wengine wengi tumemkalia kooni Isabela kwa sababu ya nafasi yake kama binti wa familia maarufu ya Angola. Unapokuwa VIP matarajio juu yako yanakuwa na hadhi hiyo hiyo.

Ndugu yangu Steve nimshauri kuwa, kama anataka kuendelea kuitwa Steve Nyerere bila kuanzisha mijadala ya aina hii, inampasa kuzingatia kuwa kuna watu wanampima kwa vigezo vya Mwalimu Nyerere na anapaswa kupima kila neno analotamka, na kila jambo analofanya kwa kuzingatia mtu huyo ambaye tunaamini anamheshimu.

Ipo sheria inayoweka taratibu za jinsi gani ya kutumia majina ya waasisi wa Tanzania: Sheikh Abedi Amani Karume, na Mwalimu Nyerere. Ni sheria inayoweka zuio la kutumia majina na picha za waasisi hao kwa madhumuni ya biashara.

Sidhani kama iko sheria inayomzuia mtu kutumia jina ambalo si lake, ingawa sijui kama anaweza akaibuka mtu hapa leo na akaanza kutumia jina la kiongozi mwandamizi aliyeko sasa na asihojiwe.

Sidhani kama suluhisho la suala hili litapatikana kutoka kwenye sheria zilizopo. Suluhisho ni kwa wasanii kama Steve kurudi kutumia majina yao halisi, pamoja na kupachika jina la kujibebea katikati ya majina yake halisi ili iwe dhahiri kuwa jina la katikati si jina lake halisi. Lakini ni bora zaidi kutumia majina yao wenyewe. Itapunguza mikanganyiko mingi.

Barua pepe: [email protected]

By Jamhuri