Chema chajiuza kibaya chajitembeza ni methali kongwe katika lugha yetu ya Kiswahili. Ni methali iliyojaa hekima na ushawishi mkubwa wa kupambanua kitu au jambo zuri na bora, au baya na dhaifu. Waswahili hutumia methali hii katika kupima mwenendo wa binadamu ndani ya jamii yao.

Wiki iliyopita, vyombo vya habari duniani na hapa nchini, viliandika habari iliyohusu Kamisheni ya Amani na Usalama ya Umoja wa Afrika (AU) imefungua jengo katika  Makao Makuu ya  Umoja huo na kupewa jina ‘Mwalimu Julius Nyerere,’ mjini Addis Ababa, Ethiopia.

Kufikiriwa, kukubalika na kupitishwa jina hilo na viongozi wa Umoja wa Afrika (AU) ni jambo jema na lenye thamani kubwa kwa Watanzania. Ni tunu na heshima kubwa tuliyopewa Watanzania. Hatuna budi kutamka ‘asante sana’.

Tunu na heshima hiyo haikutolewa kiupendeleo wala kimzahamzaha, hata kidogo. Tafakuri ya kina imefanyika na kubainika jina kuntu ni ‘Mwalimu Julius Nyerere’ – mtoto wa Tanzania na Afrika, aliyepigania haki na utetezi wa kuondoa dhuluma kwa Mwafrika.

Ndiyo maana Rais wetu mpendwa, Dkt John Magufuli, katika hafla hiyo, alithubutu kusimama kifua mbele na kuwashukuru viongozi wote wa Umoja wa Afrika kwa uamuzi wao wa kulipa jengo hilo jina Mwalimu Julius Nyerere.

Rais Magufuli alisema kuwa viongozi hao wamefanya hivyo kutokana na kutambua mchango wa Mwalimu Nyerere katika kupigania amani na usalama. Aidha, Mwalimu alikuwa Mwafrika halisi na kiongozi mahiri na shupavu.

Rais hakuishia hapo, alisema kuwa katika maisha yake yote duniani, Mwalimu Nyerere ni mmoja kati ya viongozi bora waliotokea Afrika. Ni kiongozi aliyepambana kujenga umoja na mshikamano wa Afrika.

Si hivyo tu, Rais Magufuli alisema kuwa Mwalimu Julius Nyerere ni miongoni mwa waanzilishi wa Umoja huu  na sisi Watanzania kwa hakika tunajivunia Mwalimu Nyerere kuwa Baba wa Taifa letu.

Alimalizia hotuba yake kwa kusema, “Wito wangu kwenu, sambamba na kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa jengo hili, itakuwa ni jambo jema zaidi kama tutajitahidi kufuata nyayo zake na kuishi maisha ya viongozi wengine hodari wa bara hili wakiwamo hayati Kwame Nkrumah, Ahmed Ben Bella, Sekou Toure, Gamal Abdul Nasser na bila kumsahau shujaa wetu mwingine hayati Nelson Mandela”.

Ukisoma kwa makini aya zote zilizotangulia, utaona kitu au jambo zuri daima huenziwa hata kama aliyetenda tendo hilo kwa sasa hayupo, bado waliopo watamuenzi kwa mema yake na kufuata tabia yake. Si rahisi kwa aliyetenda mabaya kuenziwa na jamii ya watu wema zaidi ya kulaaniwa.

Ni miaka ipatayo 18 sasa tangu Mwalimu Nyerere afariki dunia (1999-2017). Ni kimwili chake tu ndicho hatunacho machoni mwetu. Lakini, fikira, mawazo na busara zake bado zinatembea ndani ya bongo za watu makini, waungwana na wapenda amani na usalama. Daima huzienzi na kuzitekeleza. Hicho ndicho chema chajiuza.

Leo, si duniani wala Afrika na hata hapa Tanzania, kila linapojichomoza jua, viongozi wabaya na dhaifu, wasaliti, mabarakala na wapenda kutawala nchi hawahubiri amani na usalama, hawajengi umoja na mshikamano  na hawatetei haki za watu wanyonge, kiukweli zaidi ya kufanya ulaghai dhidi yao.

Kwa sababu nafsi zao zimetawaliwa na tamaa za kuwa viongozi wakuu wa nchi. Fikira na madhumuni yao ni kujenga chuki na mfarakano. Kujilimbikizia mali kwa njia isiyo halali, kulea umaskini na kujenga umbo la maneno mazuri nje na kujaza ndani sumu ya kuangamiza watu.

Viongozi kama hao ni hatari. Tujihadhari nao. Tuwaambie waache tabia ya kuihadaa dunia kwa kutoa maneno ya uzushi na kuwaaminisha watu eti wao ndiyo viongozi bora na wanaokubalika, lakini wanaonewa na kunyang’anywa walichopewa na watu, ilhali hawana walichonyang’anywa na wanashindwa kuthibitisha zaidi ya kulalama tu. Hicho ndicho kibaya kinachojitembeza.

Laiti Mwalimu Nyerere na baadhi ya viongozi wenzake wa Afrika waliokumbukwa katika Mkutano wa 28 wa Viongozi wa Umoja wa Afrika hivi majuzi wangekuwa wazushi, wapekepeke na mabarakala, Kamisheni ya Amani na Usalama ya Umoja huo isingemtunuku na kumuenzi Mwalimu Julius Nyerere na kuipaisha Tanzania yetu iliyojaa amani na usalama. 

Wananchi tujihadhari na viongozi wazushi wanaojitangaza.

By Jamhuri