Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe ameitaka Tume ya Mabadiliko ya Katiba kusikiliza zaidi maoni ya wananchi na kuyapokea badala ya kuyajibu kila yanapotolewa.

Waziri Chikawe alitoa kauli hiyo kwa waandishi wa habari mwishoni mwa wiki wakati akizindua Kitabu kiitwacho Mabadiliko ya Katiba na Hatima ya Tanzania kilichoandikwa na Naibu Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Tanzania Luteni Kanali Lidwino Mgumba.

 

Amesema jukumu la Tume hiyo si kutetea rasimu yao ya Katiba bali ni kusikiliza wananchi wana maoni gani juu ya rasimu hiyo. Aidha, Waziri huyo aliwataka wajumbe wa mabaraza ya katiba kutumia nafasi waliyonayo ipatikane katiba itakayowajali Watanzania wote.

 

Serikali imetoa wito kwa watanzania kuhakikisha wanachangia ipasavyo katika kutoa maoni juu ya rasimu ya katiba iliyotolewa hivi karibuni na Tume ya Mabadiliko ya Katiba nchini Tanzania ipate Katiba itakayokidhi matakwa ya wananchi.

 

Waziri Chikawe alimpongeza mtunzi wa kitabu hicho kwa kutumia Katiba kuandika kitabu kwa kuwa ni suala nyeti. Aliongeza kuwa wananchi hawana budi kuandika vitabu mbalimbali vinavyohusu mila na tamaduni za Kitanzania kuzihifadhi kwa kuwa zinatoweka.

Naye Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Dk. Emmanuel Nchimbi alimpongeza Mtunzi wa Kitabu hicho kwani amekiandika wakati mwafaka huku akiwataka watumishi wa Umma kutumia ujuzi walionao kuandika vitabu mbalimbali vitakavyoelimisha umma wa Watanzania.

 

Awali akizungumza kwenye uzinduzi huo, Luteni kanali Mgumba aliwasisitiza Watanzania kusoma kitabu chake wapate ufahamu wa masuala ya Katiba na hatimaye washiriki vizuri katika mchakato wa kupata Katiba Mpya.

 

Katika kuhakikisha wanafunzi wa shule za sekondari wanapata uelewa wa masuala ya Katiba amegawa nakala za kitabu hicho kwa wanafunzi waliopo Halmashauri ya Manispaa ya Songea na Nachingwea.

857 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!