Kwao neno la kwanza kujifunza ni ‘rafiki’ jina la kwanza wanalojua ni ‘Nyerere’

 

Kwa baadhi ya Watanzania, jina la Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, si muhimu sana kwao. Hii pengine inathibitisha ule usemi wa ‘nabii hakubaliki kwao’.

Lakini kwa walimwengu wengine, mambo ni tofauti kabisa. Miongoni mwa walimwengu wanaomheshimu, kumpenda na kumuenzi kwa vitendo Mwalimu Nyerere, ni marafiki zetu wa Jamhuri ya Watu wa China.

Urafiki wa dhati kati ya Mwalimu Nyerere na Mwenyekiti Mao Zedong; ndiyo ulioyawezesha mataifa haya mawili — Tanzania na China — mwaka huu wa 2014 kuadhimisha miaka 50 ya Ushirikiano uliotukuka.

Bila shaka yoyote, ni kwa sababu hiyo, hivi karibuni maofisa wa ubalozi wa China hapa nchini walizuru nyumbani kwa Baba wa Taifa, eneo la Mwitongo, Butiama mkoani Mara; lengo kuu likiwa kuona namna ya kuasisi ushirikiano kati ya Makumbusho ya Mwalimu Nyerere kijijini hapo na ile ya Mwenyekiti Mao iliyopo China.

Mwalimu Nyerere alizaliwa Aprili 13, 1922 kijijini Butiama. Alifariki dunia Oktoba 14, 1999 na kuzikwa hapo hapo alipozaliwa. Mwenyekiti Mao alizaliwa Desemba 26, 1893 katika Kijiji cha Shaoshan, Jimbo la Hunan; na kufariki dunia Septemba, 1976.

Kaimu Balozi wa China hapa nchini, Li Xuhang, alizuru Makumbusho ya Mwalimu Nyerere kijijini Butiama, akilenga kuthibitisha urafiki wa kweli kati ya Mao na Nyerere; na China na Tanzania. Kwenye ziara hiyo pia walikuwapo maofisa kadhaa wa Ubalozi wa China hapa nchini; Katibu wa Ukuzaji Ushirikiano Kati ya China na Tanzania, Joseph Kahama; na Mdhamini wa Asasi ya Hassan Maajar, Balozi Bertha Semu-Somi. Mwenyekiti wa Ukuzaji Ushirikiano Kati ya Tanzania na China ni Dk. Salim Ahmed Salim.

Balozi Li na ujumbe wake waliwasili Butiama alasiri, na kulakiwa na viongozi wa Wilaya ya Butiama, wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya (DC) hiyo, Angelina Mabula.

Maudhui makuu ya ziara hiyo kijijini Butiama yalikuwa kukabidhi zawadi za picha za ziara zilizofanywa na Mwalimu Nyerere kuanzia miaka ya 1960 hadi miaka ya 1980 ambako alikutana na viongozi wakuu mbalimbali wa China.

Kwenye maelezo ya kumkaribisha Li, DC Mabula alitoa maombi mahsusi kwa Serikali ya China, kupitia ubalozi wake, kusaidia kuboresha Makumbusho ya Mwalimu Nyerere ambayo hakuona shaka yoyote kukiri kuwa haiendani na hadhi na hazina kubwa ya kihistoria iliyotukuka ya Mwalimu Nyerere.

“Tuliwasilisha wazo la namna ya kuboresha Makumbusho ya Mwalimu Nyerere wakati Balozi wa China alipozuru Butiama Aprili 2014. Tumelenga kuifanya Butiama kuwa sehemu ya utalii na lango la kuingia na kutokea Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kwa sababu ni karibu,” anasema Mabula.

Anasema Makumbusho ya Mwalimu Nyerere ni mahali ambako kumekuwa kukiwavutia wananchi na watu wa mataifa ya nje kwenda kujifunza na kushuhudia maisha ya Mwalimu Nyerere.

“Kwa bahati mbaya Makumbusho hayana miundombinu ya kutosheleza mahitaji ya wageni. Wengi huwa na shauku kubwa ya kuzuru Makumbusho haya, lakini kile wanachokitarajia, na kile wanachokikuta ni tofauti kabisa. Wanalalamikia ukosefu wa miuondombinu kama majengo au kumbi za mikutano, huduma za intaneti, malazi, migahawa/hoteli; na huduma za burudani,” anasema.

DC Mabula anaongeza kuwa upo mkakati mahsusi wa kupanua Makumbusho ya Mwalimu Nyerere na pia kuweka huduma muhimu zinazokosekana sasa. Kwenye upanuzi huo, anasema kutajengwa kumbi kubwa tatu zitakazobeba kazi au mchango wa Mwalimu Nyerere katika masuala ya uchumi, kisiasa na maendeleo ya kijamii.

“Nyumba moja ya sanaa itasheheni kumbukumbu za ushirikiano kati ya Tanzania na China zikigusa masuala ya kisiasa, kiuchumi na kijamii. Hapo kutaoneshwa uhusiano wa karibu kati ya Makumbusho ya Mwalimu Nyerere na Makumbusho ya Mwenyekiti Mao ambazo ni muhimu sana kwa historia za mataifa haya mawili.

“Kutajengwa ukumbi wa mihadhara wenye huduma za vifaa vya kisasa kwa ajili ya mijadala ya kitaaluma na makongamano yatakayohusu filosofia za Mwalimu.

“Pia kutakuwa na kumbi zitakazokuwa na historia ya marais wastaafu wa Tanzania; kumbi za kisasa za mikutano; kumbi za ngoma za utamaduni; maktaba ya kisasa itakayokuwa na vitabu vya Mwalimu na machapisho mengine yanayomhusu; kutakuwa na ofisi maalum kwa ajili ya watafiti; chumba maalum cha kompyuta na huduma za kisasa za intaneti; nyumba za kulala wageni na watumishi wa Makumbusho; na ofisi za kutosha kwa wafanyakazi,” anasema.

DC Mabula anasema ni jambo jema kwamba ardhi kwa ajili ya upanuzi wa Makumbusho ya Mwalimu Nyerere, tayari ipo. Matarajio yake ni kwamba ujenzi utaanza baada ya taratibu zote za kisheria zitakapokamilika. Matarajio ni kuona kuwa Makumbusho ya Mwalimu Nyerere yanakuwa na ushirikiano wa karibu sana na Makumbusho ya Mwenyekiti Mao kwa ajili ya kubadilishana uzoefu, taarifa na mbinu mbalimbali za uendeshaji makumbusho.

Nyumba ya zamani ya Mwalimu

Mwanzoni mwa miaka ya 1950, baada ya kutoka masomoni Edinburgh; Mwalimu Nyerere alijenga nyumba yake ya awali kabisa ya ‘kienyeji’. Mwanzoni mwa miaka ya 1960 nyumba hiyo ilifanyiwa ukarabati, lakini ikabaki kwenye muonekano wa kiramani ule ule. Hii ndiyo nyumba aliyoitumia akiwa Butiama kwa kipindi chote akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mwaka 1986 baada ya kung’atuka alihamia katika nyumba mpya aliyojengewa na chama cha TANU (Tanganyika African National Union) katika eneo la Mwitongo. Aliishi kwenye nyumba hiyo hadi alipohamia kwenye nyumba aliyojengewa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na kuishi humo kwa kama wiki mbili hivi.

DC Mabula anasema: “Kimsingi nyumba ya awali kabisa aliyojenga Mwalimu ni ya kihistoria. Kwa sasa ipo katika hali mbaya. Inahitaji ukarabati. Nyumba hii ipo chini ya uangalizi wa familia, lakini tunadhani tuna wajibu wa kuhamasisha michango kwa ajili ya kuikarabati kwa manufaa ya historia ya Taifa letu.”

Anaamini kwamba kupanuliwa na kuboreshwa kwa huduma katika Makumbusho ya Mwalimu Nyerere kutasaidia mno kuinua shughuli za kiuchumi na kijamii katika kijiji, Wilaya ya Butiama na Mkoa wa Mara kwa jumla.

“Idadi ya wageni itaongezeka, ajira zitaongezeka, fursa kwa wasanii na wasanii wa kazi za mikono za kujiajiri zitaongezeka; tatizo la nyumba za makazi kwa watumishi litatatuliwa, mapato kutokana na Makumbusho yataongezeka; vifaa vya kumbukumbu vitatunzwa vizuri zaidi; na historia ya mataifa mawili – Tanzania na China — itajulikana vizuri,” anasema.

Anaongeza: “Msaada unahitajika sana ili kutekeleza mradi huu. Tunahitaji msaada wa kifedha, mafunzo kwa watumishi wa Makumbusho na ujenzi wa majengo mbalimbali.”

 

Li aahidi mambo mazuri

Kwa upande wake, Li anasema: “Kwetu China tuna msemo usemao ‘Tunapokunywa maji, tusiwasahau mababu zetu waliochimba kisima’. Leo hapa tulipo hatupaswi kuwasahau waasisi wetu — Mwenyekiti Mao na Mwalimu Nyerere. Tumekuja hapa kama sehemu ya maadhimisho ya Kumbukumbu ya Miaka 50 ya Urafiki wetu – China na Tanzania.

“Tumekuja kuangalia hali ya Kijiji cha Butiama. Tumekuja kuona nini tunachoweza kufanya kwa ajili ya Makumbusho ya Mwalimu Nyerere na Shule ya Msingi Mwisenge ambayo ndipo Mwalimu Nyerere aliposoma.

“Butiama na Mkoa wa Mara kwa jumla ni mahali pazuri sana. Ni nchi tajiri, ina rasilimali nyingi. Eneo hili limetoa viongozi wakuu katika nchi hii. Wametoka viongozi kama Mwalimu Nyerere, Jaji Joseph Warioba, Joseph Butiku, Profesa Muhongo (Sospeter), Mwanasheria Mkuu wa Serikali (Jaji Frederick Werema). Wametoka wakuu wa majeshi na viongozi wengine wengi.

“Ukombozi wa Tanzania umeanzia hapa (Butiama). Hii ni nchi iliyojaaliwa kuwa na fursa za uwekezaji, vipaji na rasilimali nyingi. Waziri Mkuu Mizengo Pinda alipokuwa China aliiomba Serikali yetu isaidie kutangaza utalii na kuongeza idadi ya watalii kutoka China. Tunaamini hapa ni mahali sahihi panapohitaji kuwa na hoteli na miundombinu ili kuweza kuitangaza vema Butiama.

“Kule China kuna kutembelea maeneo muhimu. Kuna Revolutionary Route. Maeneo ya mashujaa wa China. Wananchi na watalii wengine mbalimbali wanatembelea huko kujifunza.

“Urafiki wa Tanzania na China ni mkubwa. Neno la kwanza kwa Mchina kujifunza ni ‘rafiki’; jina wanalojua Wachina wengi ni ‘Nyerere’. Kwa hiyo kwa suala la utalii Butiama ni kitovu.

“Urafiki kati ya Makumbusho ya Mwalimu Nyerere na Mwenyekiti Mao tunaufanyia kazi. Kila mwaka tunatenga nafasi zaidi ya 200 kwa Watanzania kwenda China kujifunza mambo mbalimbali na kuhudhuria semina. Naamini watumishi wa Makumbusho ya Mwalimu Nyerere watapata nafasi pia,” anasema Li.

Baadaye, Li na ujumbe wake walikabidhi zawadi za picha kwa Mkurugenzi wa Makumbusho ya Mwalimu Nyerere, Emmanuel Kiondo; na kushuhudiwa na mmoja wa watoto wa Mwalimu — Madaraka Nyerere, ambaye alirejea kuishi Butiama tangu mwaka 1999.

Picha hizo ni zile ambazo Mwalimu alipiga akiwa na viongozi mbalimbali wa China kama vile Deng Xiaoping na Chou En-Lai. Li aliahidi kuwa picha za Mwalimu Nyerere na Mwenyekiti Mao zinaandaliwa ili baadaye zikabidhiwe katika Makumbusho hiyo.

Kwa upande wake, Kiondo anasema ushirikiano kati ya Makumbusho ya Mwalimu Nyerere na ile ya Mwenyekiti Mao ni jambo la faraja kubwa.

Anasema Mwalimu ana historia kubwa inayohitaji kuhifadhiwa katika eneo kubwa na lenye huduma za kisasa za mawasiliano. Anaamini kwa kuboresha Makumbusho hayo, wageni wengi watazuru Butiama.

Makumbusho ya Mwalimu ina vitu halisi alivyotumia vikiwamo nguo, saa, viatu, sahani, uma na visu; zawadi alizokabidhiwa kutoka sehemu mbalimbali duniani, nishani na tuzo kadha wa kadha. Pia kuna picha nyingi na gari lililotumiwa na Mwalimu kwa mara ya mwisho akiwa Butiama.

Vivutio vingine ni nyumba zilizojengwa juu ya majabali bila kuathiri mazingira yake ya asili; wanyama kama pimbi, tumbiri na hata nyoka wanaopatikana ndani ya msitu wa asili ndani ya Mlima Muhunda.

Vivutio vingine ni nyayo za binadamu katika miamba ndani ya Msitu wa Muhunda na michoro ya wanyama ya binadamu wa kale katika mapango kadhaa.

Lakini kitu kingine kinachovutia wageni wengi ni hali ya Butiama ambayo inaonesha wazi namna Mwalimu ambavyo hakuwa na tamaa ya kupendelea sehemu aliyozaliwa, kwani hata barabara ya lami iliyopo yenye urefu wa kilometa 11 ilijengwa wakati Mwalimu akiwa ameshafariki dunia.

Pamoja na hayo, muonekano wa Butiama uko hatarini kubadilika kwa kasi kutokana na Butiama kufanywa kuwa Makao Makuu ya Wilaya ya Butiama; na hivyo kuelekea kuwa mji.

1928 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!