Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China zimetiliana saini mkataba wa ushirikiano wa kiuchumi na kiufundi ambako Zanzibar itapatiwa Sh bilioni 14.8.

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar iliwakilishwa na Waziri wa Nchi Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo, Omar Yussuf Mzee; na China iliwakilishwa na Naibu Waziri wa Biashara, Zhong Shan.

 

Baadhi ya walioshuhudia utiaji saini huo ni alietiana saini ambapo ulishuhudiwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Sief Ali Idd na kwa upande wa China ni Naibu Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Hui Liangyu.

Kwa mujibu wa mkataba huo, Zanzibar itafaidika katika ujenzi wa majengo mapya na ukarabati mkubwa wa majengo yaliopo katika Hospitali ya Abdulla Mzee.

 

Pia ujenzi wa Skuli ya Msingi ya Mwananakwerekwe itafadika kwa msaada huo. Shughuli nyingine ni utiaji wa taa za barabarani zitakazotumia nishati ya jua katika baadhi ya barabara kuu za mjini. Aidha, mkataba huo unaelezea kuwa Zanzibar itapata mafunzo mafupi na marefu katika fani tofauti ambayo itapendekezwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

 

Mbali na hayo pia  kutakuwapo uchimbaji wa visima vya maji pamoja na maeneo mengine ambayo nchi mbili zitakubaliana.  Pia ujumbe huo wa China umetiliana saini na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar juu ya msaada wa wataalamu wanne kutoka China ambao watakuwapo Zanzibar kwa miaka miwili wakiwafundisha mafundi wa mitambo wa studio ya kurushia matangazo ya redio na kutoa vifaa mbalimbali kwa ajili ya studio hiyo.

 

Ujumbe huo wa China ukiongozwa na Naibu Waziri Mkuu  uliwasili Zanzibar na kupokelewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Idd pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wakiwamo mawaziri, makatibu wakuu na naibu makatibu wakuu pamoja na maofisa mbalimbali wa Serikali.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein jioni hiyo hiyo alikuwa na mazungumzo na Naibu Waziri Mkuu wa China Hui Liangyu, Ikulu.

 

Walizungumzia ushirikiano kati ya Zanzibar na China. Usiku, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Idd alimwandalia chakula mgeni wake katika hoteli ya Lagemma, Nungwi.

 

Siku iliyofuata Naibu Waziri Mkuu wa China na ujumbe wake walizuru Kanisa la Anglican, Mkunazini na baadaye kuelekea Beit el Ajaib na Jumba la Wananachi Forodhani.

 

 

By Jamhuri