*Mfanyabiashara auawa, wampora dhahabu, mamilioni

*Mtoto, mke, majirani waeleza ‘sinema’ yote ilivyokuwa

Lukumani Yunge (13) ambaye ni mtoto wa Yemuga Fugungu (31) aliyeuawa wiki moja iliyopita nyumbani kwake katika Kitongoji cha Masota, Kata ya Uyovu Lunzewe wilayani Bukombe, ameeleza namna polisi walivyomlazimisha awaonesha chumba kinachotumiwa na baba yake kuhifadhia dhahabu.

Yunge anasoma darasa la nne katika Shule ya Msingi Kanembo. Amewaeleza waandishi wa habari waliozuru nyumbani kwao kuwa Yemuga aliuawa na polisi kwa madai kwamba alimjeruhi mwenzao eneo la Lunzewe.

 

Baada ya kumuua, polisi walitangaza kwamba Yemuga alijiua kwa kujipiga risasi tumboni baada ya kumjeruhi polisi mwenzao. Hata hivyo, mwili wa Yemuga ulipofanyiwa uchunguzi, ulikutwa na matobo mawili ya risasi tumboni na kichwani. Ndugu wa marehemu waligoma kumzika wakitaka uchunguzi ufanywe kwanza.

 

Yunge amedai kwamba wakati akiwa amelala, alisikia mlio wa bunduki huku lango likigongwa. Alipotoka alimulikwa kwa kurunzi na mmoja wa askari waliofika nyumbani hapo. Alidai kuwa askari mwenye kurunzi alimwamuru ampeleke katika stoo ambayo baba yake aliitumia kuhifadhi dhahabu kabla haijauzwa.

 

“Nahitaji uoneshe ilipo stoo yenye makopo ya dhahabu ni wapi…nitakushuti, nioneshe haraka,” Yunge amemnukuu polisi huyo akimwamuru.

 

Yunge anasema, “Nilipomjibu ‘sijui’, akanipiga makofi na ubapa wa panga mgongoni, kisha akaniamuru nikalale. Lakini kila nilipotaka kurudi mlangoni ulipokuwa mwili wa marehemu baba walinizuia.”

 

Hata hivyo, katika kile kinachoonesha kuwa polisi hao walifuata mali za Yemuga, na si kumkamata, Yunge anasema polisi alimfuata kwa mara nyingine huku akionesha sura ya upole na kuanza kumbembeleza amwonesha ilipo dhahabu.

 

“Nikashangaa kuona askari ambaye awali alinipiga bapa za mapanga mfululizo, anarudi na uso wa huruma na kuanza kunibembeleza nimuoneshe ilipo stoo, nami nilishikilia msimamo wa awali na ndipo alipochukia na kuanza kunipekua.

 

Mfukoni alikuta Sh 150,000 zilizotokana na mauzo ya mchanga na kokoto. Akazichukua na kuniamuru niendelee kulala ili nisione kinachoendelea. Nilikuwa natoka na kuchungulia na kuona wanatoa mabulungutu ya pesa kwenye maiti ya baba yangu,” anasema Yunge.

 

MAELEZO YA MKE WA YEMUGA, LUCIA KILAZA

Anasema tukio hilo lililotokea Februari 21, mwaka huu. Lucia anasema ilikuwa saa nne usiku alipofika mumewe na kumhabarisha kuwa gari lao aina ya Fuso Fighter, T 765 BPR limekamatwa na askari polisi kwa madai kuwa lilikuwa na kokoto za wizi.

 

“Aliniambia, ‘Hivi kweli, Mama Kulwa, polisi wananitaka nini? Nimewasaidia mangapi? Leo wanakamata mali zangu na wanataka kuniua’. Wakati huo tulikuwa sebuleni, saa tisa tukasikia geti linagongwa, kuchungulia nje tukaona askari wametanda mlangoni.

 

“Mume wangu akaniambia, ‘hawa watu wananitafuta nini? Hebu twende tukalale’. Tukaingia chumbani. Tulivyoingia tukasikia wanaita Yemuga toka nje. Mume wangu hakutoka. Ndipo baadaye waliruka uzio wakaingia ndani,” anasema Lucia.

 

Anaendelea kusema, “Walipoingia ndani ya uzio waliita tena wakimtaka mume wangu ajisalimishe mwenyewe, na aliposhindwa kutii amri hiyo polisi walianza kuishambulia nyumba tulimolala kwa kutumia silaha za moto, kabla ya kurusha mabomu matatu ya machozi na moja la kishindo ambalo lilipiga ukuta na kuuharibu.

 

Lucia anasema madai ya polisi kwamba alijiua mwenyewe si ya kweli, bali aliuawa kwa kupigwa risasi zilizokuwa zikielekezwa ndani ya nyumba yao.

 

Anasema mumewe hakujiua kwa kujipiga risasi sehemu mbili za mwili, kwani bastola yake inayodaiwa na polisi aliitumia kujiua ilikuwa chumba kingine na hata walipoingia ndani kukagua akiwa tayari amekufa silaha hiyo waliichukua kwenye chumba hicho.

 

Baada ya kumuua, polisi waliutoa mwili wa marehemu nje na yeye kumtupa nje ya uzio, kisha kuingia ndani ya nyumba hiyo na kuanza kupekua na kuchukua baadhi ya mali zikiwamo – simu, Sh milioni 370 zilizokuwa kwenye masanduku mawili na kwenye gari.

 

“Walichukua pia nguo, kadi za benki za NMB na NBC, video kamera. Baada ya kufuatilia vitu walivyorudisha ni kadi za benki, gari na funguo zake,” anasema.

 

MAELEZO YA MSIMAMIZI GARI LA MAREHEMU

Msimamizi wa gari lililokamatwa likiwa na kokoto zinazodaiwa na polisi zilikuwa za wizi, Maarifa Kibaliza (20), anasema baada ya kukamatwa aliwekwa mahabusu na ilipofika saa sita usiku walimtoa ndani na kumtaka awaongoze polisi kwenda nyumbani kwa Yemuga.

 

Anasimulia kuwa walipofika huko yeye akiwa na pingu mkononi, alishuhudia askari wakipiga risasi hewani na kurusha mabomu ya machozi ndani ya nyumba. Anasema baadaye aliona baadhi ya askari wakiutoa mwili wa Yemuga na mke wake (Yemuga) ambaye kwa wakati huo alikuwa amepoteza fahamu.

 

MAELEZO YA JIRANI

Reuben John, jirani wa marehemu Yemuga, anasema kuwa baada ya askari kufika eneo la tukio, walipiga risasi hewani huku wakimtaka mfanyabiashara huyo atoke nje, na kwamba wengine wawili walifika nyumbani kwake.

 

Anawataja polisi waliofika nyumbani kwake kuwa ni Pesambili na George wa Kituo cha Runzewe ambao walifika kwa  ajili ya kumuomba “moko” iliyotumika kuvunja mlango wa nyumba ya marehemu Yemuga.

 

Anasema alipowauliza kulikoni, walidai kuwa wako na wakubwa zao akiwamo Mkuu wa Polisi Wilaya ya Bukombe anayedaiwa kuongoza operesheni hiyo.   Anasema baada ya kupeleka “moko” kwa wenzake, walirudi kwake kujificha kuhofia lawama kutokana na ukweli kwamba Yemuga alikuwa akiwasaidia mambo mengi.

 

“Pesambili akasema hata mchana wa siku hiyo marehemu (Yemuga) aliwasaidia laki moja na isingekuwa vizuri akaonekana eneo la tukio, na ni bora kazi hiyo ya kumkamata ifanywe na askari wageni kutoka Bukombe, ambao kwa wakati huo walikwishavamia nyumbani kwake na kuvunja mlango na kupiga mabomu ndani baada ya marehemu kugoma kujisalimisha mwenyewe.

 

“Baadaye alikuja askari mmoja hapa nyumbani…naona ndiye aliyekuwa akiongoza msafara huo, kwani alipowakuta George na Pesambili wamejificha nyumbani aliwafokea na kuwataka wakafanye kazi iliyokuwa imewaleta, na ndipo walipoondoka nami nilibakia hapa nyumbani nikishuhudia kila kitu kinachoendelea.

 

“Baadaye alikuja tena Pesambili akaniambia ‘dogo una habari? Yemuga na mkewe wamejiua kwa kujipiga risasi.” Habari hizi zilinishitua na kuamua kwenda kujionea, nikakuta maiti ya Yemuga imetupwa nje huku mikono yake ikiwa imepigwa pingu kwa nyuma na baadaye mmoja wa askari akatoka ndani kwa marehemu akiwa ameshika bastola ya marehemu mkononi huku akisema, ‘afande nimeiona, nimeiona hii hapa,’ huku akiionesha kwa kuiinua juu,” anasema.

 

Anaongeza, “Lakini kumbe mke wa marehemu hakufa, alikuwa amezimia tu, ndipo nilipomwita dada yangu ili aje ampepee na ndipo baadaye alipozinduka. Alikuwa hawezi kuongea, na hata alipokuwa akisemeshwa na wale maaskari aliwajibu kwa kuandika chini ardhini, nadhani ni kutokana na moshi wa mabomu yaliyokuwa yakipigwa mle ndani ya nyumba yao.

 

“Baada ya hapo polisi waliingia ndani ya nyumba na kuanza kupekua na kuondoka na vitu mbalimbali. Muda si mrefu askari mmoja aliondoka na mwili wa marehemu kwenda Bukombe, baadaye na mimi walinirudia kwenda kutoa maelezo kituoni.”

 

MAELEZO YA VIONGOZI WA SERIKALI ENEO LA TUKIO

Viongozi wa Serikali ya Kijiji, akiwamo Mwenyekiti wa Kitongoji cha Masota, Evarist Mandwa, na Mwenyekiti wa Kijiji, Peter Kuhanda, wanasema askari hao hawakufuata sheria za kufanya kazi kwani hawakupewa taarifa.

 

“Sidhani kama kweli mtu anaweza kujiua kwa kujipiga risasi mara mbili. Kutokana na nguvu iliyotumiwa na polisi uwezekano wa wao kuhusika moja kwa moja ni mkubwa katika mauaji hayo. Na kwa kawaida sheria inasema anapokuwapo mtuhumiwa eneo husika, askari wanapaswa kutoa taarifa kwetu viongozi wa Serikali ya Kijiji ili kuwapa ushirikiano,” anasema Mandwa.

 

Ofisa Mtendaji wa Kijiji hicho, Wilison Kasala, anasema alipata taarifa za tukio hilo siku iliyofuata. Alitarajia kuitisha kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Kijiji ili kujadili tukio hilo. Wanatoa wito kwa ngazi za juu serikalini na kwenye vyombo vya dola kuchunguza tukio hilo.

 

Diwani wa Kata ya Runzewe, Yusuph Fungameza, anasema madai ya polisi ya kwamba Yemuga alimjeruhi askari kituoni wakati akidai gari lake si ya kweli.

 

“Hivi kama mtu amejeruhi askari tena kituoni iweje wasubiri atoke eneo hilo na baadaye wamfuate nyumbani kwake? Kwanini wasimkamate hapo hapo? Wao walikuwa na SMG na yeye alikuwa na bastola, inawezekana mtu mmoja ashinde askari zaidi ya 30?” Anahoji Diwani huyo.

 

Anasema Serikali inapaswa kulichunguza tukio hilo na kuwachukulia hatua za kisheria polisi wote waliohusika, hasa ikizingatiwa kuwa walipora fedha na mali mbalimbali.

 

MAELEZO YA KAMANDA WA POLISI MKOA WA GEITA

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Leonard Paulo, alisema Yemuga alijiua kwa kujipiga risasi baada ya kudhani amemuua askari wa kituo cha Runzewe, Fortunatus Beatus.

 

Anasema chanzo cha sakata hilo ni gari la mfanyabiashara huyo kukamatwa na askari wa doria waliokuwa katika eneo la Nyantare – barabara kuu ya Runzewe na Nakanyaki – likiwa limebeba kokoto zinazodaiwa kuwa ni za wizi.

 

Kamanda anadai kwamba mfanyabiashara huyo wakati akikamatwa alionekana kuwa amelewa, na akawa anawafokea askari, hali iliyozua mabishano baina yao. Anadai kwamba katika mabishano hayo, alitoa bastola na kuwarushia risasi askari na kusababisha majeraha kwa mmoja wa askari waliokuwa karibu na tukio hilo, kisha akakimbia.

 

Anadai kwamba mfanyabiashara huyo aliingia katika nyumba ya jirani ya mwanajeshi wa eneo hilo, na kuwalazimisha waliokuwa ndani wampatie mavazi ya kijeshi la wananchi na kisha kutokomea nayo nyumbani kwake.

 

“Baada ya mfanyabiashara huyo kuchukua mavazi hayo ya kijeshi, alielekea nyumbani kwake ambako polisi walimfuata kwa lengo la kumkamata. Wakati askari wakiwa katika harakati za kumdhibiti, aliendelea kuonesha ukaidi, hali iliyowalazimu askari warushe bomu la machozi katika nyumba alimojifungia.

 

“Liliporushwa bomu la machozi yule bwana aliamua kujilipua kwa risasi, nadhani alijua kuwa ameshamuua askari wetu kutokana na kumpiga risasi tumboni na mapajani,” anadai Kamanda Paul.

 

MAELEZO YA MKUU WA MKOA WA GEITA, SAID MAGALULA

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Said Magalula, anasema askari waliohusika katika tukio hilo watawajibishwa kisheria, kutokana na ukweli kwamba hakuna mwenye ruhusa ya kumuua mtuhumiwa.

 

Magalula anasema hatua ya kuwawajibisha askari hao itakuja endapo kweli uchunguzi unaoendelea, sambamba na ripoti ya jopo la madaktari sita kutoka Dar es Salaam, Mwanza, Geita na Bukombe, utaonesha kuhusika katika mauaji hayo.

 

1491 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!