Ufisadi wa kutisha na matumizi mabaya ya madaraka vimebainika kuwapo katika Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) ya jijini Arusha, JAMHURI inawathibitishia wasomaji.

Pamoja na kununuliwa kwa vifaa vya mabilioni ya shilingi ambavyo, ama havitumiki, au vipo chini ya kiwango, Makamu Mkuu wa NM-AIST, Profesa Burton Mwamila, anadaiwa kutumia muda mrefu kusafiri ndani na nje ya nchi.

Nyaraka zinaonesha kuwa kuanzia Novemba 27, 2014 hadi Januari 18, mwaka huu alisafiri safari 40, ikiwa ni wastani wa safari tatu kila mwezi.

Katika kipindi hicho safari za nje ya nchi zilikuwa 13, na za ndani zilikuwa 27.

“Amesababisha hata wasaidizi wake nao wawe watu wa kusafiri tu. Safari hizo zimegharimu fedha nyingi mno. Katika kipindi cha mwanzo cha zuio la Rais kwa safari za nje, alisafiri safari mbili za Ethiopia – hatuna hakika kama alikuwa na kibali. Nusu ya mwezi huwa hayupo ofisini,” kimesema chanzo chetu.

 

Ununuzi wa vifaa

Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa chuo kilinunua vifaa vyenye thamani ya dola 120,000 za Marekani (Sh milioni 240) kupitia kampuni ya Dar Worth ya Dar es Salaam bila kuwashirikisha wataalamu wa teknolojia ya mawasiliano.

Ununuzi wa Smart Board hizi zinazotumika kufundishia zimetengenezwa kwa teknolojia ya Kimarekani. Imebainika kuwa hazitumiki licha ya kufungwa katika vyumba vya madarasa.

“Asilimia kubwa ya ufundishaji wa elimu ya juu unatumia PowerPoint Presentations ambayo inahitaji kuwa na projector tu na kompyuta, hivyo kuondoa umuhimu mzima wa kununuliwa kwa vifaa hivyo. Haya ni matumizi mabaya ya fedha kwani zipo elecronic boards nyingi ambazo ni nzuri na ambazo zingeweza kununuliwa kwa gharama nafuu kuliko kutumia fedha nyingi kununua vifaa ambavyo havitumiki,” kimesema chanzo chetu.

Harufu nyingine ya ufisadi ipo kwenye ununuzi wa mashine kubwa tano za kuchapisha vitambulisho.

“Hizi ni Heavy Duty ID Printers, kazi yake ni kutengeneza ID cards nyingi kwa mara moja. Mara nyingi hutumika kwenye viwanda au kampuni kubwa zinazotengeneza vitambulisho au vipeperushi kwa ajili ya matangazo; kitu ambacho NM-AIST hakifanyi wala hakihitaji.

“Mashine hizi mpaka leo zipo zimehifadhiwa katika ghala ndani ya jengo la maktaba na maabara – chumba namba M 02.  Zimewekwa humo ndani hazitumiki na wala hakuna mpango wowote wa matumizi tangu mwaka 2012. Tunaamini hii nayo ni sehemu ya matumizi mabaya ya fedha,” amesema mtoa taarifa wetu.

 

Simu ya mkononi

Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa Mwamila imebainika kuwa ankara ya malipo ya simu yake ya mkononi yanafikia wastani wa Sh milioni 3.5 kwa mwezi. Kiasi hicho ni karibu mara 10 ya kile kilichotengwa na Serikali ambacho ni wastani wa Sh 400,000 kwa mwezi.

Katika mchanganuo huo, JAMHURI imebaini kuwa Mei, 2014 bili ya malipo ilikuwa Sh 3,515,953.53 kupitia hati ya madai Na. 29037000001933 kutoka kampuni ya simu ambayo kwa sasa tunalihifadhi jina lake.

November 2014 bili iliyopokewa ni Sh 2,662,082.62 kupitia hati ya madai Na. 29610000001972; Desemba 2014 (Sh 1,285,054.85) kupitia hati ya madai Na. 29741000001973.

 

Mashine za mamilioni zinaoza

Imebainika chuo kina idadi kubwa mno ya mashine zenye thamani ya mamilioni ya shilingi zinazooza kwa kutotumika tangu ziliponunuliwa mwaka 2012.

Nazo ni Lathe Machine, Miling Machine na Shaper Machine ambazo thamani yake ni Sh milioni 220.

“Kwanini zilinunuliwa kama hazihitajiki? Je, hii ilikuwa njia ya kuhalalisha matumizi batili ya fedha za Serikali?” Amehoji mmoja wa watumishi wa chuo.

Vifaa vingine visivyotumika tangu viliponunuliwa mwaka 2012 ni APC- Smart UPS, RT 192, surt 192 XLBP (Standbay Betry for Server). Idadi yake ni zaidi ya 200 na zilinunuliwa kwa karibu Sh milioni 200.

Mashine nyingine tatu ni za kudurufia  ambazo gharama yake ni dola 30,000 za Marekani kila moja.

Hizi hazijawahi kuunganishwa, hazijawahi kutumika hadi leo (2016). Thamani yake ni zaidi ya Sh milioni 180. Pia zilinunuliwa Electronic Display Boards kwa Sh milioni 50; na sasa zote zimetelekezwa stoo kwa madai kwamba zinatakiwa zinunuliwe kubwa zaidi ya hizo kulingana na mahitaji ya kazi.

Aidha, imebainika kuwa televisheni mbili zimenunuliwa kwa Sh milioni 50 licha ya vifaa hivyo kutokuwapo kwenye bajeti.

“TV hizo zimewekwa katika ukumbi wa mikutano, si za kisasa kiasi cha kuwa na gharama kubwa kiasi hicho, hakuna sababu ya kuziweka ukumbini ukizingatia PowerPoint/projector ndizo zinazotumika zaidi hapo ukumbini,” kimesema chanzo chetu.

Pia imebainika kuna servers cabinets karibu 100 ambazo zilinunuliwa na kutelekezwa stoo.

 

Kupuuza matengenezo

“Chuo kilinunua na kufunga mtambo wa simu kwa ajili ya matumizi ya nje na ndani, mfumo huo ni teknolojia ya Kimarekani iitwayo Avaya G 450 Telephone System. Teknolojia hii ni ya gharama kubwa sana ambayo Serikali iligharimia ununuzi wake.

“Mei 2014 mtambo huu uliungua kifaa chake cha ndani kijulikanacho kama Avaya S 8300D Media Server Blade, kifaa hiki (Avaya S 8300D Media Server Blade) hugharimu kama dola 2,000 hadi dola 4,000 za Marekani (kwa mujibu wa taarifa za mtandao wa Electronic Business wa Amazon.com (Ref. http://www.amazon.com/Avaya-S8300D-Media-Server-Non-GSA/dp/B00GAJNW2S).

“Kutokana na uongozi wa chuo kutokuona thamani ya mtambo huu na wala bila ya kujali gharama kubwa ambayo Serikali ilinunua mtambo huu, hadi leo haujafanyiwa matengenezo tangu Mei 2014.

Gari la chuo lenye namba SU 38375 aina ya Toyota Land Cruiser V8 limeharibika injini huku likiwa bado ni jipya kabisa. Dereva wake aliomba asiliendeshe ili lifanyiwe matengenezo, lakini akalazimishwa na hatimaye likafa injini. Kuna mashine za kudurufia zimesimama kufanya kazi kwa kukosa matengenezo. Nazo ni mashine tatu za Konica Minolta Bizhub 501; ASC Heavy Printers OCE Vario Print (VP 2110 (idadi ni 2).

“Zimetelekezwa maktaba sehemu ya Multimedia. Hizi ni printer za gharama kubwa sana kutokana na uwezo mkubwa na hutumika kwenye viwanda vikubwa au kampuni kubwa zinazofanya masuala ya uchapishaji.

“ASC Heavy Printers CS 2430 (idadi ni 2); ASC Heavy Printers TA 400 CI (4); Kyocera Task Alfa (TA 300I zikiwa ni 10; Kyocera FS 3040 MFP ambazo zipo 20,” kimesema chanzo chetu.

Kwa upande wake, Prof. Mwamila anasema kuharibika kwa baadhi ya mashine kunatokana na ukosefu wa majengo.

Anasema: “Fedha za majengo na fedha za vifaa vya maabara na karakana zilikuwa tofauti. Hizi mashine ni muhimu sana kwa Chuo cha Sayansi, Uhandisi na Teknolojia. NM-AIST inatakiwa kuwa na karakana ambako ndiko mashine hizi zitakapowekwa. Bahati mbaya fedha za awali za majengo hazikutosha kujenga karakana, ambako mashine hizi zingefungwa.

“Jengo litakalokuwa na karakana linajengwa sasa, hivyo tunategemea kuwa mashine hizo zitaanza kutumika katika muda usiokuwa mrefu kutoka sasa. Kwa upande mwingine kama zisingenunuliwa wakati huo tungezipata kwa bei kubwa zaidi sasa kutokana na kuporomoka kwa thamani ya shilingi ya Tanzania.”

Kuhusu matumizi makubwa ya fedha kwa simu yake ya mkononi, Prof Mwamila ameiambia JAMHURI: “Kwa sasa, simu za mezani hapa chuoni hazifanyi kazi baada ya mtambo wa Avaya ambao ulikuwa unatumika kuziendesha kuharibika. Kwa sababu hiyo mawasiliano yote ya simu kati ya chuo na taasisi nyingine yanategemea simu za mkononi za makamu mkuu wa chuo, manaibu na maofisa wengine wa chuo. Chuo kiko mbioni kutengeneza mtambo huo – uhaba wa fedha ndiyo unaochelewesha matengenezo.”

 

>>INAENDELEA

2309 Total Views 1 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!