Conte ajawa mchecheto EPL

Ligi Kuu nchini Uingereza imeingia katika hatua ya lala salama huku nafasi ya kutwaa ubingwa ikiwa mikononi mwa vilabu vya Chelsea yenye alama 78 kwa kucheza michezo 33 na Tottenham Hotspur yenye alama 74 ikiwa na michezo 33.
Kutokana na timu hizo kukaribiana kwa kuwa na tofauti ya alama 4 kati yao Kocha wa Klabu ya Chelsea, Antonio Conte ameliomba Shirikisho la mpira nchini humo mechi zao na Klabu ya Tottenham kuchezwa kwa wakati mmoja.
Akitoa maoni yake juu ya hali halisi ilivyo katika kipindi hiki ambako ligi ikielekea ukingoni, amesema kuna haja ya mechi zinazohusu vilabu vya Tottenham na Chelsea kuchezwa kwa wakati mmoja.
“Ni lazima tuhakikishe tunapata bingwa halali pasipokuwepo na mizengwe ya aina yoyote na jibu la haya yote ni kuhakikisha mechi zetu zinachezwa wakati mmoja,” amesema Conte.
Amesema tofauti ya alama 4 katika mbio za kuelekea kutwaa ubingwa wa nchi kama Uingereza ni suala linalohitaji umakini na tahadhari ya hali ya juu.
“Unapocheza katika klabu kama Tottenham, ukishinda ni sawa, lakini unapokuwa katika klabu kama Chelsea mkipoteza mechi ni balaa,” amesema Conte.
Amesema katika msimu huu Chelsea na Tottenham zina nafasi ya kutwaa ubingwa hali ambayo imeendelea kuongeza ushindani.
Amesema klabu ya Tottenham kwa mara ya mwisho ilitwaa ubingwa mwaka 1961 miaka 56 iliyopita hali inayowapa ari ya kupambana kupata ubingwa.
Kwa upande wake kocha wa Tottenham, Mauricio Pochettino akizungumzia ushauri huo amesema Conte anapaswa kuheshimu utamaduni wa Waingereza na si vinginevyo.
“Haijawahi tokea katika ligi hii watu kukaribiana kwa pointi halafu mechi zao zikachezwa wakati mmoja wakati ligi bado mechi zaidi ya tatu ligi kumalizika,” amesema Pochettino.
Amesema kitu pekee wanachokiomba yeye na wachezaji wake ni uungwaji mkono kutoka kwa wapenzi wote wa klabu hiyo nchini humo na duniani kote.
Kocha huyo raia wa Italia anaikumbuka miaka yake ya 2011 hadi 2014 alipokuwa akiinoa klabu ya Juventus walipojikuta wakishushwa daraja kwa tuhuma za kupanga matokeo.
Klabu ya Juventus ilishushwa daraja baada ya kuhusishwa na upangaji wa matokeo na kupanda daraja katika msimu uliofuata kabla ya kuhamia katika ligi ya Uingereza.
Conte ambaye katika siku za hivi karibuni alishika nafasi ya pili kama ya kocha bora nyuma Massimiliano Allegri wa Juventus ni miongoni mwa makocha bora wa Ligi Kuu ya Uingereza.
Katika miaka ya hivi karibuni Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) imetokea kuwa ligi inayopendwa kiasi cha kufuatiliwa na wapenzi wengi wa mchezo huo duniani kote na kujizolea umaarufu mkubwa.