Si masuala ya uchumi na kijamii tu ambayo yameathiriwa na kuibuka kwa virusi vya corona (COVID-19) duniani, kwani hata masuala ya michezo na burudani nayo yameathirika kwa kiasi kikubwa.

Kuibuka kwa ugonjwa huo ulioanza nchini China mwishoni mwa mwaka jana kabla haujasambaa katika nchi nyingi duniani na kuua maelfu ya watu, kumesababisha kusitishwa kwa shughuli nyingi za burudani kama njia ya kuzuia kusambaa kwa virusi hivyo.

Matamasha mengi ya muziki na shughuli nyingine za burudani zimeahirishwa katika nchi nyingi baada ya kuwapo tishio la kusambaa kwa ugonjwa huo.

Mmoja wa watu walioathiriwa na ugonjwa huo ni mwigizaji na mwongoza sinema maarufu, Tom Hanks, na mke wake Rita Wilson. Hivi karibuni Hanks ametangaza hadharani kuwa yeye na mkewe wamelazimika kujifungia ndani baada ya vipimo kubainisha kuwa wameambukizwa virusi hivyo.

Hanks amewaambia mashabiki wake kupitia mitandao ya kijamii kuwa hivi sasa yeye na mkewe wanalazimika kushinda ndani kulingana na maelezo ya madaktari.

Hata hivyo, amewatoa hofu mashabiki wake kwa kuwaeleza kuwa hali yake si mbaya sana na hivi sasa ametengwa na watu wengine huko nchini Australia.

Nchi nyingi, hasa barani Ulaya, Asia na Marekani ambako ugonjwa huo umeshika kasi, wamelazimika kuahirisha matukio makubwa ya burudani na michezo kama njia ya kuzuia virusi hivyo visisambae kwa wingi.

Hanks anasema kabla ya kugundulika kuwa na virusi hivyo yeye na Rita walijisikia uchovu, akiwa na homa na maumivu ya kichwa.

“Ili kuendana na hali ya mambo kama wanavyoshauri wataalamu wa afya, tulilazimika kupima virusi vya corona na tukabainika kuambukizwa. Tutaendelea kutengwa kwa muda hadi hali yetu itakapotengemaa,” anasema.

Mtoto wa Hanks, Chet, aliyethibitisha habari hizo anasema: “Ni kweli wazazi wangu wameambukizwa virusi vya corona, inatisha. Wote wako Australia kwa sababu baba alikuwa anarekodi sinema huko. Lakini nimezungumza nao kwa simu muda mfupi uliopita, wanasema wako poa, wala hawaumwi sana na hawana hofu.” 

Hanks alikuwa anarekodi sinema kumhusu mwanamuziki Elvis Presley, inayoongozwa na Baz Luhrmann.

Mwanamitindo maarufu duniani, Supermodel Naomi Campbell, naye ametoa onyo kwa watu akiwataka kuzingatia usafi ili wajikinge dhidi ya maambukizi ya corona.

“Safisha kila kitu utakachokigusa,” anasema Naomi katika ujumbe kwa njia ya video huku akionekana akisafisha mkanda wa ndege aliyokuwa amepanda, siti aliyokalia, kitenza mbali, meza na dirisha.

“Hivi ndivyo ninavyofanya katika kila ndege ninayopanda. Sijali watu wananichukuliaje,” anaongeza.

Pamoja na burudani, lakini shughuli za michezo nazo zimeathirika kama vile mbio za Mwenge wa Olympic, ambazo zimeahirishwa.

Mashindano ya langalanga, ambayo yalikuwa yaanze msimu wake mwishoni mwa wiki huko Australia, yamepigwa kalenda kama ilivyo kwa mbio ndefu za London nchini Uingereza (London Marathon). Hali kadhalika na Boston Marathon za nchini Marekani.

Uingereza, Ujerumani, Ufaransa, Italia na Hispania ni miongoni mwa nchi ambazo zimesimamisha kwa muda ligi zao baada ya wachezaji kadhaa na makocha kuambukizwa virusi hivyo.

Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta na mchezaji wa Chelsea na timu ya taifa ya Uingereza, Hudson Odoi, ni miongoni mwa watu waliopimwa na kubainika kuambukizwa virusi hivyo.

Mechi za mzunguko wa pili wa hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya (UEFA), zilizokuwa zimepangwa kupigwa leo na kesho nazo zimeahirishwa.

Ingawa ugonjwa huo haujaingia nchini mwetu, lakini wiki kama tatu zilizopita Shirikisho la Soka nchini (TFF) lilichukua hatua kadhaa, ikiwemo kuwataka wachezaji kutosalimiana kwa kushikana mikono kabla ya mechi kama ilivyo ada.

By Jamhuri