Na Thobias Mwanakatwe
 
MGOGORO wa kiasiasa unaoendelea ndani ya Chama cha Wananchi (CUF) umedhihiriha jinsi viongozi wanavyofinyanga sharia na demokrasia ya vyama vingi ilivyo na mwendo mrefu kabla ya kufikiwa.
Chama hicho ambacho ni cha tatu kwa ukubwa nchini, mgogoro wake ulianza baada ya Prof. Ibrahimu Lipumba kujizulu nafasi ya uenyekiti wa taifa wakati wa uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 2015, lakini mwaka 2016 akatangaza kurejea ndani ya chama hicho.
CUF kilikuwa chama kilichokuwa kinakwenda vyema kwa upande wa upinzani, lakini ghafla wiki chache kabla ya uchaguzi, dhoruba kubwa ikaukumba Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ambapo Prof. Lipumba aliyekuwa mstari wa mbele kuunganisha vyama vya upinzani alijiengua ghafla.
Ukiacha Lipumba, hata aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbrod Slaa naye aliamua kujiengua kwa walichodai kuwa dhamiri zimewasuta na wanapinga ujio wa mgombea wa Ukawa, Edward Lowassa.
Baada ya mvurugano huo, CUF waliounda Kamati ya Muda ya Uongozi iliyoongozwa na Julius Mtatiro, ambayo ilianza kuendesha shughuli za CUF, lakini baada ya muda mfupi kamati hii ikakwamishwa.
Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mtungi aliingilia kati mzozo huo na kumtambua Prof. Lipumba kama mwenyekiti halali pamoja na kujiuzulu kwake awali.
Profesa Lipumba alionekana kuwa msaliti kwa chama chake kutokana na kujiondoa katika uongozi wa chama hicho katika dakika za mwisho, ambapo uwepo wake ulikuwa muhimu na ulihitajika kuliko wakati wowote wa harakati za upinzani hapa nchini.
Hali hiyo ilizaa mpasuko mkali ndani ya chama na kuwa na makundi mawili, Cuf Lipumba na CUF Maalim Seif kila mmoja akiwa na wanachama wake.
Hivi sasa mgogoro huo umeingia katika hatua mbaya baada ya wiki iliyopita Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la Chama cha Wananchi (CUF) kutangaza kuwavua uanachama wabunge wanane wa chama hicho kwa madai ya utovu wa nidhamu ikiwemo kukisaliti chama hicho.
Mwenyekiti wa CUF, anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyamavya Siasa, Profesa Ibrahimu Lipumba, katika taarifa yake aliyotoa Julai 24, mwaka huu amesema baraza hilo pia liliwavua uanachama madiwani wawili wa viti maalum mkoa wa Dar es Salaam kwa makosa kama hayo.
Amesema wabunge hao waliovuliwa uanachama ni kati ya 10 walioitwa hivi karibuni kuhojiwa na Kamati ya Maadili na Nidhamu wakitakiwa kujibu tuhuma zinazowakabili za kukihujumu chama hicho kwa maelezo kuwa walitaka kushirikiana na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kumwondoa yeye (Prof. Lipumba madarakani).
Prof. Lipumba baada ya kutangaza kwenye vyombo vya habari siku hiyo kuwatimua wabunge hao anasema amewasilisha nyaraka za hatua zaidi kwa Spika wa Bunge na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.
“Wao wakajenga mazingira ya kwamba Freeman Mbowe wa Chadema awe Msemaji wa CUF, alafu wanadiriki kukaa na viongozi wa Chadema na mwenyekiti anasema yeye ni Makamu Mwenyekiti wa Kanda ya Pwani ametumwa na Mwenyekiti wake wa Kanda ya Pwani, Fredrick Sumaye kuzindua Operesheni Ondoa Msaliti Buguruni na wabunge wa CUF wapo. Kubenea anasema hawa viongozi wa CUF tumewakaribisha tu hiki ni kikao cha Chadema hao viongozi wa CUF kwamba wao ndio wanaendesha Operesheni ya ondoa msaliti Buguruni,” alisisitiza Prof. Lipumba.
Baada ya mzozo huo, Lipumba ameandika barua kwa Spika kumweleza kuwa amewafukuza uanachama wabunge wanane.
 
Spika abariki kutimuliwa wabunge nane wa cuf
 
Spika alipokea barua ya maazimio ya “Baraza la CUF” Julai 24, na kueleza kuwa anaendelea kutafakari suala hilo.
Hata hivyo, siku moja tu baada ya kupokea barua kutoka kwa Prof. Lipumba, Spika wa Bunge, Job Ndugai alitoa taarifa kwa vyombo vya habari ya kukubali barua aliyoandikiwa na Prof. Lipumba kuwatimua uanachama wabunge wake wanane wa viti maalum.
Hatua ya Spika kukubaliana na barua ya Prof. Lipumba ilimaanisha kuwa wabunge hao wamepoteza viti vyao bungeni na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, ikatakiwa kuteua wanachama wengine kuziba nafasi hizo.
Taarifa iliyotolea na Bunge Julai 26, mwaka huu ilieleza kuwa Spika amechukua uamuzi huo kwa mujibu wa Ibara  ya 67(1)(b) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977).
Spika alitoa uamuzi huo siku moja tu baada ya kueleza kupokea barua ya Profesa Lipumba na kusema anaitafakari kabla ya kutoa uamuzi wake.
Wabungu waliopoteza nafasi zao ni Severina Mwijage, Saumu Heri Sakala, Hadija Al- Qassmy,Salma Mwassa, Riziki Mngwali, Raisa Mussa, Miza Bakari Haji na Halima Mohammed.
MNYIKA AMPINGA SPIKA
Wakati suala hilo la kutimuliwa wabunge hao likishika kasi, mbunge wa Kibamba (Chadema) John Mnyika,  July 28, 2017 aliibuka na kueleza kuwa hatua ya Spika Ndugai kubariki kufutiwa uanachama Wabunge wa Viti Maalumu wa CUF ni makosa.
Mnyika alisema ni makosa kwasababu bado kuna kesi mahakamani kuhusu utata wa uongozi wa Chama hicho. Aidha, Mnyika alimuomba Spika kutangaza wateule ambao wametangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi July 27, 2017.
 
NEC YATANGAZA WABUNGE WAPYA
Wakati hayo yakiendeela Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilitangaza kuteua wabunge wapya kuziba nafasi zilizoachwa wazi na wabunge wanane waliovuliwa uanachama.
Taarifa ya NEC kwa vyombo vya habari ilieleza kuwa kwa mujibu wa Ibara ya 78(4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ikisomwa pamoja na kifungu cha 86(8) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, sura ya 343, Tume hiyo ilitangza kuteua wabunge wapya.
“Tume ya Taifa ya Uchaguzi katika kikao chake cha tarehe 27 Julai 2017 imewateua wafuatao kuwa Wabunge wa Viti Maalum katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Wananchi (CUF). Rukia Ahmed Kassim, Shamsia Aziz Mtamba, Kiza Hussein Mayeye, Zainab Mndolwa Amir;
Wengije ni Ndugu Hindu Hamis Mwenda, Sonia Juma Magogo, Alfredina Apolinary Kahigi, Nuru Awadh Bafadhili.
Tume ilieleza kuwa uteuzi huo umefanyika baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye kwa mujibu wa Kifungu cha 37(3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 alitaarifu Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuwepo kwa nafasi waza nane (8) za Wabunge wa Viti Maalum kupitia CUF.
MAALIM SEIF APINGA
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad alinukuliwa akisema bado wanawatambua wabunge wanane waliovuliwa uanachama na kupoteza sifa za kuwa wabunge. Wabunge hao wamefungua kesi iliyopewa namba 143/2017 kupitia Wakili wao Peter Kibatala.
Katika mazingira haya yanabaki maswali mengi ambayo yanashuka kama nyundo. Najiuliza, je, Maalim Seif akishinda kesi ya msingi mahakamani Lipumba atasimamia miguu ipi?
 
Je, utamaduni uliozoeleka wa Bunge kutofanya uamuzi wowote unaoingilia muhimili mwingine wa dola umepotelea wapi katika suala hili? Je, nchi bado inaheshimu utawala wa sharia? Yangu macho.
4107 Total Views 1 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!