Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Profesa Kitila Mkumbo akijaza fomu maalumu baada ya kusoma mita ya mteja wakati wa kuhakiki mita za wateja wakubwa na wadogo. Aliyechuchumaaa ni Meneja wa DAWASA Ubungo, Mponjoli Damson.

Rais Dk. John Magufuli ametimiza miaka mitatu madarakani. Katika kipindi hiki taasisi kadhaa za serikali zimekuwa zikielezea mafanikio yaliyopatikana katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Katika kutekeleza azima ya kuelezea kuhusu mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano, Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA), Mhandisi Cyprian Luhemeja, amesema mamlaka hiyo imepata ufanisi mkubwa, ambapo makusanyo ya maduhuli yameongezeka kutoka Sh bilioni 2.9 kwa mwezi mwaka 2014/15 hadi kufikia Sh bilioni 10.5 kwa mwezi kwa sasa.

Mhandisi Luhemeja amesema lengo la DAWASA ni kuhakikisha wanakusanya Sh bilioni 13 kwa mwezi kuanzia Januari 2019.

Katika kuhakikisha lengo hilo linatimia, DAWASA imejizatiti kuandaa miradi kadhaa ya uboreshaji wa huduma ya majisafi na majitaka, kwa mfano; mradi wa upanuzi wa mtambo wa Ruvu Chini kuongeza uwezo wa uzalishaji kutoka lita za ujazo milioni 180 kwa siku kufikia lita za ujazo milioni 270 kwa siku.

Hatua nyingine ni ujenzi wa bomba kubwa la kipenyo cha mita 1.8 la kusafirisha maji kutoka Ruvu Chini mpaka kwenye matenki ya Chuo Kikuu cha Ardhi, kilichoko jijini Dar es Salaam na upanuzi wa mtambo wa Ruvu Juu ili kuongeza uwezo wa uzalishaji maji kutoka lita za ujazo milioni 82 kwa siku kufikia lita za ujazo milioni 196 kwa siku.

Mhandisi Luhemeja amewaambia wanahabari kwamba upo ujenzi wa mabomba makubwa ya kusafirishia maji kutoka Mlandizi hadi Kimara kilomita 57, kipenyo ‘48’ na ‘42’.  Amesisitiza kuwapo ujenzi wa tenki kubwa la kuhifadhia maji lenye uwezo wa kuhifadhi lita za ujazo milioni 10, tenki hilo litajengwa Kibamba katika Manispaa ya Ubungo.

Sambamba na upanuzi huo wa miundombinu, amesema uchimbaji wa visima virefu 20 vya Kimbiji na Mpera utasaidia kuongeza kiwango cha maji jijini Dar es Salaam.

Mhandisi Luhemeja amesema DAWASA imejipanga katika kuhakikisha tatizo la maji linakuwa historia kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam pamoja na Mkoa wa Pwani. Amesema kukamilika kwa mradi wa maji Chalinze unaotarajiwa kukabidhiwa mwezi Desemba 2018, utaongeza tija katika kuleta suluhisho la maji.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Luhemeja, kiwango cha uzalishaji maji kimeongezeka kutoka lita za ujazo 300,000 hadi kufikia lita za ujazo 502,000 kwa siku katika kipindi cha miaka mitatu, huku upatikanaji wa maji ukiongezeka hadi kufikia asilimia 75, ambapo kwa wastani jumla ya wakazi milioni 4.7 wanapata huduma ukilinganisha na mwaka 2015 ambapo wakazi milioni tatu walikuwa wanapata huduma hiyo.

Amesema katika kuhakikisha maeneo ya Jiji la Dar es Salaam yanapata maji, DAWASA imeanza ujenzi wa kilomita 1,025 za mtandao wa mabomba ya maji, ujenzi wa matenki 19 pamoja na upanuzi wa mtambo wa kuzalisha maji Wami kutoka mita za ujazo 500 hadi 900 kwa siku.

Mhandisi Luhemeja amesema katika kuhakikisha huduma ya maji inasogezwa kwa wananchi, DAWASA Mpya itaanza ujenzi wa viosk 350, ujenzi wa kituo cha pampu ya kuongeza nguvu ya maji, mradi ambao utahudumia vijiji 65. Mtendaji Mkuu huyo amesema jumla ya wananchi 320,000 watahudumiwa.

Amesema katika miaka mitatu ya utawala wa Rais Dk. Magufuli, DAWASA imepata ongezeko la idadi ya wateja waliounganishiwa huduma ya maji na kufikia wateja 298,000. Wakati huohuo, Luhemeja amesema DAWASA imerahisisha huduma ya maunganisho mapya kwa njia ya mkopo pamoja na kuboresha kituo cha huduma kwa wateja (Call Centre) kwa kutumia mifumo ya kielektroniki.

Luhemeja amesema DAWASA imejipanga kumaliza tatizo la maji Dar es Salaam ifikapo mwaka 2020. Upatikanaji wa huduma ya maji katika Jiji la Dar es Salaam utakuwa asilimia 95 kwa majisafi na asilimia 30 kwa majitaka.

Katika kufikia malengo ya mradi wa mfumo wa usambazaji wa majisafi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mpaka Bagamoyo, mabomba yenye urefu wa kilomita 1,426 yatalazwa na wateja wapya zaidi ya 300,000 wataunganishwa.

Amesema kuhusu mradi wa mifumo midogo midogo inayojitegemea ya usambazaji maji kwenye maeneo yasiyo na mtandao ‘off grid water supply schemes’, kutakuwa na maunganisho ya wateja wapya 100,000.

Luhemeja amesema DAWASA inatekeleza miradi ya mifumo ya usambazaji wa majisafi maeneo ya kusini mwa Jiji la Dar es Salaam (Part 4D na 4E) ambapo mabomba yenye urefu wa kilomita 400 yatalazwa na wateja wapya zaidi ya 71,600 wataunganishwa.

Amesema ujenzi wa mifumo midogo midogo 50 ya kuchakata majitaka ‘Off Grid Sanitation Systems’ katika maeneo yenye msongamano wa watu kama vile Manzese, Tandale, Mburahati, Vingunguti na Buguruni unatekelezwa.

Afisa Mtendaji Mkuu huyo amesema ujenzi wa mradi wa maji Kisarawe, ujenzi wa mradi wa maji Chalinze Mboga, ujenzi wa mradi wa maji maeneo ya Viwanda Kibaha na Bagamoyo nayo inatekelezwa na iko katika hatua tofauti tofauti.

Amesema miradi ya ujenzi wa mifumo mipya ya majitaka na mitambo ya kisasa ya kuchakata majitaka maeneo ya Jangwani, Kurasini na Mbezi Beach inajengwa, kumalizia uchimbaji wa visima vya Kimbiji na Mpera pamoja na kujenga mifumo ya usamabazaji maji na ujenzi wa Bwawa la Kidunda ili kuwa na uhakika wa maji kwenye Mto Ruvu kipindi chote cha mwaka.

Hali ya huduma ya Majisafi na Majitaka mwaka 2015

 

Mhandisi Luhemeja amesema DAWASA ilikuwa inahudumia eneo lenye wakazi milioni 5.9, huku akisisitiza kwamba hali ya upatikanaji wa maji katika eneo hili ilikuwa ni asilimia 68, ambapo kwa wastani jumla ya wakazi milioni 3 walikuwa wanapata huduma.

Amesema mahitaji halisi ya maji kwa wakazi wa jiji ilikuwa ni mita za ujazo 450,000 wakati uzalishaji ulikuwa ni mita za ujazo 300,000 kwa siku.

Amesema miaka mitatu iliyopita kiwango cha upotevu wa maji kilikuwa ni asilimia 57 kutokana na uchakavu wa miundombinu ya usambazaji wa maji, huku kiwango halisi cha maji yaliyokuwa yanawafikia wananchi  ilikuwa ni lita za ujazo 129,000 kwa siku, hivyo kusababisha upungufu wa mita za ujazo 321,000 kwa siku.

Kwa mujibu wa takwimu za Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, sehemu kubwa ya Jiji la Dar es Salaam ilikuwa na uhaba mkubwa wa huduma ya maji, hivyo kusababisha mgao wa maji na wizi mkubwa wa maji hasa kwenye maeneo ya Magomeni, Tandale, Mburahati, Kimara na mengineyo.

Amesema eneo la huduma lilikuwa linakumbwa na magonjwa ya mlipuko mara kwa mara, mfano kipindupindu kutokana na miundombinu duni ya majitaka. Urefu wa mtandao wa usambazaji wa maji ulikuwa kilomita 2,500.

Luhemeja ameseman ufanisi wa DAWASA haukuwa wa kuridhisha, ambapo makusanyo ya maduhuli yalikuwa kiasi cha Sh bilioni 2.9 kwa mwezi, kutokana na mifumo duni ya malipo.

Amesema kiwango cha upotevu wa maji kimeshuka na kufikia asilimia 44, lengo ni kufikia asilimia 30 mwisho wa mwaka wa fedha 2020/21. Sehemu kubwa ya Jiji la Dar es Salaam kwa sasa linapata huduma ya maji, hivyo kupunguza kwa kiwango kikubwa wizi wa maji na mgao katika maeneo mengi.

Katika miaka hii mitatu, Mhandisi Luhemeja anasema maeneo ambayo hayakuwa na huduma sasa yamefikiwa ni pamoja na Segerea, Kinyerezi, Kipawa, Ukonga, Changanyikeni, Goba, Mivumoni, Salasala, Madale, kwa Msuguri, kwa Mbonde, Misugusugu, Kiwalani, Miti Mirefu na baadhi ya maeneo ya Manispaa ya Kigamboni.

Amesema kilomita 176 za mtandao chakavu zimebadilishwa kwa kutumia fedha za ndani, hivyo kuchangia kupunguza kiwango cha maji yanayopotea, huku jumla ya kilomita 500 za mabomba zimepanuliwa, hivyo kuongeza wigo wa upatikanaji wa maji. Kwa sasa DAWASA ina mtandao wa kilomita 3,000 kutoka kilomita 2,500 zilizokuwepo mwaka 2015.

Mamlaka ya Majisafi na Majitaka DSM (Dar es Salaam Water and Sewerage Authority – DAWASA) iliundwa tarehe 4/4/1997 baada ya Serikali kufanya marekebisho ya Sheria Na. 7 ya mwaka 1981 kwa kuunganisha shughuli za DSSD (Dar es Salaam Sewerage and Sanitation Department).

Mwaka 2001 Sheria Na. 7 ya Mwaka 1981 ilifutwa na kuanzishwa Sheria Na. 20 ya maji Dar es Salaam iliyoanzisha DAWASA.

Mwaka 2003 DAWASA iliingia mkataba wa miaka 10 wa ukodishaji na City Water Services (kwa lengo la kuleta mtaji na teknolojia ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma), mwaka 2005 City Water walishindwa kutimiza masharti ya mkataba na mkataba wao ukasitishwa.

Mwaka 2005 DAWASCO (Dar es Salaam Water and Sewerage Corporation) iliundwa chini ya sheria ya Mashirika ya Umma (Public Corporations Act, 1992 Order No. 139).

Juni 2005 DAWASA ilisaini mkataba wa ukodishaji kwa miaka 10 (umeongezwa muda hadi Agosti 2018). Baada ya utendaji wa DAWASCO kuimarika Serikali ya Awamu ya Tano iliamua kuunganisha taasisi hizi na kufanya kuwa moja. Yaani  DAWASA Mpya.

Katika kuhakikisha kwamba juhudi za kupanua miundombinu za majisafi zinakwenda sambamba na zile za kuweka miundombinu za majitaka, Mhandisi Luhemeja amesema karibu kila nyumba jijini Dar es Salaam ina karo la maji.

Amesema DAWASA imeamua kufufua sehemu mahususi za kuhifadhi majitaka ili kuilinda jamii na magonjwa ya mlipuko kama vile kipindupindu. Luhemeja amesema DAWASA iko katika mchakato wa kununua malori 20 yatakayosaidia kuimarisha hali ya utoaji wa huduma ya majitaka.

“Japo bado tuko kwenye changamoto ya ununuzi. Private sector wanafanya, ila kimsingi huduma hiyo inatakiwa kufanywa na DAWASA. Sisi tuko regulated, tumeshazungumza na EWURA ili watupatie bei, hilo pia litasaidia hata hao private kufuata bei elekezi.

“Tumeanza kujenga treatment centre, tumeanza na Toangoma, tumejenga nyingine Vingunguti. Kujenga mtandao wa majitaka ni aghali sana,” anasema Mhandisi Luhemeja.

By Jamhuri