Mkuu wa Wilaya (DC) ya Geita, Manzie Mangochie, ameingia kwenye vita ya maneno na waandishi wa habari wilayani humo. Katika hatua ambayo haijapata kutekelezwa na DC yeyote, sasa Mangochie, anataka taarifa za waandishi wote, pamoja na sifa zao za elimu. Hoja yake ni kwamba anataka kuandaa “Press Cards”; jambo ambalo kwa miaka yote limekuwa likifanywa na Idara ya Habari (Maelezo).

Hata hivyo, hatua ya DC huyo haitokani na jambo jingine, isipokuwa chuki yake dhidi ya waandishi wa habari ambao wamekuwa wakiandika habari zake nyingi zenye mkanganyiko ambazo hataki kuzisoma. Hatua yake ya kuanza kuwabana wanahabari ni mwendelezo wa ubabe na matumizi mabaya ya madaraka. Baadhi ya habari za karibuni kabisa zilizomchefua DC huyo, ni hizi zifuatazo:

DC aagiza shule ivunjwe

Mkuu wa Wilaya ya Geita, Manzie Mangochie ameanza kazi kwa kusitisha ujenzi wa Sekondari ya Kata ya Lubanga wilayani hapa kwa kile alichodai eneo hilo lilistahili kujengwa hoteli ya kitalii na si shule.


Mkuu huyo wa wilaya alisitisha ujenzi huo jana alipofanya ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye kata hiyo ikiwamo shule hiyo iliyojengwa kwa nguvu za wananchi ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Serikali za Mitaa yaliyofanyika kiwilaya katika Kijiji cha Lubanga wilayani Geita.


Hata hivyo akiwa eneo ilipojengwa shule hiyo alipigwa na butwaa kuona imejengwa juu ya mlima wenye mawe mengi na baada ya kuhoji eneo la wanafunzi watakapojipanga eneo la ukaguzi na utakapowekwa uwanja wa  michezo wa shule aliamua kusitisha ujenzi huo mara moja baada ya kukosa majibu ya kuridhisha kutoka kwa viongozi wa serikali wa eneo hilo.

Shule hiyo imefikia kiwango cha ujenzi wa madarasa matatu.

Geita Gazeti Mtanzania

Julai 7, 2012

CUF wamshitaki DC kwa RC

CHAMA cha Wananchi (CUF) wilayani Geita, kimemshitaki Mkuu wa Wilaya (DC) hiyo, Omary Manzie, kwa Mkuu wa Mkoa (RC), Said Magalula, kwa madai ya kutawala kibabe, kushindwa kutatua kero za wananchi na kuwabagua kwa itikadi za vyama.


Hatua hiyo imetokana na malalamiko mbalimbali ya wananchi ambayo yamekuwa yakiwasilishwa kwake kwa ajili ya kuyapatia ufumbuzi, lakini baadhi yao huwatimua ofisini mwake kwa madai hana nafasi ya kusikiliza majungu.


Katibu wa CUF wilayani Geita, Sevelin Malugu, aliliambia gazeti hili jana kuwa DC aliteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuwatumika wananchi wote, lakini hali hiyo imekuwa kinyume na matarajio yao.


“Mimi namuona DC wangu ni limbukeni wa madaraka… kama nafasi aliyonayo anakuwa hivyo, je, angepewa ukuu wa mkoa ingelikuwaje au angekuwa yeye ndiye Kikwete si angeliweza kutemea mate watu?” alihoji Malugu.

Gazeti Tanzania Daima

Agosti 23, 2012

DC atangaza vita na mwandishi wa habari

Mkuu wa Wilaya (DC) ya Geita, Manzie Omari, ametangaza kupambana kufa au kupona na mwandishi wa habari wa gazeti la Tanzania Daima, Victor Eliud, kwa madai ya kumchafua.

 

Pia, amemtishia maisha mwandishi huyo akisema atakiona cha moto ikiwa ni pamoja na kumfikisha mahakamani kama hatakoma kile alichokiita kuandikwa vibaya katika baadhi ya tuhuma zinazomkabili.

 

Mkuu huyo wa wilaya alitoa kauli hiyo siku chache baada ya gazeti la Tanzania Daima kuchapisha habari iliyokuwa na kichwa kisemacho, “CUF wamshitaki DC kwa RC”, ikinukuu barua ya chama hicho kwenda kwa RC Magalula kuelezea namna ya uongozi wa DC huyo ulivyo wa ubabaishaji, hivyo yeye kusema ililenga kumchafua.

 

Katika mazungumzo ya njia ya simu Agosti 23 mwaka huu, yaliyodumu kwa zaidi ya dakika 20, mkuu huyo wa wilaya hakutaka kumpa nafasi ya kuzungumza mwandishi huyo isipokuwa kumshambulia moja kwa moja.

 

“Hivi wewe Victor unanitafuta nini? Unadiriki kutumia kalamu yako kunichafua siyo? Unatumiwa na huyo kiongozi wa CUF kunichafua mimi. Nataka kukueleza nimekuwa DC kwa muda mrefu wala sikuanzia hapa (Geita). Mwambie huyo Malugu kwamba ofisi yangu haina muda wa kujibu barua zake…Na kama huyo Malugu ana ndoto za kuwa DC, mwambie hataupata hadi anaingia kaburini. Hakuna rais wa kumteua akae akijua,” alisema.

DC apoteza msafara wa Mwenge

Katika hali isiyokuwa ya kawaida, mbio za Mwenge wa Uhuru ziliingia dosari mara mbili wilayani Geita, baada ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Manzie Mangochie kuupoteza msafara na risala iliyokuwa imeandaliwa.

 

Kitendo hicho, kilichosababisha kiongozi wa mbio za Mwenge kitaifa, Kapteni Honest Mwanossa, kushindwa kuzindua miradi ya maendeleo.

 

Tukio hilo lililotokea juzi saa 10 jioni lilisababisha msafara huo kusimama kwa muda wa dakika 10 katika kijiji cha Ngula, kitendo ambacho kilionekana wazi kumkera Kapteni Mwanossa na kutoa karipio kali kwa DC huyo.

 

Msafara huo, ulishindwa kuzindua mradi wa kikundi cha kuweka na kukopa cha Nyamalimbe, ambacho kilitarajia kukaguliwa na kiongozi wa mbio hizo, kabla ya kuondoka saa 11 kwenda kukagua shamba la mihogo katika Kijiji cha Ngula.


Kapteni Mwanossa, aliamua kuusimamisha msafara huo baada ya kupita kundi kubwa la wananchi waliokuwa wamejiandaa kuupokea Mwenge wa Uhuru, wakiwa wamejipanga pembeni mwa barabara.

Gazeti la Mtanzania Agosti 28, 2012

Kiongozi wa mbio za Mwenge amgwaya DC

KATIKA hali inayoonesha nidhamu ya woga, Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa, Kapteni Honest Mwanossa, amemsafisha Mkuu wa Wilaya (DC) ya Geita, Manzie Mangochie mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, Said Magalula, kuhusu kudaiwa kupoteza msafara wa mwenge wilayani kwake.


Kapteni Mwanossa alimweleza mkuu huyo wa mkoa kuwa taarifa alizozisikia katika vyombo vya habari ni za uzushi na hakuna mradi uliopitilizwa ingawa alikiri kuwepo kwa mradi huo aliodai kwamba baadaye ulifutwa katika ratiba.


Mwanossa alitoa kauli hiyo wakati akitoa shukrani zake kwa Mkuu wa Mkoa wa Geita katika viwanja vya Shule ya Msingi Chato kabla ya kuendelea na mbio hizo katika Mkoa wa Kagera.


“Baba yangu, Mkuu wa Mkoa Magalula, uliyoyasikia sio ya ukweli, tumekimbiza vizuri mwenge wetu wa uhuru katika Wilaya ya Geita, ule mradi ulikuwepo, lakini kumbe ulifutwa kwenye ratiba kwa hiyo hakuna kilichoharibika… tumeshirikiana vizuri, uliyoyasikia ni ya kupuuza,’’ alisema Mwanossa na kusababisha miguno kutoka kwa baadhi ya watu waliokuwapo kwenye ziara hiyo mkoani Geita.

Tanzania Daima

Septemba 3, 2012


CCM yapinga maagizo ya DC

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Geita, Joseph Musukuma, amepiga marufuku utaratibu wa Mkuu wa Wilaya hiyo, Omary Mangochie, wa kuwazuia wafanyabiashara kufunga maduka siku ya Alhamisi na kuyafungua saa nne asubuhi kwa ajili ya kufanya usafi katika maeneo yao. Musukuma alitoa agizo hilo jana wakati wa majumuisho ya ziara yake ya kukagua miradi mbalimbali na kuwawajibisha viongozi wanaokosa uadilifu kwa kula fedha za umma ambapo alitoa ruhusa kwa wananchi wa mkoa huo kufungua biashara yao siku hiyo.


“Kuanzia leo mimi kama Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita na kwa rungu nililopewa na chama natangaza rasmi kuanzia leo hakuna cha ‘Mangochie Day’ hapa, hiyo kazi waachiwe mabwana afya tumewaajiri kwa kazi hiyo… mtu akikusumbua kwamba umefungua duka leo siku ya usafi nipigie simu nidili naye,” alisema. Kauli hiyo ilionekana kuwafurahisha wananchi wengi hivyo walijikuta wakishangilia kwa kumuita ‘jembe…..jembe…’


Kwa upande wake, mkuu wa wilaya hiyo, alilaani kitendo cha mwenyekiti huyo kuingilia madaraka hayo bila makubaliano na kusema huo si uongozi bali ni ubabe, kwani hatua hiyo ililenga kuhakikisha mji wa Geita unakuwa katika mazingira safi.


“Nimeshangazwa na taarifa hiyo; huyu mwenyekiti anasumbuliwa na utoto, hiyo siyo akili ya kiongozi mwadilifu. Wewe utazuiaje mipango ya serikali kwa Katiba ipi na utaratibu upi, kwa mujibu wa katiba kwa nafasi yake hana mamlaka ya kuzuia huo mpango,” alisema

Gazeti Tanzania Daima

Desemba 11, 2012


2084 Total Views 3 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!