Demokrasia iliyotundikwa msalabani

 

Mwaka 2015 kuelekea Uchaguzi Mkuu wa taifa letu la Tanzania, niliandika makala
nyingi katika gazeti hili la JAMHURI. Makala zangu zilikuwa zinakosoa mwenendo
wa chama tawala (CCM).
Sihitaji kusimulia kilichonitokea lakini inatosha kudokeza kiduchu: ‘Niliambulia
vitisho vya kuondolewa uhai wangu.’ Nilijiuliza maswali mengi sana. Je, ni kweli
kwamba kuikosoa Serikali ni dhambi? Na kuisifia ni utukufu? Je, ni kweli kwamba
kukikosoa chama tawala ni dhambi? Kama kukisifia chama tawala ni utukufu kwa
nini kukikosoa iwe dhambi?
Ni maswali mepesi kujibika lakini yanahitaji busara kuyajibu. Nikiwa katika hali ya
kujiuliza maswali mengi nilikutana na nasaha ya mwanaharakati wa Afrika Kusini,
Steve Biko. Mwanaharakati huyu, alipata misukosuko katika taifa lake, alipata
kunena nasaha hii; “Ni bora ukaishi miaka michache duniani jina lako likabaki
linaishi kwa wema na haki duniani kuliko kuishi miaka mingi duniani na ukatoweka
kama mzoga.”
Katika maisha yangu namwomba Mungu vitu vitatu. Kitu cha kwanza, namwomba
Mungu anijalie kukiishi kile ninachokiandika na ninachokizungumza. Kitu cha pili,
namwomba Mungu anijalie fadhila ya unyenyekevu. Kitu cha tatu, namwomba
Mungu anijalie nife kifodini.
Niko tayari kufa nikitetea haki za wanyonge, uhifadhi bora wa mazingira,
demokrasia safi, siasa safi na utawala bora. Niko tayari kufa huku nikiitetea,
kuipenda na kuilinda imani Katoliki. Mimi si mwanasiasa, sihitaji kuwa
mwanasiasa. Kuwa mwanasiasa katika nchi za Kiafrika ni gharama sana. Mimi ni
mwanasaikolojia, mtunzi wa vitabu vya mageuzi ya kifikra na mtunzi wa vitabu vya
imani Katoliki.
Leo wasomaji wangu wengi mnaweza kujiuliza swali hili: Leo Bhoke ametoka
kwenye makala za mageuzi ya kifikra mpaka kwenye makala za siasa?
Ninafahamu kwamba ninao wasomaji zaidi ya 600 katika ukurasa wangu wa
‘TUZUNGUMZE’ ambao ninawasiliana nao kila mara. Gazeti hili la JAMHURI
limeniongezea familia kubwa sana.
Sasa kila mkoa nina mwanafamilia, hii ni zawadi ya familia takatifu niliyoipata
katika gazeti hili la JAMHURI. Shukrani zangu za dhati nazielekeza kwa Deodatus
Balile na Manyerere Jackton kwa kuanzisha gazeti ambalo limenikutanisha na
Watanzania ambao sasa ni wanafamilia wangu.
Mimi ni Mtanzania, ninayo haki ya kikatiba ya kutoa maoni yangu katika Taifa
langu, bila kujali maoni yangu yatapuuzwa ama yatapokewa. Nazungumza
kuhusu kile ninachokiona kikitokea katika Taifa langu, katika makala hii nafahamu
nitatofautiana na baadhi ya watu kimawazo hasa watawala wasio na hadhi ya

kiutawala na wasomi wasio na hadhi ya kisomi.
Furaha yangu ni kuona natofautiana na walio wengi, kwani katika kutofautiana
nao nitanufaika kwa kujifunza mwono wa fikra zao thabiti ama fikra zao dhaifu.
Mwanasayansi Sir Isaack Newton (1642-17272) anasema; “Mkituona
tumesimama juu, ujue tumesimama kwenye mabega ya miamba iliyotutangulia na
kama katika maisha yangu nimefanikiwa kuona mbali kuliko watu wengine ni kwa
sababu ya kusimama mabegani mwa watu wakubwa.”
Historia yetu kutoka ukoloni hadi leo ni shule ya awali mpaka chuo kikuu ya
mafunzo ya amali za maisha, umakini, fikra na utendaji. Tulipotoka ni mbali,
tujipime na tujitafakari. Tanzania ni yetu, wa kuiua ni sisi Watanzania wenyewe na
wa kuijenga ni sisi wenyewe. Maisha yana ladha pale tu tunapotofautiana
mitazamo.
Maisha hayawezi kuwa na ladha kama mitazamo yetu itafanana. Tukifanana
mitazamo tutakuwa kama wanyamapori wa mwituni wajulikanao kama nyumbu.
Kuna mafanikio makubwa katika kutofautiana mitazamo.
Maana yangu ni kwamba; huwezi kunilazimisha nikubaliane na mtazamo wako
kama mtazamo wako hauna vigezo vya kunishawishi nikubaliane nao. Hali
kadhalika, mimi pia siwezi kukulazimisha ukubaliane na mtazamo wangu kama
mtazamo wangu hauna vigezo vya kukushawishi ukubaliane nao.
Ni kweli kwamba binadamu wote ni sawa, lakini uwezo wa kufikiri na kufikia
uhalisia wa mambo hutofautiana. Mawazo aliyonayo mtu huweza kumtofautisha
na mtu mwingine. Ili maisha yako yawe na ladha, lazima yapate mkosoaji.
Binadamu ni mkosoaji na mkosolewa. Kukosolewa ni kuambiwa ukweli mwingine
tofauti na ule ulioushikilia ama unaouamini wewe. Kila binadamu anaishi na
falsafa yake awe anaijua au haijui, bado ni falsafa. Ikitokea mtu kwa sababu ya
ujinga wake asielewe anaishi falsafa gani ya maisha, hilo litakuwa ni tatizo lake
binafsi na siyo tatizo la falsafa anayoishi…
Tukubaliane wote kuwa hakuna binadamu aliyekamilika, kama yupo binadamu
aliyekamilika basi huyo atakuwa siyo binadamu aliyeumbwa na Mungu. Kila
binadamu ana ujinga wake, unapokosolewa ni kama unaoneshwa ujinga wako
ulionao. Kwa bahati mbaya siyo kila binadamu anaweza kuuona ujinga wake ama
kuukubali ujinga huo.
Demokrasia ni kutofautiana kimawazo, iwapo nchi inafuata mfumo wa demokrasia
basi imekubali watu wake kutofautiana mawazo. Demokrasia haina tofauti na
mchezo wa mpira wa miguu, kila timu lazima icheze kwa bidii ili ishinde. Hijawahi
kutokea wachezaji wa timu moja kufungwa miguu uwanjani huku wenzao
wakicheza.
Mwalimu Nyerere anasema hivi; “Demokrasia ya kweli ni lazima ihitaji kila mtu
aweze kusema kwa uhuru kabisa na mawazo ya kila mtu lazima yasikilizwe, hata
kama mawazo ya mtu huyo hayapendwi kiasi gani au walio wengi wanadhani
amepotea kiasi gani, si kitu.”

Misingi ya demokrasia inafundisha kwamba kiongozi aliyeingia madarakani
kidemokrasia hawezi kutaka kuongoza bila kufuata demokrasia iliyomweka
madarakani. Nje ya demokrasia uongozi wake hauwezi kuwa salama na mihimili
mingine haiwezi kuwa salama.
Ningeulizwa leo kama Tanzania kuna demokrasia au hakuna, ningejibu ya kuwa
hakuna demokrasia, kuna kivuli cha demokrasia. Haiwezekani leo Bunge letu
tukufu lisirushwe ‘live’ lakini cherekochereko za ndoa zirushwe ‘live’.
Hii ni aibu! Mimi ni miongoni mwa Watanzania walionyimwa fursa ya kupima
uwezo na fikra za wabunge wetu. Tunao wabunge ambao wawapo bungeni,
ajenda yao kubwa ni kusifia kazi za rais tu. Tunao wabunge ambao hawana
uwezo wa kuibua mawazo jengefu ya kulikwamua Taifa letu kutoka kwenye
kongwa la umaskini.
Taswira ya kisiasa katika Taifa letu sasa hivi haiko salama. Hilo liko wazi, sihitaji
kuyasimulia mateso wanayopata baadhi ya viongozi wa upinzani. Watanzania
wote tunayaona. Dunia inayaona. Vyama shindani sasa hivi wanapitishwa kwenye
tanuri la moto. Wengine wanaungua kwa kuuguza majeraha ya risasi. Wengine
wanaungua kwa kusota rumande. Wengine wanaungua kwa kuuguza majeraha
ya mapanga. Wengine wanatoweka katika mazingira tatanishi. Waandishi wa
habari wengine wametoweka. Wengine sasa hivi wameamua kuwa waandishi wa
kuisifia Serikali tu.
Hapana hii si Tanzania tunayotakiwa kuijenga. Nchi ya waoga wa kuthubutu. Nchi
ya wanafiki. Nchi ya kujipendekeza kwa watawala. Nchi ya kukubali bila kuhoji.
Inatosha kuishauri Serikali kusoma alama za nyakati. Kuna maisha baada ya
miaka mitano ya uongozi. Kuna maisha baada ya miaka kumi ya uongozi.
Mungu alipompa Malaika Lucefer cheo cha uwaziri mkuu mbinguni, Lucifer
alijisahau, alidhani kwamba Mungu hatamtoa tena kutoka kwenye nafasi yake ya
uwaziri mkuu. Jambo la kukumbuka hapa ni kwamba; kuna wakati shetani alikuwa
malaika mbinguni. Shetani kabla hajaondolewa mbinguni alikuwa malaika mkuu.
Ni kwamba yeye ndiye aliyekuwa waziri mkuu katika serikali ya Mungu. Akalewa
madaraka ya uwaziri mkuu. Akajiona anaweza kuiongoza dunia na mbingu.
Akatamani kuabudiwa kama Mungu Mwenyezi anavyoabudiwa. Akajiona anaweza
kuumba. Akajaa kiburi na majivuno. Mwenyezi Mungu akachukizwa na nyendo za
shetani, akamuondoa kutoka kwenye ufalme wake wa milele. Kisa cha shetani
kuondolewa mbinguni ni majivuno.
Nabii Isaya anatufunulia siri hiyo. Tunasoma hivi, ”Jinsi ulivyoanguka kutoka
mbinguni, ewe nyota ya alfajiri, mwana wa asubuhi! Jinsi ulivyokatwa ewe
uliyewaangusha mataifa. Nawe ulisema moyoni, ‘Nitapanda mpaka mbinguni,
nitakiinua kiti changu juu kuliko nyota za Mungu: Nami nitaketi juu ya mlima wa
mkutano, katika pande za mwisho za kaskazini’. Nitapaa kupita vimo vya
mawingu, nitafanana na yeye aliye juu’ (Isaya 14:12-14). Tuogope kulewa
madaraka tuwapo madarakani.

Siasa siyo uadui, siasa ni hoja, siasa ni sehemu ya maisha ya binadamu.

Mwanafalsafa Hegel anasema binadamu ni mnyama wa kisiasa. Hizi siasa za
kushambuliana kwa mapanga, risasi ni siasa zinazopandikiza chuki ya kudumu
kwa kizazi hiki na kinachokuja. Ni hatari taifa kuwasikiliza watu fulani na
kuwapuuza watu baadhi. Ni hatari kwa taifa kuyaamini mawazo fulani na
kuyapuuza baadhi ya mawazo.
Ni hatari kwa taifa kuwachukia wasema ukweli. Ni hatari katika taifa kuwa na
genge la watu wanaojulikana na wasiojulikana. Kuna matukio ya Watanzania
wenzetu kutekwa, kuteswa na wengine wanauawa. Kisa siasa! Nyumba
tunayoijenga ni moja, tung’ang’ania fito za nini?
Nihitimishe makala yangu kwa kuwaomba wasomi wa nchi yetu wazitoe akili zao
likizo na kuzileta kwenye taifa lao. Taifa letu linahitaji mgongano wa kifikra.
Mgongano huu wa kifikra utaliingiza taifa katika mijadala itakayoleta mawazo
mbadala.
Binafsi huwa natofoutiana na mitazamo ya baadhi ya viongozi wetu. Wapo baadhi
ya viongozi wameishia darasa la saba, au kidato cha nne au kidato cha sita. Huyu
kiongozi yeye anapenda kuitwa mheshimiwa. Ukimwita jina tofouti na mheshimiwa
ni kosa la kinidhamu.
Lakini ukiingia ndani ya kichwa cha kiongozi huyu utakuta ana mawazo ya
kimaandazi-maandazi. Sasa kiongozi mwenye mawazo ya kimaandazi-maandazi
anatatoa wapi mawazo jengefu ya kifikra?
Niwaombe sasa wanazuoni na wasomi mbalimbali walioko katika taifa tuanzishe
mijadala ya mawazo jengefu katika midahalo ya kitaifa, kwenye vyombo
mbalimbali vya habari kama magazeti, redio na televisheni. Lengo kuu likiwa ni
kuijenga Tanzania yenye ushindani wa kifikra.
Nchi yetu inahitaji kujengwa kwa misingi imara kutoka kwetu, ni jukumu letu
kuijenga nchi yetu imara kwa faida yetu na kizazi kijacho.