Demokrasia ni mfumo wa utawala ambao mamlaka yake yanatokana na matakwa ya umma. Ni mfumo wa asasi au chama kinachoshirikisha watu kutoa uamuzi kwenye masuala yanayohusu maendeleo.

Katika fasili nyepesi, demokrasia ni uhuru na uwezo wa watu katika kutawala mwenendo na mambo yanayohusu maisha yao kwa kutumia vikao vilivyowekwa kikatiba na kisheria. Kutokana na maelezo haya, utaona demokrasia si aina moja. Kila chama, asasi au nchi ina demokrasia yake.

Nchi yetu imepata kupita katika mfumo wa vyama vingi, chama kimoja na sasa tena katika vyama vingi vya siasa. Kila chama kinayo demokrasia yake. Katika mwenendo huu, demokrasia si neno au jambo geni katika masikio ya Watanzania.

Pamoja na uenyeji wake, bado inaonekana kama dhana mpya ambayo haijazoeleka na kueleweka vizuri kwa viongozi, wanachama na raia wa nchi hii. Hali hii inatia shaka kutokana na kauli zinazotolewa na wanasiasa na majibu kutoka kwa serikali na wananchi wapendao usalama na amani.

Hivi ninavyozungumza, tunavyo vyama vya siasa vipatavyo 22 na kila chama katika itikadi yake inazungumzia demokrasia. Kila uchao baadhi ya viongozi wa vyama hivi wanalalamika. “Demokrasia inaminywa. Tunahitaji kujikomboa na kuleta mabadiliko ya kupata habari na kuzungumza.”

Wengine katika vyama hivi wanaeleza hapana. “Demokrasia haiminywi. Taratibu za kusimamia na kutekeleza misingi ya demokrasia inafuatwa kikatiba na kisheria.” Ni dhahiri, kauli mbili hizi zinaonyesha hali ya kupingana kisiasa katika fasili ya neno demokrasia.

Upinganaji huu haustahili kupewa nafasi ya mabishano na kuwajaza hofu wananchi. Mazungumzo ya hiyari na salama yaanzishwe baina yao, kupoza joto la kisiasa na kuzima moto unaokusudiwa kuleta zahama nchini. Kwani, “mwanzo wa ngoma ni lele.” Na hizo lele ni kama ninaanza kuzisikia.

Katika FASIHI FASAHA ya juma lililopita nilisema kauli na matendo ya baadhi ya viongozi wetu nchini yasiwe chachu, machocheo au nyenzo za kukomoa, kukinza au kusaliti chombo chochote katika harakati zake. Na leo ninasema wanachama na wananchi tusikubali kutashititiwa na kupata taharuki tukatumbukia katika shimo la moto.

Viongozi kumbukeni kutamka maneno ya maudhi na vitisho kwa wafuasi wenu si busara hata chembe. Zaidi ni kujenga chuki za milele katika jamii mbalimbali nchini. Pia kuwapa njia maadui wa nchi kufuta historia na utamaduni wetu uliotukuka duniani kote.

Ukweli sifurahishwi na kauli tata zitolewazo na baadhi ya viongozi wetu. Na sina mzuka au haja ya kuzikariri na kuzitaja hapa tena. Wasemao na wasikilizao wanatambua nisemayo. Uzalendo wangu haunishawishi kulea kauli na matendo yao. Je, wewe upo wapi? Bado kujitambua? Badilika.

Ni wazi silaha inachoma, inakata na inaua. Sumu inadhuru au kuua. Sumu si shubiri kutibu mgonjwa. Na maneno makali ni kama sumu au silaha. Viongozi mtafakari kwanza kabla ya kutoa kauli. Msihadaike na neno demokrasia kwa utamu na uzuri wa kutamka. Lina hatari.

Ikumbukwe kila taifa lina utamaduni, mila na desturi zake ambazo zinatengeneza mfumo wa maelewano na makubaliano kwa masilahi ya watu wake. 

Kisiasa tunaweza kusema kama demokrasia. Ndiyo maana kila taifa lina demokrasia yake kwa masilahi ya wananchi wake.

Watanzania hatuna budi tumaizi kila nchi ina majira na mazingira yake, utamaduni na demokrasia yake. Vipi utamaduni wa nchi za Ulaya ukubalike Tanzania?  Mbona demokrasia yetu haikubaliki katika nchi za Ulaya? Tusikubali kufanywa mazumbukuku na kujinadi hadharani kwa kipande cha mkate.

Wanachama wa vyama vya siasa na wananchi wenzangu tuwe na hadhari tunaposikiliza kauli za viongozi hawa. 

Ni bora mara mia kuwa mdadisi kuliko kuwa mtii wa kila kauli. Utiifu unahitaji nidhamu ya dhati, si nidhamu ya woga. Tubadilike, tuwe wakweli na wathubutu wa maendeleo yetu.

By Jamhuri