Demokrasia ni uhuru na uwezo wa watu katika kutawala mwenendo na mambo yote yanayohusu maisha yao kwa kutumia vikao vilivyowekwa kikatiba na kisheria.

Demokrasia na haki za binadamu si misamiati mipya kwa Watanzania kuelewa na kutumia katika harakati zao za kulinda na kuboresha kanuni za haki, usawa na amani katika taifa lao huru.

Ni misamiati kongwe iliyowapa jeuri Watanzania kuweza kusaidia nchi jirani kupata uhuru wao na kujenga utulivu wa nchi zao. Huo ndiyo ujirani mwema ambao leo Watanzania tunajivunia.

Demokrasia iliasisiwa Ulaya na Wazungu. Wakatuzunguka katika mambo ya elimu, itikadi, mazingira, uchumi na maendeleo ya binadamu.

Hakika Wazungu wale wakasambaza demokrasia katika mabara ya Asia, Afrika, Australia, Marekani na Ulaya kwenyewe. Waliopokea demokrasia kila mahali wakazuka na tafsiri yao. Leo demokrasia inazungumzwa na kutekelezwa kiaina aina kutokana na mahitaji yao.

Wajuzi wa mambo wanasema kuwa demokrasia ni mfumo wa utawala ambao mamlaka yake yanatokana na matakwa ya umma. Ni mfumo wa asasi au chama kinachoshirikisha watu kutoa uamuzi kwenye masuala yanayohusu maendeleo.

Yamkini demokrasia ni mfumo wa utawala wenye mamlaka na matakwa ya umma. Ni utawala wa watu kwa ajili ya watu na kwa manufaa ya watu. Ni utawala unaoheshimu na kuzingatia haki za binadamu.

Vinara wakuu wa matumizi ya demokrasia ni wanasiasa, wanaharakati wa siasa na wanasheria katika vyama vyao vya siasa na katika asasi zao za jamii, kupigania haki za binadamu. Kwenye majukwaa ndiko kwenye ulimbo.

Wakulima, wafanyakazi, wafanyabiashara na wale wenzangu mimi pangu pakavu tia mchuzi, wamo nje – ndani kuzungumzia demokrasia. Waandishi wa habari ndio wapambe wakubwa wa kutangaza misamiati hii kupitia vyombo vyao vya habari, kama vile magazeti, redio, runinga na kadhalika.

Katika kutekeleza demokrasia duniani, ikaonekana kuna masuala ya haki, usawa na ubinadamu. Hivyo ipo haja ya kuwa na utaratibu ambao utaheshimu, utalinda na utaondoa uonevu na dhuluma kwa binadamu.

Desemba 10, 1948 Baraza la Umoja wa Mataifa lilitoa taarifa rasmi juu ya tangazo la dunia la haki za binadamu. Tangazo hilo linataja haki za binadamu katika vifungu thelathini, haki ambazo binadamu wanastahili kuwa nazo katika jamii wanamoishi.

Tangazo linakiri heshima ya asili na haki sawa kwa binadamu wote na kwamba heshima na usawa ndiyo msingi wa uhuru, haki na amani duniani. Linazidi kusema wazi kwamba kutojali na kudharau haki za binadamu ndicho chanzo cha vitendo vya kishenzi ambavyo vimeharibu dhamiri ya binadamu na kuleta uhasama wa kitabaka.

Baadhi ya haki za binadamu zinazotajwa: “Watu wote wamezaliwa huru, hadhi na haki zao sawa. Wote wamejaliwa akili na dhamiri, hivyo yapasa watendeane kidugu.”

By Jamhuri