Katika uchaguzi wa Urais kule Marekani mwaka huu 2016, mjini Pheledaphia kulikuwa na zomeazomea wakati Chama cha Democrats kikimteua Hillary Clinton kuwa mgombea Urais wake.

Rais Obama alisema hivi, “Don’t boo, vote” you’ve got to get in the arena …because democracy isn’t a spectator sport….”. Haya ni maneno mazito kwa wapenda demokrasia wowote wale. Siyo suala la kuangalia ukiwa pembezoni eti ngoja tuone watafanyaje bali ni suala la kutenda (participating not mere observing). Ni fundisho tosha kwa nchi za kiafrika zinazojenga demokrasia halisi. Uchaguzi maana yake ni waliojiandikisha waende wakapige kura. Huko ndiyo kuwajibika na siyo kulalamikia matokeo baada ya uchaguzi kumalizika. 

Kule Marekani, vijana wengi sana katika Chama cha Democrats walimtaka Mzee Bernie Sanders kama chaguo lao. Lakini chama kikamteua Bibi Hillary Clinton na hapo ukatokea mtafaruku ndani ya chama. 

Kwa upande wa Republicans, wao walimtaka Ted Cruz, ni mwenzao vigogo wote. Republicans walisema sera za Trump si njema kwa nchi ile. Kuna watu hapa nchini Tanzania wamediriki kusema wazi wazi, Trump angekuwa CCM angekatwa. Kwanza watu wanaamini mgombea wa chama awe mtu anayekubalika, atakayeleta ushindi, na ana historia gani ndani ya chama. Trump yote hayo hakuwa nayo ndiyo sababu vigogo kama Marais wastaafu akina Bush (Baba na Mwana Rais wa 41 na wa 43) walijiweka kando katika uchaguzi wa Trump. Pamoja na yote hayo hao marepublicans walimteua TRUMP kupeperusha bendera yao katika uchaguzi ule na amefanya kweli ameipeperusha bendera za Republicans na ameshinda sasa ndiye Rais Mteule wa Marekani. 

Kwa utaratibu wa demokrasia, chama kikishateua mgombea inafuata sasa nidhamu ya chama. Wajumbe wote huungana na kusimama nyuma ya mteuliwa wa Chama. Makundi yanakoma na unatokea mshikamano wa kukipiku chama kingine watakachopambana nacho kwenye uchaguzi mkuu. Demokrats wamefanya hivyo na Republicans wamefanya hivyo katika uchaguzi wa mwaka huu. Pamoja na vigogo wa Republican kumsusia Trump, Republicans kama chama walishikamana. 

Hapa kwetu hali namna hiyo haitokei. Tulijionea nini kilitokea kule Dodoma pale wengi waliokiimba “tuna imani na Lowassa, oya oya oya”. Kumbe chama cha CCM kikamteua Magufuli lakini tumeona badala ya Lowassa kufanya kama Bernie Sanders kumuunga mkono mteule wa chama, yeye akakihama chama na wafuasi kadhaa akatoka nao wakaenda upinzani na huko akagombea Urais. Kwenye demokrasia iliyokomaa kama nchi za Magharibi hilo kamwe halitokei. Ni imani ya chama inayowaunganisha wala siyo madaraka.  Ndiyo maana sasa marepublicans wanasema “Trump will unify their party”

Huu ndio ustaarabu wa demokrasia katika nchi za wenzetu. Kwa ukomavu namna hiyo Rais Obama aliwatahadharisha wajumbe wa Mkutano Mkuu ule wa Chama cha Democrats kuwa suala siyo KUZOMEA bali ni KUPIGA KURA. Kwa vile kiongozi Mzee Bernie Sanders alishahutubia mkutano ule na kuahidi kumuunga mkono Hillary Clinton na akawaomba wafuasi wake wote waungane naye katika uamuzi ule ndipo Rais Obama alikazia ombi lile kwa maneno haya, “If you are serious about democracy, you can’t afford to stay home just because she might not align with you on every issue” (President Obama on 22 July 2016 in Philadelphia while endorsing Hillary). 

Kutokana na ombi hili la Rais Obama wa Marekani mimi kwa tafsiri yangu isiyokuwa rasmi ninasema hivi, “MSIZOMEE, KAPIGENI KURA”. Mnapaswa kuingia katika ulingo wa mapambano. Demokrasia siyo mchezo wa kuangalia mkiwa mmekaa nje ya uwanja wa mapambano. Inabidi kila aliyejiandikisha ajitokeze kupiga kura yake. Ndiyo kuwajibika kwenyewe. 

Baada ya kusema hivyo, Rais Obama alimalizia hotuba yake ile kwa kumuunga mkono Hillary Clinton, mteuliwa wa Chama chake cha Democrats. Ndipo akawatahadharisha wana demokrats akiwaasa “basi hamuwezi kubaki majumbani bila kupiga kura eti kwa vile mnasigana na Clinton katika hili au lile”. Ndipo akawatolea uvivu na akawahimiza “don’t boo, vote” yaani MSIZOMEE KAPIGENI KURA”. 

Kule Visiwani eti walisusia marudio ya kura kwa kile wanachokiita kusigana na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi! Laity wangejitokeza wote kwenda kupiga kura, ninaamini matokeo yangekua tofauti. Sasa kuwaendea wa Magharibi kuisema Tanzania kutasaidia nini? Hukupiga Kura, mambo yamekwisha Donald Trump atacheka tu na kuendelea kukebehi waafrika kwa yale maneno yake “in my opinion most of these African countries ought to be recolonized again for another 100 years because they know nothing bout leadership and self governance” (kutoka WatsApp AT & T Lte: Search – at 2:20pm). 

Matamshi haya ni baada tu ya kuchaguliwa kwake. Sasa wewe mtanzania unakwenda kumwomba asaidie kutatua tatizo lako la uchaguzi si atakudharau zaidi? Nidhamu ya chama ni muhimu sana. Maamuzi ya chama yanapaswa kutekelezwa na wanachama wote. Demokrasia maana yake ndiyo hiyo – “wengi wape” ni msimamo wa chama, kushikamana pamoja katika utekelezaji wa maamuzi ya chama. 

Katika vyama vya siasa barani Afrika, viongozi wanaitafsiri demokrasia kwa namna inavyowanufaisha wao. Wakihitilafiana tu ndani ya chama kunatokea mfarakano. Ama watu wanajitoa ndani ya chama na kuanzisha chama chao au wanasusa kupiga kura. 

Kule Dodoma baada ya kutangazwa jina la Mhesh. John Pombe Joseph Magufuli wapo waliochukizwa na uteuzi ule pamoja na kuwa viongozi katika Halmashauri Kuu ya chama na wengine hata katika Kamati Kuu. Kitendo chao cha kutokupokea uteuzi wa chama, ni dhahiri utovu wa nidhamu ndani ya Chama. Minong’ono inaanzia hapo. Kutokuridhika kunazua, manung’uniko. Kunaanzisha makundi na hata tabia ya kusemana na hapo mitandao inazushwa.

Hayo ndiyo yanaonesha utamaduni wetu waafrika uko tofauti sana na utamaduni wa wenzetu wa Magharibi. Suala la umimi linaingia sana katika nchi za dunia ya tatu. Hivi ikitokea hali hii mimi nitakuwa wapi? Mimi nitakuwa nani? Hapo ndipo uzalendo unapotushinda. Basi tafsiri ya neno demokrasia inakuwa tofauti na inavyotafsiriwa kule nchi za Magharibi. Hakuna kiongozi Mwafrika anaweza kumezea kama yule Mzee Bernie Sanders kwa kutunza nidhamu ya chama. 

Kama maneno yale ya Rais Obama kuwahimiza wamarekani wajitokeze kwa wingi wapige kura zao, wala wasibaki majumbani kwa kisingizo chochote kile yangefuatwa nafikiri idadi ya wapiga kura ingekuwa kubwa. 

Hii maana yake ni nini? Mwaka jana katika uchaguzi ule mkuu wa hapa kwetu, wananchi waliojiandikisha katika daftari la wapiga kura walikuwa watu 22,658,247 kwa huku Bara na watu 503,193 kule Visiwani. Basi wapiga kura wangekuwa jumla ya watu 23,161,440. Lakini wakati wa kupiga kura ni wananchi 15,596,110 ndio waliojitokeza na hii ni sawa na asilimia 67.30 ya walioandikishwa. 

 

>>ITAENDELEA

By Jamhuri