Serikali tunayoihitaji ijayo ilete matulizo kwa hayo yaliyotokea hapa nchini. Watu wajaliwe, waheshimike na wapate kupiga hatua mbele ya hapa walipo. Kwa kutokuwa na uti wa mgongo wa utawala – UTUMISHI WA UMMA mzuri kama hapo zamani hitaji la utawala wa sheria sasa na wakati huu ni la muhimu kweli. 

  Nchini Nigeria na Ghana siasa haikuingilia kubomoa utumishi wa umma uliojengeka enzi za mkoloni (The civil service is intact). Uhabeshi, tunaona, pamoja na matatizo yao yote utumishi wa Shirika lao la Ndege “Ethiopian Air Lines” kamwe haukuingiliwa na wanasiasa – bado linajiendesha kwa faida mpaka leo. Ni fahari ya taifa lile la Uhabeshi. Basi tunahitaji utawala bora ule wa haki na wa kufuata sheria. 

Nina taarifa kutoka kwa Watanzania waliokuwa wakifanya kazi katika mashirika ya UN kule Nigeria na Ghana. Wamesimulia namna taasisi ya kuzuia rushwa ilivyo na meno makali ya kung’ata watumishi wabadhirifu. Mfano mmoja unasema mhitimu mmoja wa chuo kikuu Nigeria aliyeajiriwa katika utumishi iwa umma, kwa sababu ya ndugunaizesheni (kule wanaita nepotism), alipandishwa vyeo haraka haraka na kwa muda wa miaka sita hivi tangu amalize chuo na kuajiriwa, akaja kuwa Katibu Mkuu katika moja ya wizara. Ikajagundulika alijinufaisha, akawa na magari zaidi ya moja, akajenga na majumba kadhaa (estate na kupangisha).

Serikali kupitia taasisi ya kuzuia rushwa ilimkalisha kikao na kumuuliza ajieleze magari yale aliyapataje na majumba yale aliyajenga kwa mtaji upi? Walimuonesha kimahesabu mshahara wake pamoja na marupurupu yote kwa miaka yote sita ya kazi bila kukatwa kodi, bila kutoa fedha za mafuta ya gari na bila kutoa hata senti ya chakula wala mavazi kwa familia yake, angepata jumla ya naira kadhaa mimi naita X wakataja (gross amount). Fedha hizo zingetosha kununua gari/aina ya Ford Escort na nyumba moja bungalow tu.

  Sasa alikuwa anakula, anavaa, anakunywa, analipa karo za shule hivyo kipato chake ni dhahiri kilikuwa chini ya hiyo gross ya X baada ya kutoa matumizi halisi yale. Angebakiwa na Y naira. Je, kwa fedha hizi za miaka sita ya utumishi wake ule angewezaje kununua magari yale ya kifahari na kujenga maestet (majumba kadhaa ya kupangisha)?

Katibu Mkuu kijana yule alitokwa na jasho na kuzirai mbele ya jopo la taasisi ile ya kuzuia rushwa! Niliambiwa alinyang’anywa magari mengine, kutaifishwa nyumba zake na akafukuzwa kazi kutoka utumishi wa umma na kufungwa jela miaka kadhaa kazi ngumu! Gari moja na nyumba moja waliachiwa familia yake.  Hayo ya huko Afrika Magharibi. 

  Hapa kwetu Serikali ya awamu ya kwanza ya Mwalimu imekuaje juu ya RUSHWA? Mwalimu amesema sana juu ya rushwa katika NYUFA uk. 15-22 pale alipoongea na wanahabari katika Hoteli ya Kilimanjaro tarehe 13 Machi, 1995 kwa kifupi alisema, “hatukuwa tunatania, ….Kiongozi wetu anakula rushwa. Anayetoa, aliyepokea Wazanaki wanasema MANZI GA NYANZA” yaani wote wanapata msukosuko. Basi ipo ile hadithi ile ya mmoja wa mawaziri enzi hizo aliyesikika kapokea rushwa na hadithi ya yule Mgiriki aliyepata kujitapa kwa kusema, “mimi Serikali yote ya Tanzania iko mfukoni mwangu”. 

Mwalimu kwa hasira sana anasema namnukuu’ nikasema “mshenzi sana huyo!” (unaweza kujisomea hayo katika ile hotuba yake niliyorejea hapo juu kutoka uk. 15-22 wa kijitabu hicho). 

Siasa ilipoingizwa katika utumishi wa umma kwa kisingizio cha kuwafuta jasho waanzilishi wa harakati za Uhuru enzi za TANU hapo “Civil Service” ikamomonyoka. Ndipo utawala ukaanza kuwa hovyo. Kanuni za utumishi zilikiukwa na hatimaye zikaachwa kabisa kutumika. Kanuni za fedha tunaita “financial regulations” zilikiukwa, kukawa hata “accounting officer” hana udhibiti wa mafungu ya fedha. Kukatokea mvurugano kati ya wataalamu wa fedha, na utawala upande mmoja na wanasiasa waliopigania Uhuru upande mwingine. 

Matokeo ndiyo haya yanatokea, malipo hewa, mikataba mibovu, hakuna mamlaka inayotawala hili au lile. Kuna uamuzi unaokingana hapo. 

  Hapa nikumbushe tu tukio lililowahi kusikika katika Wizara ya Maliasili. Kuna wakati Katibu Mkuu akiitwa Permanent Secretary, Benard Mlokozi (hayati sasa), na Waziri wake akiitwa Ole Saibul (naye hayati) waliwahi kutunishiana msuli hadi kufikia hawaongei wala kushauriana katika ofisi moja.

  Hivi karibuni wizara hiyo hiyo, waziri amehamisha watumishi wakati sheria za utumishi wa umma zinasema wazi kuwa ni Ofisi Kuu ya Utumishi ndiyo pekee yenye madaraka ya kuhamisha mtumishi wa umma. Mvurugano ule ulisababishwa Katibu Mkuu Maliasili kubadilishwa. Hizi naita ni vurugu mechi katika Serikali yetu. 

 Mwaka 1999 Bunge lilipitisha sheria za malipo ya uzeeni zinazojulikana kama Retirement Benefits Act No. 2 of 1999 kwa watumishi wa umma na Retirement Benefits Act No. 3 of 1999 kwa wanasiasa. Kuna mafao tofauti hapo kati ya mtumishi wa umma anayestaafu na mwanasiasa anayestaafu. 

  Kwenye marupurupu ya wanasiasa wastaafu Act No. 3 of 1999 inasema wazi miongoni mwa marupurupu yao. Lipo fungu linaitwa “a winding up allowance of…” hili ni fungu mahususi kwa viongozi wa siasa lakini halipo kwa wastaafu watumishi wa umma.  Ni malipo ya kufungia ofisi anapostaafu kazi ile ya siasa.

 Kuingiza siasa kwenye utumishi kumesababisha ikama katika Idara ya Utumishi kuongezeka sana. Huo ni mzigo kwa walipa kodi. Mabadiliko yarekebishe na hili pia. Siyo suala la chama gani kitatuletea unafuu wa maisha. Hapa ni kuwa Serikali itakayoingia AWAMU YA V ilete mabadiliko kwa wananchi wote.   Mabadiliko muhimu ni kufufua UTUMISHI WA UMMA na kujenga Taifa lisilo na walionacho na wasionacho. Je, hayo yanawezekana? Chama gani kipo tayari kweli kutumikia wananchi wa Tanzania? Mimi siamini katika ushabiki wa kelele za mabadiliko. Ninaamini katika UTU wa mgombea, maadili yake na utayari wake kufufua moyo ule wa kuwainua wahitaji wanyonge wa nchi hii. Moyo aliokuwa nao Baba wa Taifa. Hakujilimbikizia mali ili familia yake ifaidi. Watoto wake wako kama sisi wananchi wa kawaida tu!

Nakubaliana na mtazamo wa Madaraka Nyerere katika Gazeti JAMHURI toleo No. 208 la tarehe 22-28 Sept. uk 17. Amefananisha wapiga kura na mashabiki wa soka. Mashabiki wa klabu za mipira kamwe hawahamihami kutoka klabu moja na kwenda nyingine. 

Mashabiki wa klabu za mpira kamwe hawafuati makocha, hawatafuti wachezaji wala hawafuati viongozi wanaotimkia timu nyinginezo. Wao mapenzi yao kwa klabu ni ya dhati na ya kudumu. Hapo naweza kusema ushabiki ni kama kusadikisha imani (conviction) ya moyo wa ndani ya mhusika. Hivyo nathubutu kusema imani katika chama haifuati mtu. Ni ridhaa ya moyo wako na utii kwa dhamiri yako. 

Kwa mtazamo namna hiyo, uchaguzi wetu mwaka huu usiwe wa ghadhabu au chuki au kisasi kwa hili au lile, bali utawaliwe na IMANI katika dhamira yako mpiga kura. Chagua kwa hiari yako nani unamwona ataweza kukuletea mabadiliko ya maisha. Ni mabadiliko ya kuondoa viongozi wazembe, wababe na wasiojali wananchi.

Ni kufumua mfumo mzima wa UTUMISHI WA UMMA na kujenga imani kwa wanyonge. Kodi yao na maliasili yao viwapatie tija katika maisha. Hapo hapatakuwa na malipo hewa na watumishi hawatakosa mishahara wala stahili zao za likizo, uhamisho au malipo ya uzeeni. Kwa ujumla kutakuwa na utawala wa haki na unaofuata sheria.

 Haya madeni ya walimu, kucheleweshwa kupanda madaraja, kutokubadilishiwa mishahara yao kwa wakati baada ya promosheni ni alama za wazi kuwa hakuna utawala wa haki na wa sheria. Basi anatakiwa rais shupavu wa kuyang’oa maovu haya katika nchi yetu. Na mtu shupavu namna hiyo anaweza kupatikana katika uchaguzi ujao. Tanzania inao viongozi wenye uwezo wa kuleta mabadiliko. Tumesikia kule Geita fedha za mishahara ya walimu eti zimetumika kwa kazi nyingine. Hapo sheria ya utumishi haikufuatwa. Ni makosa makubwa. 

  Nchi zote zilizoendelea wakati kama huu kuna viashiria vinaelekeza mtiririko wa matokeo ya uchaguzi ujao. Wenyewe wanaita “predictions” huku kwetu utabiri namna hiyo haupo. Zipo taasisi kudhaa zimejaribu kuelezea utabiri wao kama uchaguzi ungefanyika hivi sasa matokeo yangekuwaje na kadhalika. Tabiri namna hii hapa nchini haziaminiki.   

  Mimi ninaamini katika usemi kuwa yaliyopita hapa duniani ni historia; yanayotarajiwa kupatikana kwetu yanatazamwa kama ndoto. Uhalisia ni hivi sasa leo hii tunaonaje uchaguzi wa mwaka huu? Bado tuna kazi ya kufanya. Bado tuna hali ya sintofahamu matokeo. Maana kwenye kampeni za Lowassa watu kibao tunawaona kwenye kampeni za Magufuli nako watu kibao; hapo ndipo Mngoni kama mimi anatumia neno “NDINDANI” yaani UTATA yupi ni yupi – “SINTOFAHAMU”.

Nasema mabadiliko siyo kaulimbiu iliyoibuliwa na chama chochote. Mabadiliko yalikuwako, yapo na yatakuja kuwapo huko tuelekeako. Tunaomba tupate mabadiliko ENDELEVU tutoke hapa tulipo kihali na kimaslahi tunyanyuke tuelekee mbele. 

Rafiki yangu mmoja amezoea sana kusema mabadiliko hayakwepeki. Yeye anasema kwa Kiingerea hivi – change is unquepable ni mchanganyiko wa neno la Kiingereza na la Kiswahili. Basi tuombe kujaliwa mang’amuzi asilia (common sense) ili tuweze kuchagua yule atakayetupeleka kwenye mabadiliko sahihi.

Tuwe watulivu (composed) tufuate mlio wa dhamiri zetu ndani yetu. 

Sina shaka Mungu ataongoza tumpigie kura nani katika uchaguzi ujao. “Man proposes but God disposes”. Wafaransa wanasema “I’homme propose, et Dieu dispose” sisi Wangoni tunasema “Bambo chapanga magawila” tusubiri hiyo tarehe 25 Oktoba, tutakapotii dhamiri zetu. Mungu atatupa wa kutuongoza katika nchi hii. Amen. 

By Jamhuri