Diaspora wa kwanza duniani walitoka Ngorongoro

Mhandisi Joshua Mwankunda

Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Profesa Audax Mabulla na Meneja Idara ya Urithi wa Utamadani katika Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) katika Bonde la Olduvai, Mhandisi Joshua Mwanduka; wanazungumzia ugunduzi wa Zinj miaka 60 iliyopita na faida zake kwa Tanzania na ulimwengu.

Mhandisi Mwankunda

Kuadhimisha miaka 60 tangu alipopatikana Zinj ni nafasi muhimu na adhimu katika kuutambulisha umma wa Watanzania na dunia kwa jumla kuhusiana na urithi mkubwa tulionao katika nchi yetu.

Kwa sasa tunazungumzia urithi wa kupatikana Zinj, lakini tuna urithi wa aina nyingi hapa ndani ya eneo la Hifadhi ya Ngorongoro na maeneo mengine katika nchi yetu. Hili tukio [kumbukizi ya Zinj] lina faida kubwa. Kwanza ni kuleta hamasa, kuleta ile hali ya watu kutaka kufahamu habari za Zinj – sambamba na hiyo watafahamishwa urithi mkubwa ambao nchi yetu inao.

Sisi ndani ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro tunaamini ni nafasi nzuri kwa watu kutambua vivutio vingine vinavyopatikana ndani ya eneo hili hasa katika kipindi hiki ambacho urithi wa utamaduni umepata hadhi kubwa, umepata msukumo mzuri – kisiasa, kijamii, kiuchumi juu ya ule urithi wa wanyama tuliouzoea.

Mengi yamezungumzwa kuhusu Zinj alivyopatikana lakini sisi tunaona huu ni wakati mzuri wa kutambulisha urithi wetu wote wa Tanzania kupitia.

Lengo kubwa la maadhimisho haya ni kuleta hamasa ya thamani na umuhimu wa urithi kama huu unapopatikana popote. Uhifadhi upo kwa kila mwananchi, na bila shaka urithi huu ukishatambulika kwa kiwango hiki tunachokwenda nacho sasa litakuwa jambo zuri.

Dunia inavyoitambua Olduvai

Ndani ya eneo la Hifadhi la Ngorongoro tuna vivutio vya aina nyingi. Kuna vivutio vya wanyama wa asilia na urithi wa utamaduni kwa maana ya kushuhudia maeneo kama ya chimbuko la mwanadamu – kitu ambacho unaweza kukiona kwa asilia, lakini pia wageni kupata fursa ya kujifunza maisha ya kawaida ya jamii zinazoishi ndani ya eneo la hifadhi.

Idadi ya wageni kwa ujumla wanaokuja ndani ya eneo la Hifadhi ya Ngorongoro inapanda. Kwenye eneo la urithi wa utamaduni, kwa mfano eneo la Bonde la Olduvai ambako hivi karibuni tulijenga makumbusho nzuri ya kisasa [ilifunguliwa na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan miaka miwili iliyopita] tumeona kuongezeka kwa wageni na faida. Faida tunazopima ni ongezeko la mapato, ufahamu na kuongezeka kwa uhifadhi kwa kile tunachokionyesha ambacho tungependa kiendelee kuwapo kwa muda mrefu kwa maana elimu kwa jamii na watumiaji wa hizi rasilimali. Lakini vilevile tunaangalia kiwango cha wageni kuridhika – kwamba mgeni amekuja na kupata kitu alichotarajia na amekipata na anaporudi [kwao] anaweza kuongelea vizuri kwa wengine na wakazidi kuendelea kuja. Hivyo vitu vyote tumeviona na vinapanda katika eneo hili la Bonde la Olduvai hasa kupitia makumbusho mpya ya kisasa.

Profesa Audax Mabulla

Ni mkakati wa serikali na ni jukumu ambalo Wizara ya Maliasili na Utalii imepewa na inaliona. Wakaona kwamba nchi hii ina utajiri mwingi na wa aina mbalimbali  ya huu tunaouita urithi wa utamaduni.

Vivutio vyetu vikubwa ni vitu vya asili – wanyama, mbuga, milima na fukwe ambavyo ni vitu vizuri, lakini wakati mwingine vinawafanya watu wasirudi mara kwa mara na vinawafanya wasikae kwa muda mrefu.

Serikali iliona hilo kwa muda mrefu kupitia wizara na wakaona kuna fursa…huu urithi wa utamaduni una nafasi yake kubwa kweye utalii. Tunazijua nchi nyingi duniani zina urithi wa utamaduni, na siyo mwingi na tofauti kama wetu, lakini urithi huo unavutia watalii wengi sana. Nchi kama Misri kwa hapa Afrika pato lake kubwa ni la utalii na hawana wanyama, hawana mbuga lakini wanatumia urithi wa utamaduni – mapiramidi na kadhalika.

Lakini nenda nchi kama Ugiriki, Italia kote huko ni hivyo. Kwa hiyo kuna mkakati na kwa hapa Ngorongoro wana nafasi nzuri kwa sababu wana hivi vitu vya urithi wa utamaduni na huu urithi wa asili. Hivi viwili vinatiana nguvu na tunaamini vikitangazwa vitawafanya watalii wanapokuja ndani ya Ngorongoro kukaa kwa muda mrefu kwa sababu watapenda kuona kreta, watapenda waone wanyama, watapenda waone Laitoli [mahali kuliko na nyayo za binadamu wa kale na masalia yao] na maeneo mengine yatakayowafanya wakae siku mbili au tatu za ziada. Kadiri mtalii anavyokaa nchini ndivyo anavyotumia pesa nyingi.

Hii Ngorongoro kama wataalamu wote wanavyosema ndiyo chimbuko la binadamu. Ukiangalia mazingira miaka hiyo milioni 2 kulikuwa na ziwa pale (Olduvai) na maji yalikuwa yakitiririka kutoka hapa (uwanja wa juu) kwenda ziwani. Ndiyo maana hawa watu waliishi kule. Maisha yao yalikuwa mazuri. Wanyama walikuwa wengi. Tunaona wanyama sasa hivi lakini wapo hao wa miaka milioni 2 mpaka milioni 1.5. Kwa hiyo ni eneo pekee Tanzania ambalo utaliona lina historia ndefu ya mwanadamu kuishi eneo hili, lakini pia kuishi na wanyama na mazingira yao yakibadilika.

The fisrt diaspora [wahamiaji] imetokea miaka kama milioni 1.7 ndiyo hapo hawa binadamu wa kale walipohama wakaenda huko Ulaya na Asia. Haikuishia hapo – ikatoea diaspora ya pili miaka kama laki 2 binadamu kama sisi [homosapian] tuna akili zetu hao wakaanza kuhama kwenda huko Ulaya na Asia. Mabadiliko ya rangi is a recent phenomenal maana tunaongelea miaka milioni 2, miaka milioni 3. Mabadiliko ya gene (jeni) frequency overtime. Mtu asije akakuuliza kama tunabadilika tutakuwaje?

Hakuna anayejua kwa sababu sisi sana sana ukiishi ni miaka 120 na mabadiliko haya mengine yanachukua miaka milioni kwa hiyo huwezi ukasema tutakuwaje lakini mabadiliko hata sasa yanatokea na tunabadilika. Hatujui huko mbele itakuwaje lakini kitu cha muhimu ni mazingira, kwamba kunapobadilika mazingira na hali ya hewa lazima uishi. Ili uishi hiyo hali ya hewa na mazingira vinachagua watu wenye jeni fulani ambao lazima waa- adapt kwenye yale mazingira. Watakaoshindwa ku- adapt watapotea. Unapo-adapt kutakuwa na kitu kinachobadilika – inawezekana hata tabia au utamaduni. Kwa hiyo ni muhimu sana sasa hivi serikali na Wizara ya Maliasili na Utalii inakazia sana kupigia chapuo huu utalii wa urithi wa utamaduni ambao tunao mwingi mno na wa aina tofauti tofauti.

Wizara imejikita sana na imekuwa ikiunga mkono haya mambo kale na urithi huu wa utamaduni ili kiwe kichocheo kingine cha kuwaleta watalii wa nje na watalii wa ndani kujifunza. Ndiyo maana tunaadhimisha miaka 60 ya Zinj ili wananchi wamjue huyu Zinjathropus na masalia mengine ambayo yamekuwako humu humu Olduvai.

Olduvai hii ina historia ya binadamu tangu miaka milioni 3.6 kwa mujibu wa nyayo zile za Laitoli. Ina historia kubwa na ndefu – miaka milioni 3.6 hakuna mahali pengine. Masalia ya wanadamu kama sisi yapo mengi tu, na hata michoro ya mwambani watu walianza kuchora miaka kama 40,000. This is the beginning of human imagination – michoro kama ya Kondoa. Walitengeneza rangi, na zile rangi zimedumu. Mahali pengine tunadhani ni kama miaka 60,000 iliyopita lakini rangi zile zimedumu mpaka leo. Walikuwa wanachora vitu vizuri. Angalia picha za kina mama, miguu yao – warembo, wamevaa sketi. Watu wanasema ‘vikuku’ is African inversion. Watu wamechorwa wamevaa ‘vikuku’ [mapambo ya miguu] miaka 40,000 iliyopita! Na mimi huwa nawaambia hata hii lipstick is an African inversion. Tuna ushahidi unaoonyesha kwamba vipodozi vilianzia Afrika. Rasta zimeanzia huku Afrika.