IMG-20160714-WA0072Jumanne Rashid ambaye mwaka 1960 alikuwa kijana mdogo, alikuwa Gombe, alimsaidia Dk Jane Goodal katika kutoa mizigo kwenye meli na kuandaa kambi kando ya Ziwa Tanganyika kwa ajili ya utafiti, kama ilivyoandikwa katika gazeti hili la JAMHURI wiki iliyopita.

Dk. Jane alirudi katika Chuo Kikuu cha Cambridge mwaka 1962, ambapo alikwenda kusoma shahada ya uzamivu katika Etholijia.

Alianza kufanya utafiti kuhusu jamii ya sokwe walioshi Kasekela, ndani ya hifadhi ya Gombe, hapo alikutana na sokwe na kuwapatia majina ya Fifi na David Greybeard ambao alikuwa akiwafuatilia kuhusu tabia zao. Hii ni sehemu ya pili ya simulizi kutokana na mahojiano maalum yaliyofanywa na JAMHURI.

Dk. Jane anaelezea namna alivyoanza kuwazoesha sokwe  kurahisisha kazi yake ya utafiti. Anasema alianza kuwazoesha sokwe kwa kutumia matunda, hasa ndizi. Anasema sokwe mtu wanapenda sana ndizi, hivyo katika kuhakikisha anafanikiwa alihitaji kuwatafutia chakula wanachopenda.

“Nilianza kuwazoesha sokwe mtu kwa kutumia ndizi, hiyo ilikuwa ni hatua muhimu sana katika utafiti wangu. Haikuwa kazi rahisi kuwazoesha maana sokwe mtu kwa asili wanakuwa na haya, hivyo ilinichukua muda mrefu kidogo,” anasema Dk Jane.

Anasisitiza kwamba kitendo cha kuwazoesha sokwe mtu,  kimeweza kurahisisha sasa wanaweza kusogelewa na watalii na kuwatazama kwa umbali wa mita tano mpaka kumi. Anasema kitendo hicho kimechukua muda mrefu kidogo.

Anasema katika kuwazoesha sokwe mtu, huchaguliwa familia moja ambayo hupewa majina na kuwafuatilia makazi yao, tangu wanapoamka asubuhi na pindi wanapokwenda kulala, jioni. Sokwe mtu wanaandaa sehemu ya malazi kama ilivyo kwa binadamu.

Dk. Jane anasema sokwe mtu, hulala na kuamka mapema, huku wakiitana na kuthibitisha kama wote ni wazima. Baada ya kukamilisha zoezi hilo, huanza maisha yao ya kawaida kwa kwenda kutafuta chakula pamoja na shughuli nyingine.

Alipoulizwa kama angeanza kufanya kazi ya kuwazoesha sokwe mtu leo angetumia mbinu zilezile za kuwapatia ndizi, Dk. Jane anasema asingeweza kufanya hivyo tena, maana wanyama hao kwa asili hujitafutia chakula wenyewe na anahisi alifanya makosa kwa aina ya ushawishi aliyoitumia kwa sokwe mtu.

“Kama ningeanza leo kufanya hii kazi ambayo sasa nimekuwa nikiifanya kwa zaidi ya miaka 50, nisingefanya kama nilivyofanya kipindi kile wakati ninaanza. Leo ningewazoesha sokwe mtu kwa mazingira yao ya kawaida kabisa,” anasema Dk. Jane.

Mtafiti huyo anasema katika miongo zaidi ya mitano ya utafiti wa sokwe mtu, amejifunza namna ya kuwasiliana nao kwa karibu hasa kupitia sauti maalum. Anasema amekuwa akiwaita sokwe mtu pindi anapowahitaji na wamekuwa wakimuitikia.

“Nimekuwa nikiwaita sokwe mtu pindi ninapowahitaji, wamekuwa wanakuja na kunikumbatia vizuri kabisa. Ninawapenda sana, nao wamekuwa wakionesha upendo mkubwa sana kwangu,” anasimulia Dk. Jane.

Wakati akiendelea na mahojiano maalum anaanza kuwaita sokwe mtu kwa sauti ya kuwaelezea kwamba yuko maeneo jirani, katika muda mfupi walimuitikia, na Dk. Jane anasema walikuwa wakimueleza sehemu walipo.

Hakika ilikuwa inavutia kuona anaweza kuwasiliana na sokwe mtu, na wao baada ya muda mfupi wanaonesha kuielewa lugha iliyotumiwa na Dk. Jane. Anasema katika sokwe mtu ambao amekuwa akiwatafiti, daima David atabaki katika kumbukumbu zake, maana alitokea kuwa rafiki yake mkubwa.

Dk. Jane anasema aliweza kuutumia ushawishi wa sokwe mtu David, ili kuweza kuingia kwenye makundi ya sokwe mtu wengine. Anasema David alikuwa ni kiongozi mzuri na ndiye alikuwa akileta makundi mengine kwake, na ikawezesha kuwazoesha kwa urahisi.

“Nakumbuka sokwe mtu David, akiwa rafiki yangu sana, alipokuwa akiniona alikuja mbio na kunilaki…alikuwa anafanya kama wafanyavyo binadamu, alikuwa ananikumbatia nami ninampapasa kichwani kuonesha kwamba ninamheshimu sana huku yeye akinipigapiga mgongongoni,” anasema Dk. Jane.

By Jamhuri