IMG-20160714-WA0072Umewahi kuwaza kuhusu binti wa miaka 26, kutoka katika nchi na bara lake na kwenda bara jingine katika kile kinachoitwa kutimiza ndoto zake? Ukikutana na Dk. Jane Goodall na kumuuliza swali hilo, jibu lake ni rahisi sana, ndiyo.

Ni siku ya Jumatatu saa 6:30 mchana. Napanda boti kutoka Kibirizi, Kigoma kwenda Hifadhi ya Taifa ya Gombe, ampako nilikuwa na miadi na mtafiti bingwa wa sokwe mtu, Dk. Jane Goodall. Nimepata kusoma mambo mengi kuhusu bibi huyo mwenye umri wa miaka 82 sasa.

Shauku ya kukutana naye ilizidi kuongezeka kila boti ilipokuwa ikipasua mawimbi kwenye Ziwa Tanganyika, ziwa lenye kina kirefu zaidi barani Afrika. Safari yangu inachukua mwendo wa saa mbili hivi mpaka ninafika katika Hifadhi ya Taifa ya Gombe.

Pale ninapokewa na wenyeji wangu, Mhifadhi Mkuu wa Gombe, Noelia Myonga, pamoja na Mhifadhi Msaidizi, Dominick Tarimo. Haraka maandalizi ya mahojiano maalumu yanafanyika. Kwa mara ya kwanza katika miaka yangu zaidi ya 10 katika tasnia ya habari, ninafanya mahojiano katikati ya hifadhi, huku milio ya wanyama na ndege ikirindima.

Maandalizi yanakamilika na msaidizi wa Dk. Jane Goodall, aitwaye Susana Name, anamleta mtafiti bingwa wa sokwe. Katika umri wake wa miaka 82, Dk. Jane haoneshi kuchoka, anapandisha kilima mwenyewe mpaka kufika sehemu iliyoandaliwa kwa ajili ya mahojiano.

Punde baada ya kufika, anakutana na baadhi ya waandishi, lakini pilikapilika za maandalizi zinawafanya hata baadhi ya wageni waliotoka ng’ambo kuja kutembelea Hifadhi ya Gombe, kuvutiwa na kuanza kudodosa kulikoni, mbona kuna maandalizi yasiyokuwa ya kawaida. Bila shaka wanaambiwa kwamba Dk. Jane Goodall yupo Gombe na anakutana na wanahabari punde.

Baada ya kufika sehemu iliyoandaliwa kwa ajili ya mazungumzo, Dk. Jane anaanza kwa utani, “mbona kuna kamera nyingi, leo kuna nini Gombe? Sijawahi kukutana na wanahabari nikiwa porini kama leo.” Maneno hayo nimeyatohoa kutoka kwenye lugha ya Kiingereza ambayo ndiyo aliyoitumia wakati wote wa mahojiano.

Baada ya kusalimiana na wanahabari, dada mmoja kutoka Columbia, Sandra Vinazco, aliyekuwa ameambatana na mumewe, anamkimbilia na kumkumbatia huku akilia kwa furaha, hali ambayo ilimfanya kila mmoja wetu pale kupigwa na butwaa. Anabembelezwa na Dk. Jane kwa muda kidogo na baadaye anatulia.

Dk. Jane anaanza kwa kuzungumzia safari pamoja na ndoto yake mpaka hapo alipo leo. Anakumbuka magumu aliyoyapitia katika familia yake. Anasema alikuwa anapenda wanyama tangu akiwa mtoto mdogo. Anakumbuka kwao hapakuwa na televisheni kwa hiyo wanyama alikuwa akiwasoma kwenye vitabu tu.

“Nilikuja Tanganyika Julai 1960, nikiwa na umri wa miaka 26. Nilisafiri kutoka Uingereza mpaka hapa, eneo ambalo leo linajulikana kama nyumbani kwa sokwe mtu. Nilikuja hapa nikiwa na sehemu ya kuandikia kumbukumbu pamoja na darubini,” anasema Dk. Jane.

Anasema kutokana na jinsi alivyokuwa anapenda wanyama, alitokea kuvutiwa na sokwe mtu. Tangu kipindi hicho maisha yake yakajikita kwenye utafiti wa sokwe mtu, ambao kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na taasisi yake, wanyama hao wanafanana kwa asilimia kubwa na binadamu. Wanafanana kuanzi mfumo wa upumuaji, damu mpaka hata ubongo.

 “Nilifika hapa Tanganyika (Tanzania) baada ya kuelekezwa na rafiki zangu waliokuwa Kenya. Nilielekezwa kwa Dk. Louis Leakey ambaye alikuwa akifanya tafiti zake huku… baada ya kukutana naye nilionesha kwamba ninapenda sana wanyama, alinikubalia na nilianza,” anasema Dk. Jane.

Anaongeza, “Nilikuwa na ndoto ya kuja Afrika, lakini nilikuwa nachekwa sana na rafiki zangu ambao walikuwa wanajua hali ya uchumi wa nyumbani. Sikuwa na fedha na nilikuwa naambiwa Afrika ni mbali sana…nilikaribishwa na Dk. Louis Leakey ambaye alikuwa anafanya utafiti.”

Anasema katika utafiti wake wa sokwe, anamkumbuka sokwe mtu, aliyekuwa amempa jina la David. Anasema sokwe mtu huyo ndiye aliyekuwa rafiki yake, baada ya kuanza kumfuatilia na ndiyo akasababisha Dk. Jane kuanza majaribio ya kuwazoesha sokwe mtu kuwasogelea binadamu.

“Sokwe mtu wanazo namna mbalimbali za kuwasiliana…sokwe hao hao pia wanatengeneza zana ambazo zinawasaidia kumudu mazingira wanayokutana nayo. Sokwe mtu kwa kiwango kikubwa anafanana na binadamu, lakini wana nguvu zaidi ya binadamu,” anasema Dk. Jane.

Dk. Jane anasema maisha ya sokwe mtu yanafanana kwa kiwango kikubwa na yale ya binadamu, ingawa yeye anabeba mimba kwa miezi minane na wiki mbili tu. Akizaa hulea mtoto kwa miaka minne mpaka mitano. Katika kipindi hicho sokwe jike, hawezi kuzaa mpaka atakapomwachisha kunyonya mtoto wake.

Anasema sokwe mtu akiwa na mimba anapenda kulala na hatembei umbali mrefu. Akifikia kipindi cha kujifungua hutoweka. Mtoto akifikisha siku tatu ndiyo huanza kujichanganya na sokwe wengine. Ananyonyesha kwa kipindi cha miezi sita bila kumpatia mtoto chakula cha aina yoyote.

Sokwe huzaa mapacha, ila ni aghalabu kutokea. Gombe tunao mapacha  -Greter na Golden – mama yao anaitwa Gremlin. Kwa sasa sokwe hao mapacha wana miaka 23. Sokwe mwenye jina la Fifi alipata kuzaa mapacha, japokuwa walishakufa, walikufa wakiwa na zaidi ya miaka 16.

Sokwe huyo alikuwa anabeba mtoto mmoja mgongoni na mwingine tumboni, na wakati mwingine huwabeba wote mgongoni.

Watoto mapacha wa sokwe wanashirikiana, kukitokea ugomvi wanasaidiana. Mara nyingi hupenda kutembea pamoja. Hata ikifikia kipindi cha wao kuanza kuzaa urafiki huendelea na wanatambuana kama wanafamilia.

Kwa nini sokwe wanapewa majina? Dk. Jane anasema kuwapa majina sokwe mtu kulilenga kuendelea kuwachunguza tabia zao katika tafiti zake. Anasema yeye kama mtafiti imekuwa rahisi zaidi hata kuwafananisha tabia kutoka kizazi kimoja cha sokwe mtu kwenda kingine.

Ukienda katika Hifadhi ya Taifa ya Gombe, majina kama Glitter pamoja na Golden siyo mageni. Hao ni sokwe mtu pacha ambao wote pia wana watoto. Dk. Jane anasema sokwe mtu hawafanani, wako kama ambavyo binadamu tunatofautiana kwa sura, tabia na hata matendo.

“Sokwe hawafanani sura. Wana tofauti kubwa tu usoni. Unaweza kukuta sokwe mtu mmoja ni mweusi zaidi, wakati mwingine ngozi yake ni angavu, mwingine anakuwa na manyoya ya tofauti. Pia hutofautishwa kwa tabia. Utakuta huyu anapenda kucheza sana wakati mwingine hapendi. Wengine wanakuwa wachoyo na wengine siyo wachoyo,” anasema Dk. Jane.

Kuhusu utawala wa sokwe mtu, Dk. Jane anasema wanao muundo wa utawala wao. Utawala huenda kwa sokwe mtu mwenye nguvu zaidi pamoja na busara, kuwaongoza wenzake. Madume wanapigana mpaka mmoja anayeshinda ndiye anayekuwa kiongozi na hatimaye kutengeneza himaya.

Anasema katika utawala wake anakuwa na sokwe wengine ambao ikitokea uvamizi wa sokwe mwingine wanamsaidia kupigana na sokwe wengine.

Dk. Jane anasema Serikali inapata mapato kutoka katika sekta ya utalii, kwa hiyo Serikali inapaswa kuwekeza katika suala la ikolojia. Inatakiwa pia kuangalia suala la miundombinu na kukifikiria kizazi kijacho, mazingira yasiharibiwe.

Akielezea kuhusu changamoto anazokutana nazo katika kuwatafiti sokwe mtu, Dk. Jane anasema mwanzo kulikuwa na msitu mnene unaounganisha Ziwa Tanganyika na sehemu za Rwanda na Uganda, lakini kwa sasa uhabifu mkubwa umefanyika na kwamba uharibifu huo umewafanya sokwe wengi kuondoka katika maeneo yao ya asili na kwenda nje ya hifadhi.

Anasema Tanzania inatakiwa kujivunia matunda makubwa ya tafiti ambazo zimekuwa zikifanywa, kwani imekuwa nchi ya kwanza kuanzisha utafiti wa sokwe mtu duniani, na tafiti hizo zimekuwa zikiendelea kufanyika.

Dk. Jane Goodall anasifia jitihada za Rais Magufuli za kupambana na rushwa. Anasema mapambano hayo dhidi ya rushwa yatakuwa na maana kubwa kwa Shirika la Hifadhi za Taifa na hifadhi zote nchini, maana fedha za kuwezesha uhifadhi zitapatikana.

Anayo matumaini kwamba jitihada zinazofanywa na Rais Magufuli zimelenga katika kuondosha matumizi mabaya ya ofisi za umma, na kitendo hicho kitaongeza ufanisi katika uhifadhi na hivyo kuongeza idadi ya watalii na pato la nchi litokanalo na sekta hiyo.

Enzi hizo, Dk. Louis Leakey, ambaye alikuwa nchini Kenya, akiendelea na tafiti zake, Dk. Jane alimpigia simu na kumwomba wakutane kujadiliana kuhusu wanyama. Dk. Leakey aliamini kwamba tafiti za kuishi kwa binadamu wa kale, alizokuwa anafanya zingeweza kuhusishwa na kuishi kwa sokwe mtu, hivyo naye alihitaji kumpata mtafiti kama Dk. Jane.

Dk. Leakey aliamua kubadili mawazo na kuamua kumfanya Dk. Jane kuwa katibu wake. Alimtuma katika Bonde la Olduvai ambako tayari alikuwa akiendelea vyema na mikakati yake ya utafiti. Mwaka 1958, Leakey alimtuma Dk. Jane, London.

Mtafiti huyo wa binadamu wa kale alitafuta fedha na Julai 4, 1960 alimtuma Dk. Jane katika Hifadhi ya Taifa ya Gombe kufanya utafiti. Dk. Jane alipokewa na Jumanne Rashid, mkazi wa Kigoma. Anakumbuka kwamba alimpokea mtafiti huyo wa sokwe mtu akiwa ameambatana na mama yake.

Jumanne Rashid, ambaye kipindi hicho alikuwa kijana mdogo, alikuwa pia Gombe. Alimsaidia Dk. Jane kutoa mizigo kwenye meli na kuandaa kambi kando ya Ziwa Tanganyika kwa ajili ya utafiti. Dk. Jane alirudi katika Chuo Kikuu cha Cambridge mwaka 1962 ambako alikwenda kusoma shahada ya uzamivu katika etholijia.

Alianza kufanya utafiti kuhusu jamii ya sokwe mtu walioshi Kasekela ndani ya Hifadhi ya Gombe. Hapo alikutana na sokwe na kuwapatia majina ya Fifi pamoja na David Greybeard ambao alikuwa akiwafuatilia kuhusu tabia zao.

Kutokana na utafiti wa Dk. Jane ulioanza mwaka 1960, leo Gombe ni hifadhi maarufu kuliko zote duniani kutokana na sifa hii ya kuwapo kwa sokwe mtu.

Mama huyu, amewafahamu sokwe kwa kiwango kikubwa. Amefika hatua anaweza kuwasiliana nao kwa milio na wakaelewana lugha. Usikose JAMHURI wiki ijayo.

1392 Total Views 1 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!