Dk. Shein: Tutaendelea kushirikiana na China

Zanzibar imeihakikishia China kwamba itaendelea kuthamini uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya nchi hizo mbili pamoja na Chama cha Kikomunisti cha China (CPC).

Hayo yamesemwa na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, wakati alipofanya mazungumzo na Naibu Waziri  wa Mambo ya Nje na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CP, Guo Yezhou, Ikulu mjini Zanzibar wiki iliyopita.

Katika mazungumzo hayo, Rais Shein amesema kuwa kwa kiasi kikubwa maendeleo ya Zazibar yanajengwa pia kupitia ushirikiano na Jamhuri ya Watu wa China, kupitia CPC.

Amesema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China imeifanyia mambo mengi Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo Zanzibar kwa kuunga mkono uimarishaji wa sekta za maendeleo.

Akitoa ushuhuda wa jinsi ya Jamhuri ya Watu wa China ilivyoisaidia Zanzibar katika kuimarisha sekta za maendeleo ikiwemo afya, elimu, viwanda, kilimo, sekta ya habari, miundombinu, michezo na mengineyo, Dk. Shein amesema kuwa nchi hiyo ni rafiki wa kweli, kwani imeanza ushirikiano mara tu baada ya Mapinduzi ya Zamzibar  Januari 12, 1964.

Ameongeza kuwa mbali ya Serikali ya China kusaidia sekta hizo, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Kiwanda cha Sukari Mahonda, Kiwanda cha Sigara Maruhubi na viwanda vingine, pia nchi hiyo imesaidia kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya elimu kwa kutoa nafasi nyingi za masomo nchini mwake.

Ameeleza kuwa kubwa kuliko yote, ni ukarabati mkubwa wa Hospitali ya Abdalla Mzee mkoani Pemba, ukarabati wa Uwanja wa Michezo wa Mao Zedong pamoja na ujenzi wa Terminal III katika Uwanja wa Ndege wa Zanzibar. 

Aidha, Dk. Shein amemueleza kiongozi huyo haja ya kukuza ushirikiano uliopo kati ya  Chama Cha Mapinduzi (CCM) na CPP pamoja na serikali zote mbili kama ulivyofanywa na waasisi wake, hayati Mwalimu Julius Nyerere na Mwenyekiti Mao Zedong.

Ameeleza kuwa ushirikiano huo ulianza tangu mwanzo wa vyama vya ASP, TANU na hatimaye kuja kwa CCM na kueleza urafiki mzuri ulioonyeshwa na viongozi wa pande mbili hizo kwa kutembeleana ambao umekuwa ukiendelezwa hadi hivi leo.

Sambamba na hayo, Dk. Shein ametumia fursa hiyo kutoa shukrani zake kwa Serikali ya China kupitia CPC kwa kusaidia ujenzi wa Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Julius Nyerere kinachojengwa Wilaya ya Kibaha, mkoni Pwani.

Kwa upande wake, Yezhou, alitoa shukrani kwa mapokezi mazuri aliyoyapata yeye na ujumbe wake tangu walipowasili nchini.

Naibu waziri huyo alimweleza Rais Shein kuwa chuo hicho ni kwa ajili ya kutoa mafunzo ya uongozi kwa nchi sita zenye vyama vya ukombozi vilivyoshirikiana na CPC ambavyo ni CCM (Tanzania), ANC (Afrika Kusini), ZANU-PF (Zimbabwe), FRELIMO (Msumbiji), MPLA (Angola) na SWAPO (Namibia).

Kiongozi huyo alimweleza Dk. Shein kuwa ili kuunga mkono juhudi ziizochukuliwa na Tanzania, Rais Xi Jinping alitoa tuzo kwa Waziri Mkuu mstaafu, Dk. Salim Ahmed Salim, hivi karibuni ikiwa ni kutambua mchango wake mkubwa katika kuiwezesha China kuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa (UN).

Pia alimhakikishia Dk. Shein kuwa China itaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha miradi mbalimbali ya maendeleo na kupongeza miradi ambayo tayari imeshakamilika huku akisisitiza kuwa bado nchi hiyo itaendeleza hatua zake za kuisaidia Zanzibar ikiwemo kuleta wataalamu, wakiwemo madaktari kutoka Jimbo la Jingsu.

888 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!
Show Buttons
Hide Buttons