*Apendekeza rais anapotuhumiwa apelekwe mahakamani

*Asitumie walinzi, magari ya Serikali wakati wa kampeni

*Kuwepo serikali 3 ikiwamo ya Tanganyika , Bunge, SenetiAliyekuwa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk. James Wanyancha (pichani), ametoa mapendekezo yake ya Katiba na kutaka rais aondolewe kinga kushitakiwa mahakamani.

Dk. Wanyancha aliyepata kuwa Mbunge wa Serengeti (mwaka 2005 – 2010), anapendekeza Katiba ijayo imzuie rais kutumia walinzi na magari ya Serikali wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu.


Anataka Katiba mpya iruhusu pia uundaji wa Serikali ya Tanganyika , jopo la maseneta na wazawa kumiliki asilimia 51 ya uwekezaji mkubwa kwenye maliasili za nchi.

 

Dk. Wanyancha ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Barabara nchini, ametoa maoni hayo ya Katiba mpya katika mahojiano maalumu na JAMHURI jijini Dar es Salaam , wiki iliyopita.


Anasema mapendekezo hayo yakizingatiwa na kupewa nafasi katika Katiba ijayo yatachangia kuimarisha uchumi na uwajibikaji wa viongozi kwa manufaa ya wananchi na Taifa.

Rais ashitakiwe

“Katiba mpya itamke wazi kwamba viongozi wa umma, akiwamo rais, akituhumiwa kufanya kosa lolote apelekwe mahakamani sheria ifuate mkondo wake,” anasema Dk. Wanyancha na kuongeza:


“Kwanini tunaogopa kumshitaki rais? Mbona Ghana rais anashitakiwa? Na sisi Katiba iruhuru Rais ashitakiwe mahakamani mara anapotuhumiwa kufanya kosa.”

 

Changamoto ya kumwondolea rais kinga ya kushitakiwa inatajwa na wadau mbalimbali kuwa ni miongoni mwa vichocheo vya kumuimarisha kiongozi wa nchi katika misingi ya uadilifu na maadili ya utumishi wa umma.

Rais apunguziwe madaraka

“Wanaosema rais asipunguziwe madaraka wananishangaza sana. Katiba iliyopo iliundwa chini ya mfumo wa chama kimoja cha siasa.


“Katiba iliyopo haikidhi mahitaji ya mfumo wa vyama vingi, ndiyo maana vyama vya upinzani vinasuasua, ilitakiwa kubadilishwa mara baada ya mfumo wa vyama vingi kurejeshwa mwaka 1992,” anasema Dk. Wanyancha.


Anasema Katiba iliyopo inampatia rais madaraka makubwa ambayo sasa hayana budi kupunguzwa kukidhi mfumo wa vyama vingi vya siasa na demokrasia ya kweli.


Anapendekeza Katiba mpya imwondolee rais mamlaka ya kuteua viongozi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), wakuu wa vyuo vikuu, msajili wa vyama vya siasa na majaji, badala yake nafasi hizo zitangazwe kuwapata viongozi wenye sifa.


“Ni vigumu NEC iliyoteuliwa na rais kumdhibiti rais wakati anapoomba kurejeshwa Ikulu. Hakuna haja ya rais kuwateua majaji, wakuu wa vyuo vikuu, majaji na msajili wa vyama vya siasa, hao ni professionals (wataalamu), nafasi zitangazwe watu wenye sifa wajitokeze kuomba ajira,” anasisitiza.


Anaongeza, “Hatuna shida kwa nafasi ya mawaziri. Rais aendelee kuteua mawaziri, lakini sasa wasiwe wabunge. Mawaziri lazima wawe wataalamu wanaoendana na wizara husika, Marekani wanafanya hivyo.


“Mtu akishakuwa mbunge haina haja ya kumteua kuwa waziri, mkuu wa mkoa wala mkuu wa wilaya. Hawa wengine inapaswa wachaguliwe na wananchi wa mikoa na wilaya husika.

“Tena inatakiwa sasa idadi ya mawaziri wa Tanzania ipunguzwe hadi 14, kwani mawaziri wakiwa wengi wanageuka kuwa watendaji na kuwavuruga wataalamu.”


Kitendo cha mawaziri kufukuzwa baada ya wizara zao kuboronga kinamkera Dk. Wanyancha kiasi cha kupendekeza utaratibu huo usiruhusiwe kwenye Katiba mpya.


“Mawaziri wasifukuzwe kazi kwa sababu ya wizara zao kuboronga, waziri haandiki hundi, wanaostahili kuwajibishwa ni wataalamu wa wizara husika. Nimekuwa naibu waziri, sikupata kuandika hundi wala kushughulikia zabuni za wizara,” anasema.

Rais asitumie walinzi, magari ya Serikali

Dk. Wanyancha anakosoa utaratibu wa rais kuendelea kulindwa na walinzi walioajiriwa na Serikali na kutumia magari ya Serikali wakati wa kampeni za kuomba kurejeshwa madarakani. Anapendekeza utaratibu huo uzuiwe katika Katiba ijayo.


“Mawaziri na wabunge wanazuiwa kutumia magari ya Serikali wakati wa kampeni, maoni yangu ni kwamba hata rais asiruhusiwe kutumia walinzi, ndege na magari ya Serikali, huduma hizo zitolewe na vyama husika kwenye kampeni.


“Lakini pia Katiba mpya izuie rais, mawaziri na wabunge kupokewa na wakuu wa mikoa na wilaya wakati wa kampeni kwani wakati mwingine kitendo hicho hushawishi wananchi kuwachagua na kupuuza wagombea wa vyama vya upinzani,” anapendekeza.


Dk. Wanyancha anaongeza kuwa Katiba mpya iwe na kipengele kinachowataka wagombea urais, ubunge na udiwani kufanya midahalo ya wazi ili wapigakura waweze kuwachuja.

 

Wagombea wasitoe ahadi

Utaratibu wa wagombea kutoa ahadi mbalimbali wakati wa kampeni za uchaguzi nao unaonekana kukosa mantiki kwa Dk. Wanyancha, hivyo anapendekeza Katiba mpya isiuruhusu.

 

“Wagombea wasiruhusiwe kutoa ahadi wakati wa kampeni… kitendo cha kuwaahidi wananchi kuwa utawajengea uwaja wa ndege, barabara, miradi ya maji na mingineyo ni sawa na hongo.


“Siwezi kuwa mjinga kusikia mgombea anatuahidi kwamba atatujengea uwanja wa ndege wa kimataifa na barabara ya lami Mugumu (wilayani Serengeti) halafu niache kumchagua,” anasema.

 

Kwa mujibu wa Dk. Wanyancha, Serikali iachiwe jukumu la kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo kulingana na uwezo wa kifedha na mahitaji ya wananchi.

Serikali ya Tanganyika

Kama inavyopendekezwa na baadhi ya wananchi, Dk. Wanyancha naye anapenda kuona Katiba ijayo inaruhusu kuwapo kwa Serikali tatu -ya Tanganyika , ya Zanzibar na ya Muungano wa Tanzania.


“Tuliingia Muungano wa nchi mbili ( Tanganyika na Zanzibar ) ikaundwa nchi moja ( Tanzania ). Lakini Zanzibar imerudi kuwa nchi kamili, ina rais wake, Katiba yake na Bunge lake (Baraza la Wawakilishi). Nchi ikishakuwa na vitu hivyo hiyo ni nchi kamili.


“Cha kushangaza tena Wazanzibar wanashirikishwa kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , kutoa maoni ya Katiba ya Muungano na kuruhusiwa kumiliki ardhi Tanzania Bara, lakini Watanganyika hawashirikishwi kwenye Katiba na Bunge la Zanzibar wala kumiliki ardhi Zanzibar ,” anasema Dk. Wanyancha na kuendelea:


“ Zanzibar ilishavunja Muungano, na kama itaachwa iendelee kuwa hivyo, basi Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iruhusu uundaji wa Serikali ya Tanganyika , vinginevyo huu Muungano utakuwa ni udanganyifu tu.”

Kuwepo Seneti ya Tanzania

“Nchi inapaswa kuwa na Seneti itakayokuwa na jukumu la kuchunguza na kutoa uamuzi wa mwisho juu ya masuala yaliyopitishwa na Bunge kuhakikisha yanajali masilahi ya wananchi na Taifa kwa ujumla. Seneti itazuia mambo yanayopitishwa kisiasa zaidi badala ya kuzingatia masilahi ya umma na Taifa,” anasema.

Watuhumiwa wa ufisadi wasimamishwe

Viongozi wanaotuhumiwa kwa ufisadi, kwa mujibu wa Dk. Wanyancha, wanastahili kusimamishwa kupisha uchunguzi kwa tuhuma zinazowakabili.


“Katiba mpya itamke kwamba viongozi wanaotuhumiwa kwa ufisadi, lazima waachie nyadhifa zao kupisha uchunguzi, na kiundwe chombo maalumu cha kuwachunguza na kutoa uamuzi haraka, jirani zetu Wakenya wanafanya hivyo,” anasisitiza.

Wazawa wamiliki maliasili asilimia 51

Kuhusu uwekezaji wa kigeni katika maliasili za nchi kama vile madini, Dk. Wanyancha anataka Katiba ijayo itamke wazi kwamba lazima wazawa waingie ubia kwa kumiliki asilimia 51 ya uwekezaji huo na wageni wamiliki asilimia 49.

 

“Wazawa wawezeshwe katika umiliki wa asilimia 51 kwenye miradi mikubwa ya uwekezaji kwenye maliasili za nchi, wageni wasiruhusiwe kuwekeza kwa asilimia 100 nchini.


Mgeni atakayekaidi hilo afukuzwe, huyo ni mnyonyaji. Bila kufanya hivyo Watanzania hatutaendelea,” anahitimisha.

By Jamhuri