Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli

 

Suala la Dar es Salaam ni “very complex” na mimi nataka niwe muwazi na nataka nizungumze kwa ukweli. Ujenzi wa barabara za Dar es Salaam zina matatizo sana .

 

Unaweza ukatengeneza barabara, ukatengeneza “service road”. Service road humo humo ndimo watu wanafanya biashara.

 

“Service road” humo humo ndiyo magereji. Lakini viongozi wapo wanaohusika na maeneo hayo. Nakubaliana na Freeman Mbowe kwamba ni vizuri service road zikaachwa. Mimi nakubaliana naye kwamba watu wasifanye biashara kwenye service road.

 

Kwenye masuala ya barabara tuache siasa. Sheria zimepitishwa hapa ikiwamo sheria namba 13 ya mwaka 2007 na sheria hii ya road reserve (hifadhi ya barabara) imeanza tangu mwaka 1932.

 

Sasa ni vizuri tufike mahali tusimamie sheria. Kwa sababu huwezi ukajenga barabara wakati watu wengine wako kwenye barabara. Ni lazima tufike mahali tuamue hata kama ni kwa machungu.

 

Nilisema siku moja jengo la TANESCO liko kwenye road reserve- si uongo, liko kwenye road reserve hata kama nilisibomoe mimi, siku moja litabomolewa tu unless (labda) tubadilishe sheria.

 

Hata kama ni jengo la serikali. Ukweli unabaki pale pale, “unless” tufike siku moja tubadilishe sheria zetu kwamba kwa barabara za Dar es Salaam upana wake sasa utakuwa ni upana wa kupita bajaji.

 

Lakini kama hii sheria ipo iliyopitishwa na Bunge, itabaki ni vile vile. Tunapozungumzia kutengeneza barabara hakuna sababu tena ya mtu mwingine anakwenda kupachika mabango barabarani.

 

Wenzetu Kenya waliamua kabisa kuwa na wizara inayoshughulikia Nairobi peke yake- wameweza kutengeneza “flyover” moja ya kutoka Thika mpaka Nairobi barabara nane kwenda juu.

 

Inawezekana katika siku zinazokuja ni vizuri basi labda barabara zote za Dar es Salaam tukichukua mfano labda zisimamiwe tu na TANROAD. Hayo ni mawazo yangu.

 

Ili kusudi tunapoamua kuchukua hatua iwe ni hatua ya mwisho pasitokee mtu mwingine wa kuingilia huku. Ili kusudi mtu akishindwa kutengeneza barabara apatikane mtu wa kulaumiwa mmoja.

 

Sasa hizi ndizo challenge (changamoto) tunazozipata kwa Dar es Salaam .

 

Kwa sasa hivi tunataka kujenga Dar es Salaam Express Road ya kutoka Dar es Salaam kuja Chalinze kilomita 100 na kutoka Chalinze kuja mpaka Morogoro njia sita. Wawekezaji wameshajitokeza wengi kwa kujenga kwa PPP.

 

Matatizo tunayoyapata, watu wamejenga kwenye “road reserve” na wapo hata wana siasa wengine wanasema wafanyie biashara humo humo, watafanyia wapi?

 

Hao hao ndiyo wamepitisha hiyo sheria. Wengine wako hapo- message sent and delivered.

 

Nasema kwa uwazi sasa ifike mahali kama tunataka kupunguza msongamano wa Jiji la Dar es Salaam ambako kwa magari yaliyosajiliwa yako zaidi ya milioni moja, ni lazima tuanze kuchukua hatua na vyama vyote tushirikiane kama ushirikiano ulioonyeshwa kwenye Bunge hili la kuunga mkono bajeti hii na ndiyo maana nimesema nawapongeza sana leo wapinzani.

 

Wabarikiwe kabisa na Mwenyezi Mungu kwa sababu wametoa mawazo mazuri tu. Kwa mwendo huu Serikali hii itakwenda vizuri kwa sababu sasa tunapata mawazo mazuri kutoka upinzani.

 

Wanazungumza wametulia very constructive, Msemaji wa Barabara naye amezungumza vizuri mama yule. Tukaona sasa CCM tuna-support tu, tunakwenda vizuri. CCM hoyeee! Na CHADEMA hoyee kwa kuunga mkono hoja hii. CUF hoyee, UDP hoyee, TLP hoyee, NCCR hoyee.

 

Na wengine wote….kwa sababu tunajenga nchi ya umoja kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania. Bahati nzuri barabara hazina siasa.

 

Waziri wa Ujenzi, Dk. John MagufuliWa CHADEMA atapita mle mle na wakati mwingine atafanya maandamano sawa sawa tu vizuri, akaenda na atapita mpaka mwisho. Wa CCM atapita mle mle, wa CUF atapita mle mle… ndiyo uzuri wa barabara. Barabara inatuunganisha wote Watanzania.

 

Ndiyo maana ninasema kwa dhati kabisa michango mikubwa sana iliyotolewa na waheshimiwa wabunge leo naipongeza sana na watalaamu wangu wameichukua na tutaifanyia kazi bila kujali imetolewa na upande gani. Kwa sababu lengo ni kutafuta “solution” ya matatizo yanayoikabili nchi yetu.

 

Maneno haya yalizungumzwa na Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli wiki iliyopita wakati akihitimisha mjadala wa bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha wa 2012/2013

 

 

By Jamhuri