Nahodha na mshambuliaji mahiri wa timu ya taifa ya Ivory Coast (The Elephants), Didier Drogba, amefanikiwa kupata nafasi ya mwisho ya kucheza katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (CAN) 2013, zitakazofanyika nchini Afrika Kusini.

Mbali na Ivory Coast, nchi nyingine zitakazoshiriki fainali hizo zitakazochezwa kati ya Januari 19 na Februari 10, ni mabingwa watetezi Zambia, wenyeji Afrika Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Ethiopia, Morocco, Ghana, Mali, Tunisia, Angola, Niger, Nigeria, Algeria, Burkina Faso, Togo na Cape Verde.


“Wote tunataka kutwaa ubingwa kwa ajili ya nchi yetu na hiyo ndiyo ndoto yetu ya muda mrefu,” anasema mchezaji huyo wa kimataifa wa klabu ya Shanghai Shenhua ya China na kuongeza:


“Umoja wetu na kujituma utatusaidia kutwaa ubingwa. Tulionesha ushirikiano wa hali ya juu dhidi ya Senegal. Sisi ni familia moja, tunapenda kuichezea nchi yetu na kila mmoja anatarajia tutachukua kombe.”


Kama nahodha na mshambuliaji, Drogba anafahamika kutokana na umahiri wake wa kuzifumania nyavu, ujanja alionao anapokuwa uwanjani, mwenye misuli, nguvu na mwanasoka asiyekata tamaa dimbani.


Alipokaribia kuondoka England alikokuwa akiichezea Klabu Bingwa ya Ulaya, Chelsea, mwanasoka huyo alipiganiwa na wachezaji wenzake wa timu hiyo wakitaka abaki.

Hata hivyo, alishikilia msimamo wake wa kutoka nje ya Ulaya kwenda China, akitoa sababu ya kutaka kubadilisha mazingira na kuhamasisha kandanda kwa taifa hilo katika Mashariki ya Mbali.


Akiwa analipwa mshahara wa pauni 250,000 za Uingereza kwa wiki (sawa na Sh milioni 600 za Kitanzania), dhamira ya Drogba ya kutaka kunyakua Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2013, inakolezwa na ukweli kwamba akishindwa hatacheza tena katika fainali hizo.


kwa sababu kwa sasa Drogba ana umri wa miaka 34 ambao kwa kandanda ni uzee, hivyo uwezekano wa kutocheza mwaka 2015 ni mdogo kwani atakuwa na miaka 37. Hata hivyo, uwezekano wa kutimiza ndoto yake ya kutwaa ubingwa mwakani unaweza kupukutika kutokana na ubora wa timu nyingi zilizofuzu kwenda Afrika Kusini.


Mchezo hautabiriki, lakini wenyeji wa michuano hiyo nao wana nafasi kubwa ya kunyakua kombe hilo walilolipata kwa mara ya kwanza mwaka 1996, wakati fainali hizo zilipofanyika nchini humo.


Timu ya Nigeria iliyokuwa ikihangaika kwa miaka mingi kulisaka kombe hilo, pamoja na Morocco, Ghana, Algeria na Tunisia nazo zinapewa nafasi ya kushinda.


Mabingwa watetezi, Zambia, inawekwa kundi la pili ikiunganishwa na timu za Mali, Burkina Faso, Togo, Angola, Niger na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, huku Ethiopia na Cape Verde zikitazamwa kama wasindikizaji.


Wiki tatu zilizopita, Zambia au Chipolopolo ilipata ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Uganda (The Cranes), katika mchezo wa kwanza wa kuamua nani akacheze fainali hizo huko Afrika Kusini, kisha ikafungwa bao 1-0 ziliporudiana kwenye dimba la Namboole jijini Kampala, Uganda.


1060 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!