Hivi karibuni Tume ya Uchaguzi imetangaza na kualika taasisi na asasi mbalimbali wanaotaka kutoa elimu ya uraia kwa wapiga kura waombe kufanya hivyo kwa tume. Ni utaratibu mzuri, tena utasaidia sana wananchi kulielewa suala zima la uchaguzi.

Kwa jinsi hali ilivyo nchini, ni dhahiri kuwa viongozi wa siasa na wapiga kura wote wanahitaji elimu ya uraia kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu baadaye mwaka huu.

Watanzania wanahitaji kuandaliwa vema katika mambo yote yanayohusu uchaguzi. Watu wanapaswa wajue maana ya uchaguzi na umuhimu wake. Watu wanapaswa kujua haki zao kama raia katika uchaguzi.

Tukiongeza na elimu ya mpiga kura, watu wanapaswa kufahamu taratibu za uchaguzi na nini wanapaswa kufanya katika kipindi hicho ch uchaguzi.

Tangu nchi yetu ianze kuchagua viongozi wake mwaka 1958 hadi hivi sasa bado kuna mahitaji makubwa ya elimu ya uraia.

Lakini kuna mambo ya kujiuliza katika suala hili. Je, nani hasa anapaswa kutoa hiyo elimu ya uraia kwa wananchi? Ni vyama vya siasa, serikali au ni asasi za kiraia (NGOs)? Hapa panahitajika kuwa na uwazi.

Jambo la msingi kabisa wananchi wanalohitaji ni kuelimishwa juu ya historia ya uchaguzi duniani na aina za uchaguzi zinazotumika katika nchi na mataifa mbalimbali.

Kutokana na hilo ndipo wananchi na nchi inaweza kujua aina ya uchaguzi ambao unafaa. Na aina hiyo ya uchaguzi ndiyo inapaswa kuwekwa katika katiba na sheria za nchi kama muundo rasmi wa demokrasia.

Wakati wa ukoloni shuleni tulifundishwa kama kasuku kukariri neno ‘democracy’ kuwa  “is a government of the people, for the people and by the people.” (Demokrasia ni serikali ya watu, kwa ajili ya watu, iliyoundwa na watu) na tuliambiwa kuwa neno hilo lilitokana na neno la Kigiriki ‘Demokratia.’ Basi Mwingereza akalikoleza na kulilemba neno lile ‘democracy’ ndipo sisi Waswahili tukalifasiri kama demokrasia, tukiwa na uelewa kuwa ni serikali ya watu wenyewe, imechaguliwa na watu wenyewe na kuwahudumia hao hao watu wenyewe!

Kumbe basi, mfumo huo wa demokrasia umenakiliwa kutoka nchi za Magharibi walikotoka Wazungu waliotutawala tangu pale Bismark wa Ujerumani alipowaita Wazungu wenzake na kugawana Bara la Afrika. Kuanzia siku ile barani Afrika ilijengeka demokrasia za Kiingereza, za Kiijerumani, za Kifaransa, za kireno, za  Kibelgiji na hata za Kiitalia na za Kispania, kulingana na mtawala katika nchi. sambamba na hilo, zikazaliwa nchi katika mataifa kulingana na mtawala aliyekuwepo.

Kwa mapokeo hayo, kila nchi barani Afrika inafuata mtindo wa demokrasia ambao uliwekwa na wakoloni wake. Hata kwa upande wa lugha, hivi sasa barani Afrika kuna makundi makubwa manne ya lugha. Zipo nchi zinazotumia Kiingereza zikijulikana kama anglophone, zipo ambazo zinatumia Kifaransa zikijulikana kama Francophone, zipo zinazotumia Kireno zikijulikana kama “Lusophone” na zipo ambazo zinatumia Kiarabu.

Lugha hizi zikatawala mataifa ya Afrika na lugha za wenyeji zikaitwa ‘vernacular’, maana yake za kienyeji (kwa lugha ya dharau ni lugha za kishenzi).

Kwa mtindo ule, Wazungu walitutawala mpaka kufikia kutufanya tujione si lolote – si chochote. Hapo ndipo tukabobea hata kulowea katika aina ya demokrasia ya wakoloni waliotutawala, tukajawa kasumba.

Sina haja ya kuliendeleza wazo hilo la kutawaliwa na madhara ya ukoloni, mimi nia yangu Watanzania tupewe elimu ya uraia ambayo ni sahihi kwa mazingira ambayo tumo hivi sasa kutuwezesha kushiriki kwa tija kwenye uchaguzi wa mwaka huu.

Kama nilivyobainisha awali, aina ya demokrasia inayoendeshwa nchini hivi sasa ni mapokeo kutoka kwa wakoloni. Kwanza Mjerumani alianza kutufunza demokrasia na kutuwekea maakida, wajumbe na machifu wetu wa asili. Mjerumani aliingia Tanganyika mwaka 1884 mpaka alipong’olewa baada tu ya Vita Kuu ya Kwanza na Mwingereza mwaka 1914.

Kwa taarifa ya wasomaji vijana, Gavana wa kwanza Mjerumani aliitwa Julius Von Soden na Gavana wa mwisho Mjerumani aliitwa Heinrich Schnee (1912-1914).

Utawala wa Mwingereza uliingia mara tu baada ya Vita Kuu ya Kwanza na alitawala kwa miaka 45, kuanzia mwaka 1916 hadi 1961 tulipopata Uhuru. Mtawala (Administrator) Mwingereza wa kwanza aliitwa Sir Horace Byatt (1916) na Gavana wa mwisho Mwingereza ndiye tunayemjua sana aliitwa Sir Richard Turnbull mpaka siku tunapata Uhuru mwaka ule 1961.

Sasa turejee kwenye mada yetu ya uraia kwa maandalizi ya Uchaguzi wetu Mkuu ujao. Kwa vile tumeiga demokrasia ya mapokeo kutoka Ulaya kupitia mkoloni, ni vema basi kujua hawa wenzetu Wazungu walianzaje kutumia huo uchaguzi kule kwao.

Historia inasema wazi, neno hili demokrasia chimbuko lake ni Ugiriki ya kale kabla hata Kristo hajazaliwa. Kwa Wagiriki wale wa kale (Classic Greece) neno lao linaitwa ‘demokratia’, lilitokana na maneno mawili ya Kigiriki. Neno moja ni ‘demos’, maana yake watu na neno la pili ni ‘kratos’ maana yake nguvu.

Hivyo, kwa kuyaunganisha maneno yale mawili lilipatikana neno moja waliloita ‘demokratia’, yaani nguvu ya watu. Hivyo wakasema serikali ya kidemokrasia maana yake ni serikali ya watu wenyewe, iliyoundwa na watu wenyewe kuwahudumia watu wenyewe.

Je, kule Ugiriki kwenyewe walianza kutumia mtindo gani wa uchaguzi wa kidemokrasia? Historia inaonyesha hawa Wagiriki wa zamani walianza uchaguzi wao kwa kupiga kura kwa kunyoosha mikono tu. Baadaye waliendelea kidogo wakaanza uchaguzi wao kwa siri. 

Hapo walibuni mbinu au njia waliyoita ‘Ostracism’, ambayo badala ya kuonyesha mikono kwenye mikutano ya hadhara walitumia vijiwe vya rangi mbili; rangi nyeupe – kukubali na rangi nyeusi – kukataa. Hawakuwa na visanduku wala karatasi za kura.

Watu wa pili ulimwenguni kutumia uchaguzi wa kura walikuwa Warumi wa kale. Inajulikana, Warumi walitawala sana Ulaya (Uingereza, Ujerumani, Ureno, Ufaransa na kadhalika) mpaka kule Mashariki ya Kati – Uyahudi kabla ya kuzaliwa kwake Kristo. 

Historia inaonyesha himaya ya Warumi ilitunga sheria mwaka 139 kabla ya kuzaliwa Kristo, kuonyesha namna ya kupiga kura katika kuwachagua viongozi wao katika himaya yote ya Warumi.

Sheria ile ya Warumi ilitamka wazi kila mpiga kura atumie kipande cha ubao kilichochongwa kama kijiko kwa kumchagua waliyetamka. Hii iliitwa ‘comitia centuriata’, ni namna yao ya kuchaguana. Hawakutumia visanduku vya kura wala vikaratasi.

Sote tuliosoma historia tunajua himaya ya Warumi ilivyoenea Ulaya. Hivyo mapokeo yao yakawa Ulaya kote. 

Kwa muda wa miaka nenda rudi, kila nchi ilitafuta namna au mtindo wake wa kuchaguana. Kwa mfano Kanisa Katoliki kule Roma mwaka 1562 lilianza kutumia uchaguzi wa kura kumchagua Papa kwa kura za siri za karatasi.

Kadiri miaka ilivyopita kukawa na namna mbalimbali za maboresho katika uchaguzi wa mataifa ya ulimwengu huu na taasisi mbalimbali. Marekani wao rais wao anachaguliwa kwa mfumo tunaoita ‘indirect election’, yaani hapigiwi kura moja kwa moja na wananchi wote. Rais wa Marekani huchaguliwa na jopo la wajumbe wa majimbo ‘electoral college’ ambao huwawakilisha wananchi wengine, wakati katika nchi nyingi watu huchagua rais moja kwa moja. Njia hii ndiyo sisi Watanzania tumeifuata.

Sina nia ya kuandika mifumo au aina za uchaguzi, la hasha! Ninachokielezea hapa ni kuwa Tanzania tulipokea mtindo wa uchaguzi kutoka kwa Waingereza. Na wao walipokea kutoka kwa Warumi. Hivyo basi, elimu ya uraia inayohitajika ni ya kutuwezesha wananchi kuona na kuelewa aina ya demokrasia asilia kwa mazingira yetu.

Wanasiasa wengi wanapenda kufuata aina ya demokrasia ya ‘kujimwambafai’ wenyewe na si ile ya asili ya Kibantu chetu. Ninayasema haya kwa sababu tunaona namna demokrasia inavyoendeshwa katika vyama vyetu vya siasa. Kila chama kina katiba yake inayoendesha uchaguzi ndani ya chama.

Mbenna ni Brigedia Jenerali mstaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

965 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!