Kwa mujibu wa Katiba ya nchi, Sura ile ya 2, Kifungu Na. 40 (2) kinasema wazi: “Hakuna mtu atakayechaguliwa zaidi ya mara mbili kushika kiti cha Rais”.

Lakini tunaweza kujiuliza iwapo utaratibu huu unainufaisha nchi kama Tanzania na katika vyama vya siasa nchini.

Na kama katiba za vyama vingine hazisemi waziwazi kuwa uongozi wa juu (mwenyekiti/katibu) uwe wa muda gani, hapo itakuwa vigumu kutabiri mchaguliwa kutoka chama kingine atafanyaje. 

Kwa vile katiba zao hazipambanui hilo wakati katiba ya nchi iko wazi kuwa kiongozi wa juu asishike madaraka si zaidi ya vipindi viwili, je, hatuoni hatari hapo ya kuja kumpata rais wa maisha? Nini kitamzuia ikiwa ndani ya chama chake hakuna kipengele kinachozuia hilo kutokea? Tutajikuta tuna demokrasia ya rais wa maisha! Hii ni hatari sana.

Mwanadamu kwa asili yake ni mwepesi sana kuona upungufu wa mtu mwingine. Nani kaona kisogo chake kilivyo? Hakuna. Lakini kila mmoja anaona vizuri sana visogo vya wenzake. Ndivyo ilivyo kwenye vyama vya siasa pia.

Kwa maana hiyo ni vigumu sana kwa vyama kuona upungufu ulio katika katiba zao, lakini wanajikita kukosoa katiba za vyama vingine. Ndiyo maana tunasikia viongozi wote wa siasa wanalilia Katiba mpya. Kwa mtazamo wao wanaiona katiba iliyopo sasa ni katiba ya chama tawala tu wala si yao! Haiwahusu na hawalazimiki kuifuata. Hilo ndilo tatizo la demokrasia.

Hebu turejee maneno ya Bwana Yesu kule Uyahudi wakati anaanza kazi yake. Akawaambia methali hii, Je, aliye kipofu aweza kuongoza kipofu? Hawatatumbukia shimoni wote wawili?… basi mbona wakitazama kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako, na boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe huiangalii? Au utawezaje kumwambia ndugu yako, ndugu yangu niache nikutoe kibanzi kilicho ndani ya jicho lako, nawe huiangalii boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe…”

Ndipo Bwana Yesu akamalizia usemi wake kwa kuwaambia wasikilizaji wake hivi: “Mnafiki wewe. Itoe kwanza ile boriti katika jicho lako mwenyewe, ndipo utakapoona vema kukitoa kile kibanzi kilichomo katika jicho la ndugu yako.” (Luka Sura ya 6, mstari wa 39,41 na 42).

Viongozi wote wa siasa katika Bara la Afrika ndivyo walivyo. Wanaona vyama vyao ni safi lakini katiba za vile vyama vingine ni vibanzi, hivyo wangependelea kuviondoa.

Ni mzee Nelson Mandela wa ANC na mzee Julius Kambarage Nyerere wa CCM ni kati ya viongozi wachache barani Afrika ambao walithubutu kukubali mabadiliko ya katiba ndani ya vyama vyao na kusema uongozi ndani ya vyama uwe na ukomo wa muda na uwe wa kupokezana. Kutokana na mtazamo wao huo, waling’atuka katika uongozi wa chama na kupisha uongozi mpya, hivyo kuendeleza ile sera ya uongozi wa kupokezana vijiti. Na kwa imani ile ile waling’atuka katika serikali, wakaenda kupumzika.

Ninajiuliza hapa Tanzania mbona hili linakuwa gumu kutekelezeka? Kila chama kinaangalia au kinalenga kushika dola tu. Lakini katiba za vyama hivyo karibu vyote zinaonyesha uimla kabisa. Hakuna nafasi ndani ya katiba kuruhusu mtu mwingine kukalia kiti cha uongozi. Je, kwa demokrasia namna hiyo tutafika kweli?

Hebu tuwe wakweli, tusiendeleze unafiki aliokemea Bwana Yesu enzi zile. Katiba za vyama vingapi barani Afrika na hata nchini Tanzania zinaruhusu huo utaratibu wa kubadilishana uongozi ndani ya vyama vyao? Au vimeweka ukomo wa uongozi ndani ya vyama hivyo? Ndiyo maana ninasema uraia sahihi hapa unahitajika sana kabla ya uchaguzi ujao.

Kule Uingereza, Marekani na hata ndani ya Jumuiya ya Madola inakubalika demokrasia ya kupokezana vijiti hata ndani ya vyama vya siasa. Hili linaonekana mara tu baada ya kila uchaguzi pale chama kinachoshindwa, uongozi wa juu wa chama kilichoshindwa unaachia ngazi na kupisha damu mpya kuongoza chama kile. Jambo hili halijapata kutokea na wala halitatokea katika nchi huru za Afrika.

Ndiyo kwanza viongozi walioshindwa uchaguzi wanatoa orodha kadha wa kadha za kasoro na kukosoa uchaguzi ule na kusema “Aluta continua, tutaendelea kupambana mpaka kijulikane.” Hiyo ndiyo tafsiri ya demokrasia katika nchi huru za Bara la Afrika.  Hapa mpaka kijulikane, ikiwa ina maana mpaka kiongozi wa chama cha upinzani ashinde na yeye awe rais. Hiyo ndiyo sababu ya viongozi kung’ang’ania kiti daima.

Suala jingine linaloonekana katika uchaguzi katika nchi huru za Afrika ni lile la vyama vya siasa kuomba watazamaji huru kutoka nje ya nchi. Hawa wanatoka Ulaya – EU, wanatoka Umoja wa Mataifa – UN, wanatoka SADC, wanatoka AU na hata kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Ninajiuliza, watazamaji hawa wanakuja kuangalia nini wakati taifa ni huru kabisa? Mbona Uingereza wamefanya uchaguzi Desemba 12, 2019 wala hapakusika watazamaji wowote kutoka nje ya Uingereza kwenda kuangalia kama uchaguzi wao ulikuwa huru? Wajerumani walishafanya uchaguzi na Wafaransa walishafanya uchaguzi wao. Je, viongozi wa nchi za Afrika walikaribishwa na vyama vya siasa kule majuu kwenda kuangalia namna uchaguzi wao unavyoendeshwa? Kwa nini sisi Waafrika Kusini mwa Jangwa la Sahara tunaomba hao watazamaji wa nje?

Kuna sheria za kimataifa zinazoagiza kuwepo kwa hao waangalizi? Au ni sisi Waafrika wenyewe tunawaomba na kuwakaribisha? Hatujiamini?

Huu ni upungufu mkubwa sana kwa viomgozi wa nchi huru za Kiafrika. Hili linaonyesha uchaguzi wetu hauaminiki, kuna wizi wa kura na hapo lazima tuombe Wazungu waje waangalie na watoe tamko kama uchaguzi wetu umekuwa huru au umeborongwa! Maskini Afrika!

Kwanza hatujiamini kama tuko huru na pili bado tunategemea matamko ya wageni kuthibitisha uwezo wetu wa kuendesha uchaguzi. Ni kweli sisi Waafrika tuko tegemezi namna hiyo katika jambo la uchaguzi?

Hapa ninapenda kukumbusha lile tamko la Baba wa Taifa alilotoa pale Chuo Kikuu cha Dar es Salam Mei 20, 1974 aliposema: “Africans are not mentally liberated yet.” Akimaanisha Waafrika hawajakombolewa kifikra. Tumejikomboa kisiasa lakini kifikra bado tu watumwa wa Wazungu. Huko ni kujidhalilisha na kuonyesha tusivyojiamini.

Inakuwaje tunadai sana demokrasia katika taifa wakati ndani ya vyama vyetu vya siasa hiyo demokrasia haimo? Tupokezane vijiti, isiwe ndani ya chama kuna ukiritimba kukalia kiti kwa zaidi ya mihula miwili huku kiongozi wewe yule yule kwa mujibu wa katiba ya chama chako huwapi nafasi wengine, bali unadai demokrasia kwenye urais ili siku moja nawe uchukue huo urais.

Hapo si ajabu hata katiba ya nchi itabadilishwa, maana malengo yako hayatakamilika kwa kipindi cha miaka 10 ya utawala, utatafuta uongezewe muda. Je, hiyo ndiyo demokrasia tunayohitaji Watanzania? Warumi zamani walituambia: “Tempora mutantur, nos et mutamur in ilLis.” Yaani muda unabadilika nasi tubadilike kama vile muda unavyobadilika. Yaani twende na wakati. Tujiweke katika mazingira ya kisasa. Rais mstaafu mzee Ali Hassan Mwinyi alipata kutamka: “Kila zama na mambo yake.”

Hii maana yake viongozi wetu na sisi Watanzania wote tuwe tayari kwa mabadiliko. Kama ulikuwa mwasisi wa chama miaka ile sasa toa nafasi kwa vijana wa leo kuendeleza yale uliyoasisi. Mabadiliko yanatokea ulimwenguni kila leo. Kusiwe na tabia ile ya ving’ang’anizi wa madaraka. Tabia inayopalilia udikteta katika utawala.

Huo ndio utaratibu aliotumia Mwalimu Nyerere alipong’atuka urais na uenyekiti wa chama alichokiasisi. Rais Magufuli ambaye alizaliwa wakati TANU inakaribia kabisa kuleta Uhuru na CCM imezaliwa akiwa kijana wa miaka 18 tu akiwa shuleni, leo hii ndiye mwenyekiti wa CCM, ana maono sahihi.

Aliwaambia viongozi wenzake Dodoma katika kikao cha Halmashauri Kuu mwezi Desemba 2019 kuwa chama hiki ni “kiwanda cha kuzalisha viongozi.” Tamko hili lina maana sana katika demokrasia.

Je, hilo halipo au haliwezekani katika vyama vingine navyo kuwa ni viwanda vya kuandaa viongozi wa kesho? Viongozi wasiwe wachoyo kutayarisha warithi ndani ya vyama vyao vya siasa, mbona wapo makada wengi tu? Wapatiwe nafasi hao vijana na wazee mtakuja kuona watakavyoichachafya CCM katika uchaguzi.

Nimalize kwa kuomba Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuandaa mtaala maalumu kwa hao watakaokuwa tayari kutoa hiyo elimu ya uraia kabla ya uchaguzi. Kusiwe na utoaji wa elimu ya uraia kiholela! Kutazuka balaa, nchi itakuja kujuta kwa nini iliruhusu hiyo elimu ya uraia uchwara kwa wapiga kura. Tunahitaji elimu ya uraia lakini kwa utaratibu unaoeleweka,  si kiholela. Basi Tanzania tujitahidi kujenga demokrasia ya Kitanzania na kamwe isiwe ya kivuli cha demokrasia za Ulaya! Tuombee uchaguzi bora 2020.

Mbenna ni Brigedia Jenerali mstaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

By Jamhuri