Tujifunze kutoka nchini Uingereza.  Nchini Uingereza wananchi wanahimizwa sana kuyasoma maandiko ya mshairi maarufu duniani, William Shakespeare.

Waingereza wanafanya hivyo ili kulinda na kudumisha mchango wa mawazo uliotolewa na mshairi huyo katika taifa lake. Wanafanya hivyo pia ili kukirithisha kizazi hata kizazi utamaduni wa kuheshimu na kukumbuka mashujaa wao.

Uingereza unapoomba kazi ya kuajiriwa, sharti la kwanza unatakiwa uwe unayafahamu mashairi kadhaa ya Shakespeare. Hapa kwetu Tanzania mambo ni tofauti kabisa. Eti tunamuenzi Mwalimu kwa kuyapa madaraja jina lake, au shule au barabara.

Hii in maana kwamba hadhi yake itakuwa inaenziwa kwa kulikuta jina la Mwalimu kwenye barabara ama shule. Ni namna nzuri lakini isiyo nzuri sana. Napendekeza lianzishwe somo maalumu la Mwalimu mashuleni, kuanzia ngazi ya elimu ya msingi hadi chuo kikuu.

Somo hili linaweza kuitwa ‘Somo la Mwalimu Nyerere’. Huo ni mtazamo wangu, lakini ningependa taifa liupokee. Kwa kufanya hivi, kizazi cha miaka 200 ijayo kitaendelea kuutambua na kuuthamini mchango wa Mwalimu katika taifa hili.

Unamkuta mhitimu wa elimu ya chuo kikuu hajawahi kusoma andishi lolote la Mwalimu Nyerere au la Shaaban Robert. Kijana anahitumu elimu yake ya chuo kikuu lakini haijui Katiba ya taifa lake.

Msomi wa namna hii tukimwita msomi ‘feki’ au msomi ‘jipu’ nafikiri tutakuwa sahihi kabisa. Halafu mtu kama huyo anapewa hadhi ya usomi katika taifa letu. Hiyo hadhi inapimwa katika vigezo vipi?  Nina mawazo tofauti katika taifa letu.

Mawazo yangu ni haya: ‘Napendekeza kila anayeomba nafasi ya urais katika taifa hili awe walau ameandika majarida ya kitafiti au vitabu’. Vivyo hivyo na mawaziri wetu tunaomba waweke mikakati ya kuongoza wizara zao kwa maandishi ili tuweze kuiona mitazamo yao. Hatuhitaji matamko ya kisiasa yaliyobebwa na mihemko isiyo na dira.

Kwa kufanya hivyo, sisi raia tutasoma kwa haraka mtazamo wa mhusika katika kulikwamua taifa kutoka kwenye mlengo wa umaskini. Mwalimu Nyerere alikuwa ni mwandishi. Mawazo yake aliyaweka katika mfumo wa maandishi na watu wote wakayasoma.

Ameandika vitabu vingi, nafikiri viongozi wengi tunaowapata sasa hivi ni wavivu wa kusoma na huu uvivu wao wa kusoma vitabu, majarida na magazeti wamewaambukiza na wale wanaowaongoza. Watanzania tukifananishwa na ‘nyumbu’ tusilaumu wala kutaharuki, sifa hii inatustahili. Kuna ukweli ambao kuupinga haiwezekani.

Watanzania hatuna utamaduni wa kusoma vitabu, magazeti na majarida na huu ndugu zangu ni ugonjwa mbaya kuliko magonjwa mengine yote. Shaaban Robert alipata kusema kweli. Alisema hivi: “Uchi wa Mtanzania uko kichwani.”

Iko hivi, hakuna tatizo linalokosa jibu katika mataifa ya watu wanaotumia akili. Taifa letu linaonekana kama taifa la watu wenye fikra duni, ni kwa sababu wasomi na viongozi wetu wamepeleka akili zao likizoni. Naomba kuikumbusha aibu ya taifa letu kwa mataifa mengine.

Ni zaidi ya miaka 55 ya Uhuru, utamaduni wa Watanzania umevaa nepi, nchi imevaa nepi, watawaliwa wamevaa nepi, watawala…, hapana, hii si Tanzania tunayotakiwa kuijenga.

Nchi ya waoga wa kuthubutu, nchi ya wanafiki, nchi ya kujipendekeza kwa watawala, nchi ya kukubali bila kuhoji. Mwalimu Nyerere akifufuka leo ataomba asizungumze chochote na kuomba arudi alikokuwa.

Leo kumekuwa na upotevu wa dira na mwelekeo wa taifa ukilinganisha na mwanzo wa maisha ya taifa letu tulipoamua kujielekeza kwenye siasa ya ujamaa na kujitegemea.

Upotevu huu wa dira na mwelekeo wa taifa lazima tuukosoe kwa juhudi zetu zote, kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kinachokuja.

1295 Total Views 3 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!