Je, ni njama za kuhujumu wanahabari?

Kuna njama za kuhujumu na kudhulumu utu na uhai wa wanahabari daima dumu. Njama hizo si ndogo, ni kubwa na zinatekelezwa usiku na mchana na wahalifu Tanzania.

Hivi tunavyozungumza wahalifu wanafaidi mali za dhuluma ya wanahabari na Watanzania katika mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Iringa, Kigoma na mingineyo, wanakula njama ya kudhalilisha uhai na utu wako, watoto wako, wazee wako na jamaa zako.

 

Ili wewe na mimi tuwapigie magoti na kuitikia ‘ndiyo bwana’, kila wanapofanya njama za kuwasulubu wanahabari. Kwa wahalifu, thamani ya uhai wako, wangu na wa mwanahabari yeyote inaanza na kuishia kwenye taaluma yetu, na uwezo wetu wa kuwatumikia.

 

Kwa hila mbalimbali zilizo wazi na za kisirisiri, kumtesa, kumsulubisha na kumuua mwanahabari anapothubutu kukataa kumtumikia.

 

Nimeanza na la mgambo hilo kuwakumbusha, kuwashitua na kuwapasha wanahabari wenzangu kuwa kuna njama ya kuua utu wetu na taaluma yetu, ili tusiendelee kufichua na kutangaza udhalimu wanaofanyiwa Watanzania.

 

Tumo kwenye masikitiko makubwa na machungu ya kina kutokana na tukio la kinyama la kumtesa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda, wiki mbili zilizopita nyumbani kwake Mbezi Beach, Dar es Salaam.

 

Tukio hili limelaaniwa na watu wote wenye kuthamini utu, upendo na amani. Tanzania imetikisika, Serikali imefadhaika na wanahabari tumehuzunika na kutatizika –  ni lipi tumewakosea Watanzania!

 

“Tunathubutu kusema kitendo alichofanyiwa mwenzetu, Kibanda, ni uthibitisho kwamba mazingira ya kazi ya uandishi wa habari nchini si salama.” Madhila haya hayana budi kuondolewa kwa kila hali.

 

Mlizamu huu wa kutesa na kuua ulianza kitambo. Nilidhani ungekoma pale Serikali ilipowakemea wahalifu kuacha vitendo hivyo. Kumbe haikuwa hivyo. Mlizamu ulipata nguvu na kububujika kufannya mto wa kuzamisha wanahabari.

 

Kwa muhtasari, mnamo miaka ya 1980, mwanahabari Stanslaus Katabalo wa Gazeti la Mfanyakazi (halipo sasa), aliuawa kwa njia ya kutatanisha baada ya kuandika habari za ufisadi. Hadi leo taarifa zake ni giza na utata mtupu!


Mwanahabari Asukile Kyando wa Shirika la habari Tanzania (SHIHATA) (nalo halipo sasa), akiwa kazini Shinyanga alipotea katika mazingira ya ajabu hadi leo haifahamiki kaburi lake liko wapi! Haya yamemfika baada ya kuandika habari za uchunguzi.

 

Saed Kubenea wa Gazeti la MwanaHALISI (pia halipo sasa) alisulubiwa na kumwagiwa tindikali. Mwandishi Richard Masatu, aliyekuwa Mhariri wa Gazeti la Kasi Mpya mkoani Mwanza, alikufa katika mazingira tatanishi. Mwaka jana, wanahabari tulimwagika machozi, kufuatia tukio la kuuawa kikatili kwa mwandishi Daudi Mwangosi wa Kituo cha Runinga cha Channel Ten mkoani Iringa. Januari mwaka huu, pia tulitokwa zaidi na machozi aliponyongwa mwandishi Issa Ngumba wa Radio Kwizera mkoani Kigoma.


Mtatiziko huo ulizidi kutia hofu, mzizimo na kilio pale mwanahabari Fredrick Katulinda wa Gazeti la Mwananchi, mwingine Shaaban Matutu wa Gazeti la Tanzania Daima walipoteswa na kupigwa kwa visingizio vya ajabu ajabu.


Februari 2013, wanahabari Abdulkarim Msengakamba wa Gazeti la Kisiwa na Christopher Lissa wa Gazeti la Sani walipata mkong’oto na kusekwa mahabusu, walipokuwa kazini katika maandamano ya baadhi ya Waislamu dhidi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP).

 

Vithibitisho vyote hivyo na vinginevyo ni ushahidi tosha kuwa wanahabari hatuko salama. Kwa hiyo hoja ya kujihami ni aula kwetu. Mkakati wa makusudi uwekwe na vyama vyetu vya wanahabari. Lengo liwe kujadili sababu au vyanzo vya matukio hayo na jinsi ya kupambana nayo pamoja na kuwapa mafunzo ya ulinzi na usalama.


Ninaiomba Serikali, hasa vyombo vyake vya usalama na ulinzi, vitekeleze ahadi zao kwa vitendo kwa kuwatia mikononi wahalifu hao. Nasi wanahabari tuamke, tusijiridhishe tu na kauli zitolewazo. Tuwe ‘vigilant’ wakati wote.


By Jamhuri