Tunakubali rushwa ni adui wa haki?

“Rushwa ni adui wa haki; sitapokea wala kutoa rushwa.”

Nimeanza na kauli hiyo kwa dhamira ya kukumbuka na kuuliza, “Wazalendo wa Tanzania wameikubali, wameizingatia na wanaitekeleza?”

Katika aya zifuatazo natupia jicho ripoti ya Tume ya Kero za Rushwa nchini, ilivyopokelewa na kutekelezwa na Serikali pamoja na raia tangu ilipoundwa na Rais wa Tanzania wa wakati huo, Benjamin William Mkapa.


Mkapa aliunda tume hiyo kwa dhamira ya kutaka Serikali itambue vyanzo na sababu za rushwa na mbinu thabiti za kuitokomeza nchini.


Aliiunda tume hiyo Januari 7, 1996 ikaanza kazi Januari 26 na kukamilisha jukumu lake hilo Novemba 6, mwaka huo, chini ya uongozi wa mwenyekiti wake, Jaji mstaafu Joseph Sinde Warioba.


Katibu wa tume hiyo alikuwa Alexander Muganda, akisaidiwa na sekretarieti. Wajumbe wengine walikuwa ni Brigedia Hashimu Mbita, Ibrahim Kaduma, Salim Othuman na Halima Kasungu.


Wajumbe wengine wa tume hiyo walikuwa ni Steve Mworia, Leonidas Gama na Balozi Fulgence Kazaura/Julius Sepeku.


Katika ripoti yake, tume hiyo ilikiri kupata kukumbwa na matatizo makuu mawili wakati wa utendaji kazi.


La kwanza ni uzito na wingi wa kazi ilizopewa, na la pili ni idadi ndogo ya viongozi waliojitokeza kuisaidia.


Kwamba Tume ilibainisha kuwa ilipata ushirikiano mkubwa kutoka kwa wananchi wa kawaida, lakini viongozi watendaji na wanasiasa waliojitokeza kukutana nayo na kutoa maoni yao kwa maandishi ni wachache wasiofika hata kumi!


Pia kulikuwapo hofu na usiri kwa baadhi ya wananchi wa kawaida katika kutaja majina yaw ala rushwa wakihofia usalama wa maisha yao. Wengine waliishia kusema, “Serikali inawajua wala rushwa.”


Katika maelezo ya jumla, Tume ilibainisha kuwa vitendo vya rushwa vinahusishwa na watumishi wa umma na wananchi wanaotafuta huduma mbalimbali, na kwamba rushwa huchochewa na mianya iliyopo katika taratibu, vishawishi, tamaa, uduni wa vipato na mmomonyoko wa maadili.


Tume ilikwenda mbali zaidi kwa kuvinyooshea kidole vyombo vya dola vinavyopaswa kuzuia rushwa lakini navyo vimejiingiza katika janga hilo, hivyo wananchi kukosa pa kukimbilia.


Leo ni miaka 17 (1996 – 2013) tangu tume hiyo ya Jaji Warioba ilipoibainishia Serikali na wananchi kuhusu kero ya rushwa.


Je, kero ya rushwa nchini imepungua, au imeongezeka?

Kabla ya kukamilisha sehemu hii ya kwanza ya mada hii ni vizuri niwarejeshe kwenye maelezo ya jumla yaliyotolewa na tume hiyo kwamba wanaodai na kupokea rushwa wamegawanyika katika makundi mawili.


Kundi la kwanza linajumuisha wanaopokea rushwa kutokana na hali yao duni ya kipato na kimaisha, hivyo wanachopewa husaidia kuziba mapengo waliyonayo.

Aina hii ya rushwa imeenea katika sekta ya uchumi kama vile elimu, ajira, ardhi, maliasili na utalii, nishati na madini.


Kundi la pili la wanaopokea rushwa ni viongozi na watumishi wa umma wa ngazi za juu ambao kuhusika kwao katika vitendo hivyo kunatokana na uroho wa kujilimbikizia mali na fedha.


Hawa ni watu wenye vipato halali vinatosheleza mahitaji yao ya msingi na wana uwezo wa kiuchumi.


1194 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!