Tusizikwe tungali hai – 2

Katika sehemu ya kwanza niligusia watangazaji wastaafu na chama chao VEMA, dira na malengo ya sera ya habari na utangazaji, na watangazaji wa ‘dot com’ na vyombo vya utangazaji. Dhana hizo tatu zimo katika mgongano wa mawazo kuhusu kuhabarisha, kuelimisha na kuburudisha Watanzania.

Wastaafu hao chini ya kaulimbiu yao ‘Tusizikwe Tungali Hai’ wanashauri watumishi na wamiliki wa vyombo vya utangazaji, kukumbuka na kuzingatia maadili na maudhui ya utangazaji yanayodumishwa katika vyombo vyao.

 

Kuajiri watumishi wenye taaluma na sifa za kuwa watangazaji, kutoa mafunzo ya kujiendeleza kitaaluma kazini, kutayarisha na kutangaza vipindi bora vya redio na runinga, kutathmini kazi za watumishi. Suala la kupokea vipindi visivyo na maadili ya Kitanzania liepukwe.

 

Huhitaji elimu ya chuo kikuu kuona na kusikia vipindi vya muziki kwa asilimia 70-80 vinarushwa hewani katika vituo vya redio na runinga ni vya muziki wa nchi za nje (Ulaya na Marekani). Nyimbo zetu za Kitanzania (hata za Afrika) zenye nasaha na mafunzo anuwai katika maisha  zinabezwa na kupondwa, eti si mali kitu!

 

Vipindi vya kuhabarisha matukio duniani havipo! Kama vipo ni vichache mno na havina habari za kina. Vya kuelimisha na kuhabarisha umma kuhusu kilimo, uvuvi na ufugaji, maendeleo ya elimu na afya, maelekezo ya amani na usalama wa jamii, na masuala ya uchumi – iwe vijijini au mijini – havipewi nafasi kama upewavyo muziki wa kizazi kipya.

 

Hii inatokana na watumishi ama hawana elimu na upeo wa masuala hayo, au ni wavivu wa kubuni na kufanya kazi walioomba na kuajiriwa.

Watangazaji wa kidotcom wanaona vipindi vya kuhabarisha  na kuelimisha vinawafaa watu wazima na wazee, wanasiasa na viongozi wananchi. Tena wanathubutu kutamka hadharani vipindi kama hivyo si vyao!

 

Vimepitwa na wakati, ni vya enzi ya analojia. Huu ni wakati wa digitali. Ama hakika, usilolijua ni usiku wa kiza.

 

Kwa ufupi niseme kuwa analojia (analog) ni mfumo wa usafirishaji mawimbi ya umeme yoyote yaani kitu kamili kwa kwenda juu, chini, juu chini (up and down) kwa muda fulani kamili. Dijitali (digital) ni mfumo wa usafirishaji wa mawimbi ya umeme vipande vipande (on and off) kwa maana kipo hakipo yaani nusu nusu hadi kuwa kitu kamili kwa muda fulani kamili.

 

Kwa maana hiyo, ndiyo maana mnatuhabarisha, kutuelimisha na kutuburudisha  kinusunusu, kivipande na matokeo yake hamjui mfanyalo na umma haufahamu myatendayo. Mbona vijana wenzenu Ulaya hawatangazi kidotcom? Si bure, mnalo jambo. Jirekebisheni.

 

Utangazaji ni taaluma inayohitaji mtu mwenye sifa ya kuwa mtangazaji. Pamoja na elimu yake ya shule au ya chuo chochote au chuo cha taaluma yenyewe na kuhodhi cheti cha awali, cheti, stashahada au shahada bado anahitaji sifa zifuatazo za kuwa mtangazaji bora.

 

Awe mwandishi mzuri wa kuandika na kusoma, mzungumzaji mzuri na mwenye lugha sanifu na fasaha (Kiswahili na Kiingereza), awe na tabia ya kujisomea na kujielimisha mambo anuwai na pia awe mbunifu katika kazi zake, awe mchapakazi na nadhifu wa mavazi na tabia. Nina uhakika wa watangazaji wa ‘dotcom’ hawana sifa hizo. Ni makanjanja ndiyo maana wanakimbilia kutayarisha vipindi vya blablaa, kuwazungumza watu, kukejeli na kufanya masihara.

 

Nadhani wakati umefika watoke huko na waende kusomea kazi hiyo, utangazaji ni kazi yenye heshima na hadhi kubwa. Baadhi ya wenye vituo vya redio na runinga muache tabia ya kuajiri watangazaji wasio na sifa wala taaluma. Mhandisi ujenzi mmoja uchwara anaweza kujenga nyumba ya ghorofa isiyo na viwango na kusababisha jengo hilo kuporomoka na kuleta hasara kwa mwenye jengo.

 

Lakini mtangazaji mmoja kanjanja anapotangaza uongo, uheke au kasumba fulani kwa umma unaomsikiliza, anabomoa umoja na maadili ya watu na kuhatarisha uelewano na mfarakano kitaifa. Nasema hivyo kwa sababu vyombo vya habari na utangazaji ni silaha, ni silaha kali na mbaya sana kuliko kisu au bunduki. Kisu au bunduki inaua mtu mmoja kwa wakati mmoja lakini chombo cha habari au utangazaji kinafarakanisha na kuua umma wa watu kwa wakati mmoja.

 

Natambua unapoomba leseni ya kuendesha kituo cha utangazaji, sharti mojawapo ni kuwa na kuzingatia sera ya habari na utangazaji ya nchi na sera yako ya kuendeshea kituo chako. Baada ya kupata leseni hufuati sera kwa nini? Haidhuru kituo chako kinaweza kuwa cha biashara, jamii au umma, Serikali bado inawajibika kuhabarisha na kuelimisha. Sera imeshatoa dira, malengo na maelekezo kuhusu vyombo vya utangazaji.

 

Leo tunashuhudia vituo 90 vya redio na 26 vya runinga kwa hatua hii hatuna budi kujikongola na vituo zaidi vitaanzishwa. Wasiwasi na mashaka yangu ni kwa watendaji na wenye vituo. Je, maudhui ya vipindi yanazingatia maadili na mandhari ya taaluma naya jamii? Vituo vinaajiri watumishi stahiki?

 

Mashaka yangu yanakwenda mbele zaidi kwa wasimamizi wa vyombo vya utangazaji. Je, vituo kweli vinazingatia athari ya matumizi ya vipindi kutoka nchi za nje kwa utamaduni na maadili ya Taifa letu, je, kweli vituo vinaimarisha amani, umoja, ushirikiano na usalama wa Taifa? Naomba wote tutafakari.

By Jamhuri