Serikali na kurupushani ya mchezo wa nyoka

Nilipokuwa na umri wa miaka saba hadi 12, nilicheza michezo mingi ukiwamo mchezo wa  nyoka. Mchezo unachezwa na idadi sawa ya watoto katika makundi mawili. Kundi la watoto na la wengine wanojifanya kuwa nyoka.

Shabaha ya mchezo ni kuweka mwili imara, kupima uwezo wa kukimbia na ujanja wa kukwepa adui. Makundi hutengana hatua kadhaa katikati yakitazamana. Mtoto mmoja huteuliwa kupiga mbiu ya hatari ya ujio wa nyoka pale walipo.


Mfano, mpiga mbiu hutangaza watoto nyoka yuko Buguruni na watoto hujibu “Naapite” Nyoka yuko Ilala “naapite”, nyoka yuko Kariakoo, “Naapite”. Watoto wanaposema nyoka huyo, ndipo watoto hupiga mayowe “nyoka wee!” na kuanza kukimbia na kutawanyika.

 

Wengine hukamatwa na wale nyoka na wengine hunusurika, mchezo hurudiwa hadi watoto wote wamekamatwa. Utaona watoto hawakujali kukimbia hadi walipoingiliwa na nyoka ndipo walipokimbia kujihami.

 

Nimekumbuka mchezo huu baada ya kusikia kuwa Serikali imekubali kuzungumza na wananchi wa Mtwara kuhusu gesi asilia. Waziri Mkuu Mizengo Pinda alitoa kauli hiyo alipokutana na wahariri wa vyombo vya habari wiki chache zilizopita Dar es Salaam.

 

Kauli hiyo imetolewa baada ya wananchi wa Mtwara na Masasi kufanya vurugu na kuharibu mali za watu na za Serikali, baadhi ya watu kujeruhiwa na wengine kupoteza maisha. Hayo yasingetokea kama Serikali ingechukua uamuzi huo mapema.

 

Tangu Desemba 2012 wananchi hao, vyama vya siasa vya upinzani, viongozi wa dini, wanaharakati na vyombo vya habari waliinasihi na waliitanabaisha Serikali kukutana na kuzungumza na wananchi wa Mtwara kuhusu gesi asilia.

 

Mbinu zote hazikufua dafu. Serikali ilijikurupusha na kujiridhisha, waliopiga mbiu zile walikuwa na lengo lao la kugombanisha Serikali na raia wake. Hata kama mbiu zile zilikusudia hivyo, haja ya kukutana bado ilikuwapo.

 

Rais Jakaya Kikwete ana msemo wake: “Akili ya kuambiwa changanya na za kwako.” Ni msemo uliojaa hekima na busara. Umejikita eneo la upendo na usalama kuliko shari, vipi Serikali ilikuwa baridi kuchanganya akili hadi maafa yalipotokea?

 

Wananchi wa Mtwara walichotaka ni mazungumzo ya pamoja kati yao na Serikali kuhusu elimu ya matumizi ya gesi asilia, itakavyosaidia kujenga uchumi na kuboresha maisha yao huku ikizingatiwa umaskini walionao muda mrefu. Leo, Tanzania kuna malalamiko mengi kuhusu uporwaji rasilimia za wazalendo na wawekezaji wanaoshirikiana na watumishi wa umma na viongozi wachache wasio na uadilifu kuhujumu uchumi wa Taifa.

 

Almasi ya Mwadui mkoani Shinyanga imelambwa yote. Dhahabu ya Nyamongo na Buhemba mkoani Mara imekombwa na tanzanite ya Arusha imefanywa rasilimali ya Afrika Kusini, mapande ya ardhi na vitalu vya kuwinda pamoja na wanyamapori kupewa wawekezaji. Kote huko wazalendo hawafaidiki hasa.


Nilifurahi Waziri Mkuu Pinda alipokwenda Mtwara na kufanya mazungumzo na viongozi na wananchi katika mikutano mbalimbali. Baada ya mazungumzo Mheshimiwa Pinda alitambua na kukiri kwamba kilichotakiwa na wananchi wa Mtwara, ni elimu kuhusu ukweli na uwazi juu ya matumizi ya gesi asilia.


Lakini Serikali kabla ya utambuzi huo, ilikwishatuhumu vyama vya siasa, viongozi wa dini na baadhi ya wananchi kupitia baadhi ya vyombo vya habari, kueneza habari kinyume cha ukweli wa matumizi ya gesi asilia na ujenzi wa bomba la gesi hiyo kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam.

 

Ukweli, habari hizo zisingepata nafasi kama Serikali kupitia watumishi waandamizi wake na vyombo vya usalama, kufanya uadilifu na kutoa elimu sahihi kwa wananchi, kwani wangechanganya akili za kuambiwa na akili zao, hivyo kukwepa ghasia kutokea.

 

Siku zote ukweli unapominywa na uwazi unapofunikwa, jawabu lake ni fujo, zahama na mfarakano. Tabia hiyo ipo tangu Serikali ya Awamu ya Kwanza. Yanayotokea leo ni majibu ya mminyo na ufuniko. Ewe Mwenyezi Mungu tuepushe na mabalaa kama hayo yasitokee tena.


Serikali haina budi kuendelea kutoa elimu ya utawala bora kinadharia na kivitendo kwa raia wake. Wananchi nao hatuna budi kutii na kufuata taratibu za utawala bora zikiwamo sheria bila shuruti na uhuru wenye mipaka.

Si busara hata chembe mkuu wa mkoa anapokataa kuwasikiliza wananchi wake, vyombo vya mabavu vya dola vinapofanya fila na kuadhibu wananchi kwa nguvu kubwa na Serikali kujipurukusha katika ukweli. Je, mnatenda haki?


Jinsi leo vyama vya siasa vinavyochochea vurugu vikitambua mali za watu zitahatarishwa na watu wengine kuumia na kupoteza maisha. Viongozi wa dini mnapoacha kuhubiri neno la Allah; na wengine kuacha kuchunga kondoo wa Bwana wapotee; na wananchi mnapokataa kuketi na kufikiri kabla ya kutenda vurugu, maana yake nini?


Namalizia kwa kuishauri Serikali kuacha kucheza mchezo wa nyoka katika maslahi na uhai wa wananchi, kuacha tabia ya purukushani, yaani kujitia hamnazo hadi inapokurupushwa au kuhimizwa na maafa.


2628 Total Views 4 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!