Vita ya kuwania nafasi ya NEC kupitia Wilaya ya Hanang’ Mkoa wa Manyara, imechukua sura mpya baada ya mmoja wa wagombea wanaoelezwa kuenguliwa kwenye Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Hanang’ kubuni mbinu mpya za kampeni.

 

Kampeni zimeanza kufanywa usiku wa manane kwa wapigakura, huku matumaini makubwa ya kambi ya mgombea huyo yakiwa kuibuka mshindi. Mmoja wa wagombea hao amekuwa akisafirisha wajumbe kutoka maeneo ya vijijini na kuwaweka katika nyumba za kulala wageni mjini Katesh, huku wakilipiwa huduma zote – malazi, chakula na vinywaji.

 

Mbinu ya kuwalaza kwenye nyumba hizo inalenga kuwaepusha kurubuniwa na kambi nyingine za wagombea. Pamoja na Dk. Mary Nagu, wagombea wengine ni Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye na Leonsi Marmo. Mmoja wa wagombea hao alifanya kampeni usiku wa manane, Septemba 9, mwaka huu, akiwasili katika ofisi za Chama Cha Mapinduzi (CCM) za Kata ya Gendabi saa 2:30 usiku na kusaini kitabu cha wageni na baada ya hapo kuzungumza na wajumbe.

 

Wajumbe aliozungumza nao wanatoka katika matawi ya Gocho, Bajomod na Giting. Mgombea huyo aliwaahidi wajumbe hao kwamba wakimchagua atahakikisha wanapatiwa misaada ya maendeleo. Septemba 11, mwaka huu, usiku saa 3:45 alionekana katika Kata ya Gendabi alikokutana na wajumbe wa kata hiyo na kuwaeleza lengo lake la kugombea nafasi ya NEC kupitia Wilaya ya Hanang’.

 

“Alitutaka tusimwangushe kwa kuwa ametutayarishia zawadi ‘nono’ endapo atashinda, na alipokuwa akiondoka akatuachia fedha tugawane,” amesema mmoja wa wajumbe waliohudhuria kikao hicho.

 

Baada ya kikao hicho aliendelea na safari yake katika Kata ya Balang’dalalu alikokutana na wajumbe katika Shule ya Msingi Balang’dalalu saa 6 usiku, huku akitumia gari la Halmashauri ya Hanang’. Mgombea huyo aliendesha kikao hadi saa 8 usiku, na kabla ya kuondoka aliwapa wajumbe hao fedha. Idadi yao ilikuwa zaidi ya 30. Miongoni mwa waliohudhuria ni viongozi wa CCM wa kata hiyo. Wajumbe waliotoka mbali walilazwa katika nyumba za kulala wageni.

 

Katika baadhi ya maeneo mgombea huyo amekuwa akikabiliwa na wakati mgumu. Septemba 11 baadhi ya wajumbe wa Kata ya Hirbadaw waligoma kupokea fedha. Baadaye waliitwa ofisi za kijiji kuhojiwa ni kwanini walikataa kupokea fedha.

 

Hoja yake kwenye vikao vyote ni kwamba endapo atakosa nafasi ya NEC atashindwa kufanya kazi vizuri. Hata hivyo, baadhi ya wajumbe walimbana wakisema huwa hatembelei kata hiyo. Maswali ya wajumbe yalimfadhaisha mgombea huyo na baadhi ya wapambe wake. Baadhi ya vijana waliokataa kupokea fedha wameshaandikiwa barua za wito wa kuhojiwa akiwamo mmoja aliyetambuliwa kwa jina la Salum.

 

Mjumbe mwingine aliyetambulika kwa jina la Kimo anabanwa sasa kwa swali lake kwa mgombea huyo, pale alipotaka kujua lini utakuwa mwisho wa kero ya ukosefu wa umeme katika kijiji chao. Kaimu Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Manyara, Samson Sanga, amesema ofisi yake haijapokea malalamiko ya kuwapo kwa rushwa miongoni mwa wagombea.

 

Hata hivyo, kuna habari kwamba Takukuru inapata kigugumizi kutokana na baadhi ya wagombea kuwa na nyadhifa kubwa. “Takukuru wanajua wazi kabisa namna rushwa inavyosambazwa huku, lakini wanamwogopa huyu mgombea,” kimesema chanzo chetu.

 

Kwa upande wake, Sumaye amekiri kupata taarifa za baadhi ya wagombea wenzake kuendesha kampeni usiku wa manane na kugawa fedha kwa wajumbe. Amesema kwa kuwa jambo kama hilo ni zito, ni vema viongozi wa CCM Taifa wakafuatilia na kupata ukweli ili hata kama ni yeye anayefanya hivyo, basi hatua ziweze kuchukuliwa.

 

Dk. Nagu hakuweza kupatikana kuzungumzia tuhuma za baadhi ya wagombea kuendesha kampeni kinyume cha taratibu na kutoa rushwa. Mwandishi kila alipompigia simu yake ya mkononi iliita bila kupokewa.


 

 

 

1281 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!