Fidia unazoweza kulipwa Serikali inapotwaa ardhi yako

Kwa kawaida Serikali hutwaa maeneo. Huhamisha  wahusika, wamiliki,  na  kuchukua  eneo  kwa  malengo  maalum  yaliyokusudiwa. Yaweza  kuchukuliwa nyumba yako, kiwanja, au  hata  shamba. 

Mara kadhaa Serikali hufanya hivi panapo mahitaji maalum ya shughuli za umma kama ujenzi wa miundombinu  kama  barabara, reli, huduma za umeme na maji, ujenzi wa shule, vyuo, vituo vya  afya na miradi mingineyo kwa manufaa ya umma. 

 

1. FIDIA YA ARDHI NI NINI

Fidia  ya  ardhi  ni  stahili  ambayo mwenye  ardhi  mmiliki  anatakiwa  kupata  pale ardhi  yake  inapotwaliwa/inapochukuliwa  na  Serikali  kwa  matumizi  maalum  ya  Serikali/umma. 

 

2. JE, UNAWEZA KUIKATALIA SERIKALI ARDHI YAKO ISICHUKULIWE?

Serikali inapotaka kumhamisha  mwananchi na kuchukua ardhi yake kupisha mradi wa umma  kisheria,  mwananchi hana uwezo wa kukataa. Hii ni kwa sababu ardhi yote ni  mali ya umma ambayo mdhamini  wake mkuu  ni Serikali kupitia mamlaka  ya  Rais. Hivyo tunaweza kusema kuwa ardhi  ni  mali  ya umma inayodhaminiwa na Serikali/Rais. 

Kwa  hiyo,  mwananchi  hawezi  kuikatalia  Serikali kuchukua  mali hiyo  isipokuwa kisheria  ni  kuwa anayehamishwa apewe fidia.  

Hata ukiamua kwenda mahakamani kupinga kutwaliwa ardhi  hutapinga kuwa Serikali isichukue ardhi yako kabisa, isipokuwa utapinga kuhusu fidia, labda fidia ndogo au utaratibu mbovu uliotumika kukadiria fidia, riba n.k. 

Labda  kuwe  na  uonevu  au  hila  katika kutaka  kutwaliwa ardhi  yako  au namna  nyingineyo  ya  nia  ovu  ndipo  unaweza kupinga  ardhi  yako  kutwaliwa. Lakini haitawezekana kupinga hatua hiyo ikiwa kuna malengo maalum ya kutwaa ardhi kwa ajili ya shughuli za umma.

 

3.  ZIJUE AINA ZA FIDIA 

Watu wengi wamekuwa wakijua kuwa fidia ni pesa tu. Linapokuja suala la fidia ya ardhi watu hudhani kinachotakiwa kutolewa na Serikali ni pesa. Hili si kweli kwa kuwa fidia haimaanishi pesa pekee kama tutakavyoona hapa chini.

(a) Fidia ya pesa. Hii ni fidia inayojulikana sana na ni aina ya fidia ambayo imekuwa ikipendwa mno na ndiyo aina ya fidia ambayo hutumiwa na Serikali mara kwa  mara  kuliko fidia nyinginezo. Maeneo ya watu hukadiriwa na hulipwa pesa kutokana na bei ya soko ya eneo husika. Imefanyika hivyo sehemu nyingi na inaendelea kufanyika.

(b) Fidia  ya  ardhi. Hii ni aina  ya  fidia  ambayo  huhusisha  kupewa ardhi.  Inachukuliwa  ardhi  yako  kwa  ajili  ya  shughuli  za  umma  unapewa  ardhi  nyingine  kufidia  iliyochukuliwa. Muhimu  ni  kuwa  usipewe  ardhi  nyingine  kama  fidia  ambayo  hadhi  yake,  ubora  wake, matumizi  yake,  na  ukubwa  wake  uko chini  ya  ile  ya  kwako  iliyochukuliwa. 

 Unatakiwa upewe ardhi yenye ubora uleule, ukubwa uleule, matumizi  yaleyale  na  hadhi  ileile. Hadhi, ubora  na  ukubwa  vinaweza  kuzidi  lakini  visipungue.  Ikiwa  utapewa  ardhi  kama fidia na ikawa chini ya ile  kiukubwa, ubora  na  hadhi  basi unayo malakamiko ya  msingi  ambayo  utayapeleka  kwa  Kamishna  wa Ardhi  au  mahakamani  ili  kupata  kiwango  cha  haki  kilichoporwa. 

Isipokuwa  hutaenda  mahakamani  kulalamika  kuwa  umepewa  ardhi  kubwa  zaidi  na  yenye  ubora  zaidi kuliko  ile  ya  kwako  iliyochukuliwa.

(c) Fidia ya jengo. Badala ya pesa  unaweza  kupewa  jengo au majengo yanayofanana  na lile  ambalo limechukuliwa au kubomolewa kupisha mradi wa  umma. Kama nilivyoeleza  hapa  juu  kuwa utatakiwa  kupewa  jengo  lenye  ubora, hadhi  na  ukubwa  uleule.  Malalamiko  utakuwa  na  haki  nayo  ikiwa  umepewa  jengo  lililo chini  ya  ubora  na  hadhi  ya  lile lililochukuliwa.

(d)  Fidia ya  kutumia  mali  za  umma.  Hii  ni  aina  ya  fidia  ambapo baada ya   kuchukuliwa  ardhi  yako,  kwa  mfano,  jengo  ambalo  ulikuwa  ukipokea  kodi  unapewa  jengo  jingine si kwa  kulimiliki  bali  kulitumia   ambapo  unaweza  kuwa  ukichukua  kodi  kama  mmiliki  kwa  muda  fulani  utakaokubaliwa  mpaka  hapo  kiwango  cha  pesa  ambacho  ungelipwa kama  fidia  kitaisha.  Hii  pia  hutumika   kufidia  mashamba   ambapo  utapangiwa  kutumia  shamba  la  umma  kwa  muda  fulani  kufidia  la  kwako  lililochukuliwa. 

(e) Fidia ya  miche  na  mimea.  Hii  hutolewa  panapo  uharibifu  wa  miche  na  mimea  katika  eneo  lako. Yawezekana  eneo  lililochukuliwa  lilikuwa na miche  na  mimea  na  imeharibiwa.  Si  lazima  upewe  pesa  unaweza  pewa  miche  na  mimea  yenye  hadhi  na  ubora  kama  wa  ile  ya  kwako. Hii hujumuisha fidia  ya  mazao  na  nafaka  pia.

( f) Fidia  kwa  makubaliano.  Hii  ni  aina  ya  fidia  ambapo  mdai  na  Kamishna  wa  Ardhi  hukaa  meza  ya  mazungumzo  na  kukubaliana  aina  ya  fidia  inayofaa  kwa  kiwango  cha  ardhi, jengo  lililochukuliwa  kupisha  mradi. Hapa  fidia  inaweza  kuwa  yoyote  kutegemea  na  makubaliano ya  pande  hizo  mbili.

Haya  yote  ni  kwa  mujibu  wa Sheria  ya  Ardhi  ya 1999 na  Sheria  ya  Ardhi ya Vijiji ya 1999.

 

Kuhusu sheria za ardhi, mirathi, makampuni, ndoa n.k, tembelea SHERIA YAKUB BLOG.