Bunge linapoteza hadhi, tusitarajie bajeti makini

Kuna kila dalili kuwa Mkutano wa Bunge unaoendelea sasa mjini Dodoma, hautapitisha bajeti inayojibu matatizo yanayowakabili wananchi kwa mwaka wa fedha 2013/2014.

Ninasema hivyo kwa sababu mkutano huo umeendelea kupoteza hadhi ya Bunge tangu ulipoanza Aprili 9, mwaka huu. Limekuwa Bunge la matusi, vijembe, kejeli na ubabe usio na tija kwa umma.

 

Tumewashuhudia na kuwasikia wabunge kadhaa (sina haja ya kuwataja), wakitumia muda mwingi kutupiana maneno makali, kulumbana na kuchambana. Ni kazi ambayo hawakutumwa na wapigakura wao. Ni utovu wa nidhamu, ubabe na kulidhalilisha Bunge.

 

Baadhi ya wabunge wameligeuza Bunge kuwa kijiwe cha mambo ambayo si hasa (siasa). Wanataka kuonekana vinara wa kuzungumza bungeni hata kama wanachozungumza hakina tija kwa wananchi walio wengi.


Ikiwa wabunge wa aina hii wataendeleza kasumba hii na kulitawala Bunge, basi Watanzania tusitarajie bajeti makini. Naam, itakuwa vigumu kwa wabunge wanaotawaliwa na hisia za chuki, unafiki, kuonana maadui na kutoaminiana kupitisha bajeti itakayopoza makali ya maisha ya dhiki yanayowakabili wananchi.


Ni fedheha kwa wabunge kutumia wasaa mwingi kupimana nguvu ya kutupiana maneno makali, na kusondana vidole kuhusu mambo yasiyo na maana bungeni badala ya kujikita katika kutetea maslahi ya umma. Ni matumizi mabaya ya madaraka.


Unapoona Kiti cha Spika hakiheshimiwi, kinakosa hekima, baadhi ya wabunge ‘wanazibwa midomo’ na wengine wana utovu wa nidhamu, basi usitarajie uwajibikaji mzuri wa Bunge.

 

Watanzania tumekuwa na matarajio kwamba Bunge la Bajeti linaloendelea mjini Dodoma, lingeibuka na dawa thabiti ya kuboresha maisha yetu kiuchumi na kijamii. Lakini dalili zinaonesha ndoto zetu hizi hazitatimia.

 

Je, tutakuwa wageni wa nani ikiwa watu tuliowachagua kutuwakilisha bungeni katika kutafuta maendeleo yetu wamekwepa jukumu hilo? Tutaendelea kutafunwa na matatizo lukuki huku wachache hao wakijineemesha na familia zao.

 

Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alipata kusema; “Kutokana na umri wake mkubwa, watu wengi wenye kasoro wamejiingiza kwenye chama hiki. Sasa kimekuwa kama kokoro ambalo wakati mwingine hubeba viumbe visivyohitajika. Tunao watu wa ajabu ndani ya CCM ambao hawafanani na CCM.”

 

Bunge letu siku hizi tunaweza kulifananisha na kokoro lenye wabunge kadhaa wasiostahili wadhifa huo, lakini pia wasiofanana na Bunge. Taswira hii ni hatari kwa mustakabali wa mhimili huu muhimu wa dola.


Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi) naye kwa upande wake, amepata kusema; “Tunahitaji kuwapima DNA (Vinasaba) viongozi wetu kubaini kama kweli wana asili ya Tanzania, maana kwa namna wasivyotujali ni kama si Watanzania wenzetu.”

 

Matendo ya wabunge wengi ni tofauti na waliyoahidi wakati wa kampeni za kuomba ridhaa ya wananchi kuwawakilisha bungeni. Waliahidi kutetea maslahi ya umma kwa uzito unaostahili, lakini mambo ni tofauti. Kwa jinsi wanavyotanguliza maslahi yao binafsi na kuwasahau wanyonge, unaweza usiamini kwamba ni Watanzania wenzetu.


Ingawa Bunge hili la Bajeti bado lina safari ndefu, lakini ishara zinazooneshwa na baadhi ya wawakilishi wetu zinatuvunja moyo.


Wengi tuna wasiwasi kuwa halitapitisha bajeti inayolenga kuwapunguzia Watanzania, walio wengi, mzigo wa matatizo yanayowanyima maendeleo.

 

Watanzania tunapenda kuona na kusikia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linajikita katika kujadili na kupitisha bajeti yenye manufaa kwa umma.

Malumbano, ubabe, matusi, kejeli na utovu wa nidhamu bungeni haviwezi kuzaa bajeti makini inayojibu matatizo ya wananchi. Haviwezi kamwe!


By Jamhuri