Dalili mbaya CCM kuelekea 2015

Ni dhahiri kuwa sasa dalili mbaya zimeanza kuonekana ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Tanzania, mwaka 2015.

Kauli ya Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, kwamba yeye na rafiki zake watatu ambao ni mawaziri ndiyo watakaoweka mgombea urais, ni kielelezo cha mgawanyiko usio wa kawaida wa vigogo ndani ya chama hicho tawala.

 

Waziri Sitta alitoa kauli hiyo kwenye kongamano la mawasiliano ya kidijitali la wanafunzi wa Idara ya Uhusiano na Masoko katika Chuo Kikuu cha Tanzania cha Mtakatifu Augustino (SAUT) jijini Mwanza, wiki iliyopita.

 

Kwa mujibu wa Gazeti la Mwananchi la Mei 28, 2013, Waziri Sitta aliwataja rafiki zake hao kuwa ni mawaziri Bernard Membe (Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa), Dk. John Magufuli (Ujenzi) na Dk. Harrison Mwakyembe (Uchukuzi).

 

Sitta aliwataja rafiki zake hao pia katika harambee ya kuchangia maendeleo ya Kanisa Katoliki la Mtakatifu Josephine Bakita, Parokia ya Igoma jijini Mwanza.

 

Binafsi ninaungana na wengine wengi kuamini kuwa si dhambi kwa mwananchi yeyote kutangaza nia yake ya kushiriki kinyang’anyiro cha uongozi hapa nchini. Hiyo ni haki ya kidemokrasia ya kila Mtanzania.

 

Lakini ‘Fikra ya Hekima’ inashawishika kuamini kwamba kauli hiyo ya Waziri Sitta ni zaidi ya haki ya kidemokrasia. Ina sura ya kibaguzi ndani ya CCM.

 

Hii ni sawa na kusema kwamba kundi hilo (Sitta, Membe, Dk. Magufuli na Dk. Mwakyembe) limeshajibagua na kujiona kuwa ndilo lenye madaraka ya kumweka mgombea atakayepeperusha bendera ya CCM katika kinyang’anyiro cha urais mwaka 2015.

 

Angalau Dk. Magufuli amejitokeza kukanusha kauli hiyo kwamba hahusiki katika kundi lililotajwa na Sitta, huku akisisitiza kuwa hafikirii kuwania urais. Lakini pia amesema hakupata kuzungumza na waziri huyo wa Afrika Mashariki kuhusu suala hilo.

 

“Sina kundi. Sijawahi kuwa na kundi na sitarajii kuwa na kundi lolote. Ninachojua kundi langu ni CCM na kiongozi wake ni mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete,” amesema Dk. Magufuli.

 

Pengine Sitta ametoa kauli hiyo kutuma salamu na tambo kwa vigogo wengine ndani ya CCM wanaotajwa kukodolea macho urais. Hiyo ni dalili mbaya ndani ya chama hicho kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao.

 

Kuna vigogo lukuli ndani ya CCM wanaotajwa kuwa na sifa za kugombea urais. Wengine wamejitangaza wenyewe. Hatuwezi kuvinyooshea kidole vitendo hivyo kwani wanaofanya hivyo wana haki ya kidemokrasia.

 

Orodha ya wanaotajwa kuwa wanafaa kugombea rais kupitia CCM ni ndefu. Wamo Edward Lowassa (Mbunge wa Monduli na Waziri Mkuu mstaafu), Stephen Wasira (Waziri wa Uhusiano na Uratibu), Shamsi Vuai Nahodha (Waziri wa Ulinzi na JKT) na Profesa Anna Tibaijuka (Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi).

 

Wengine ni Profesa Sospeter Muhongo (Waziri wa Nishati na Madini), Dk. Emmanuel Nchimbi (Waziri wa Mambo ya Ndani), January Makamba (Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia) na Frederick Sumaye (Waziri Mkuu mstaafu).

 

Kwa hiyo, kitendo cha Waziri Sitta kutangaza kuwa wakati ukifika, yeye, Membe, Dk. Magufuli na Dk. Mwakyembe watachagua mmoja wao kuwania urais, kimewabagua wana CCM wengine walio kwenye orodha hiyo. Hii si dalili nzuri ndani ya CCM.

 

Basi, siku nyingine tunaweza kuwasikia Lowassa, Wasira, Dk. Nchimbi na Profesa Tibaijuka nao wanaunda kundi la kirafiki litakaloandaa mgombea urais.

 

Vivyo hivyo, hata Sumaye, Profesa Muhongo, Makamba na William Lukuvi (Waziri wa Sera, Uratibu na Bunge) nao wanaweza kujipambanua kuwa ndiyo watakaochagua mmoja wao anayefaa kuwa Rais wa Tanzania mwaka 2015. Kwa hiyo lazima kutakuwa na msuguano utakaopunguza nguvu ya CCM katika uchaguzi huo.

 

Hata hivyo, kwa upande mwingine msuguano huo utaviongezea vyama vya upinzani mwanya wa kupenya na hatimaye kimojawapo kufanikiwa kuingia Ikulu. Watanzania watakuwa wamefanya mabadiliko ya utawala, ambayo si siri yanasubiriwa kwa shauku kuu.

 

Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete, inawezekana anapenda kukiacha chama hicho kikiendelea kushika madaraka ya nchi. Basi, bila shaka hatachelewa kukemea dalili mbaya zinazooneshwa na baadhi ya wanachama wake kuelekea Uchaguzi Mkuu, mwaka 2015.

By Jamhuri