Wabunge hawa hawatufai

 

Nianze kwa kuwapa pole mawaziri Shamshi Vuai Nahodha (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa), Balozi Khamis Kagasheki (Maliasili na Utalii), Dk. Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani ya Nchi) na Dk. Mathayo David Mathayo (Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi), waliopitiwa na rungu la Rais Jakaya Kikwete la kuvuliwa nyadhifa hizo, wiki iliyopita. Huo ndiyo uwajibikaji wa kisiasa.

Lakini kwa upande mwingine, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeendelea kudhalilishwa na baadhi ya wabunge ambao bila shaka dhamira yao ni zaidi ya uongozi wa kuwatumikia wananchi.

 

Inashangaza kuona na kusikia kwamba kadiri siku zinavyozidi kusonga mbele, ndivyo vitendo vya hujuma dhidi ya Bunge vinavyozidi kuongezeka. Wabunge ambao kimsingi ndio wanapaswa kuwa wa kwanza kulinda hadhi ya Bunge, baadhi yao wameendelea ‘kulichafua’.

Vikao vya Bunge siku hizi vinatia aibu. Tunashuhudia viti vingi vikiwa wazi kutokana na utoro wa wabunge wengi! Tatizo la matumizi mabaya ya madaraka kwa wabunge limetanuka kutoka kwenye utoro wa vikao vya Bunge hadi ‘kulamba’ posho za ziara za kibunge, kisha kuziepa. Ni aibu kubwa! Wiki iliyopita Spika wa Bunge, Anne Makinda, aliguswa na tatizo la hujumu ya posho za ziara za kibunge na kusisitiza kwamba wabunge waliozipokea bila kwenda ziara husika lazima wazirudishe.

“Waheshimiwa wabunge nimesema kama mlichukua pesa bila safari, mnarudisha… Wote kabisa ninawajua na ninalifanyia kazi. Wote waliochukua pesa warudishe, ndiyo utaratibu wa Serikali… Wote watarudisha,” alisisitiza Spika.

Sakata la hujuma ya posho za Bunge liliibuliwa bungeni na Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba (CCM), alipoomba mwongozo wa Spika akitaka kujua hatua zinazopaswa kuchukuliwa dhidi ya mbunge aliyechukua posho kwa ajili ya safari za kibunge, lakini akakwepa na kwenda safari binafsi.

Vitendo vya utoro wa wabunge kwenye vikao vya Bunge na uhujumu wa posho za ziara za kibunge vinavyoendekezwa na baadhi ya wabunge haviwezi kujitenga na ufisadi unaohusisha matumizi mabaya ya madaraka.

Vitendo hivyo vinadhihirisha wazi kuwa baadhi ya wabunge walitafuta nafasi hiyo kwa ajili ya kuitumia kujitafutia maslahi yao binafsi, siyo kuwatumikia wananchi. Wabunge wanapotumia fedha za Bunge kushughulikia mambo yao binafsi, yasiyo na tija kwa Bunge na umma ni usaliti mkubwa kwa wananchi ambao ndiyo chanzo cha fedha hizo kutokana na kodi wanazotozwa na Serikali kwa njia mbalimbali.

Madhara ya utoro wa wabunge bungeni na hujuma ya posho za ziara za kibunge ni makubwa katika jamii ya Watanzania, ikiwa ni pamoja na kuwakosesha maendeleo waliyotarajia. Vikao vya Bunge huandaliwa kwa gharama kubwa inayotokana na kodi za wananchi. Mbunge asipovihudhuria bila sababu za msingi anakuwa ameupunja umma wa Watanzania wanaomtegemea kuchangia mijadala ya maendeleo ya taifa letu.

Kwa upande mwingine, mbunge asipohudhuria ziara za kibunge ndani na nje ya nchi huku akiwa ameshapokea posho, anakuwa amelidhoofisha Bunge kwa kulipunguzia idadi ya wabunge wenye uelewa wa mambo yenye tija kwa umma yaliyoandaliwa katika ziara hizo.

Dalili zinaonesha kuwa idadi ya wabunge wahujumu Bunge itaendelea kuongezeka ikiwa uongozi husika hautaharakisha kuchukua hatua kali za kinidhamu na kisheria dhidi ya wahusika ili iwe onyo kwa wengine wanaojiandaa kuiga kasumba hiyo.

Njia nyingine itakayosaidia kudhibibiti vitendo vya kulihujumu Bunge ni wananchi kuhakikisha tunakuwa makini kwa kuchangua wabunge waadilifu na wenye dhamira ya kweli ya kutuwakilisha bungeni. Wabunge watoro bungeni na matapeli wa posho za Bunge hawatufai, tuwakatae.

Tunaweza kusema Spika wa Bunge ametumia mamlaka yake vizuri kwa kuahidi kuwabana wabunge waliotapeli posho za ziara wazirejeshe. Lakini hata hivyo, kuna swali la kujiuliza: Kwanini amechelewa kuchukua hatua hiyo wakati tatizo hilo inasemekana ni la muda mrefu, halijaanza juzi?

Umefika wakati Bunge litimize wajibu wake kwa Watanzania. Lijikite katika kujadili na kupitisha masuala yenye majibu sahihi ya matatizo yanayowanyima wananchi maendeleo kwa muda mrefu sasa.

Vitendo vya utovu wa nidhamu, utoro wa wabunge bungeni na utapeli wa posho za vikao na ziara za kibunge, pamoja na ushabiki wa kisiasa wenye sura ya kuvibeba vyama vya siasa usiyo na tija kwa umma vidhibitiwe kwa nguvu kubwa.

Bunge lirejeshewe hadhi yake. Taratibu na kanuni za Bunge zizingatiwe na kufuatwa na kila mbunge. Wabunge wahujumu Bunge siyo chagua la Watanzania walio wengi. Hao ni watu waliojipanga kuchafua taswira nzuri ya Bunge mbele ya umma, huku wakisukumwa na ‘roho mtaka-vitu’. Hawatufai kabisa!


 

By Jamhuri