Tumeruhusu kucheka na nyani shambani, tutavuna mabua

 

Ni wazi sasa maji yanaelekea kuuzidi unga! Nchi yetu iko katika hatari ya ‘kuvuna mabua’ kufuatia kasumba ya kutoa mwanya wa ‘kucheka na nyani shambani’. Serikali na vyombo vyake vya dola vitabaki kulaumiwa, kwa kushindwa kudhibiti mfululizo wa matukio ya kutisha yakiwamo mauaji ya watu kikatili.

Wiki iliyopita tumesikia na kushuhudia anguko kubwa la wahitimu wa kidato cha nne nchini. Asilimia 60 wameishia kupata sifuri! Hili ni pigo la kihistoria nchini.


Machafuko ya kidini yanaelekea kuota mizizi, huku nchi ikiwa haijapona majeraha ya mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino), matumizi mabaya ya madaraka na ubadhirifu wa mali za umma. Lakini pia, migogoro ya wakulima na wafugaji.


Baadhi ya wananchi wanajichukulia sheria mkononi –  wanaua askari polisi na kuteketeza kwa moto vituo vya polisi, magari na majengo ya serikali!


Februari 10, mwaka huu, Mchungaji Mathayo Kachila (45) wa Kanisa la Pentecostal Assemblies of God Tanzania (EAGT) mkoani Geita, aliuawa kikatili katika vurugu za kugombea uchinjaji wanyama baina ya Wakristo na Waislamu!


Lakini pia, Februari 17, mwaka huu, Padri Everist Mushi (pichani kulia) wa Kanisa Katoliki aliuawa kinyama kwa kumiminiwa risasi za moto mjini Unguja. Siku tatu baada ya mauaji hayo, Kanisa la The Pool of Siloam lilichomwa moto mkoani Kusini Unguja.


Matukio ya mauaji ya viongozi hao wa kiroho na uchomaji wa kanisa hilo, yamekuja miezi kadhaa baada ya watu wanaodhaniwa kuwa waumini wa Kiislamu kuvamia na kuharibu makanisa, magari na mali nyingine eneo la Mbagala, Dar es Salaamu, kufuatia tukio la mtoto wa Kikristo kukojolea kitabu cha dini ya Kiislamu (Qur’an).


Hata hivyo, ni faraja kubwa kuona kwamba kwa muda wote wa matukio hayo, Wakristo wamekuwa wavumilivu kuepusha maafa zaidi nchini. Lakini pia baadhi ya viongozi wa Kiislamu wamesikika mara kadhaa wakiwataka waumini wa dini hiyo kuepuka kutumia nguvu katika kutatua matatizo yanayogusa hisia za kiimani.


Kuna watu wasioitakia mema nchi hii, na wanaendelea kuhatarisha amani na mshikamano wa Watanzania. Hawa ni pamoja na walioamua kukumbatia migogoro ya kidini, ushirikina, chuki za kisiasa na maovu mengine yasiyokubalika katika jamii.

 

Uwajibikaji wa Jeshi la Polisi katika kulinda usalama wa raia na mali zao haujaridhisha. Baadhi ya watuhumiwa wa uhalifu wanaachiwa katika mazingira tatanishi.


Serikali haijaonesha dhamira ya dhati katika kudhibiti uhalifu nchini. Ni kama imeruhusu kucheka na nyani (wahalifu, waanzilishi na wachochezi wa chokochoko) katika shamba la mahindi, ili hatimaye Watanzania wapate hasara ya kuvuna mabua (kugawanyika, kuingia katika mapigano ya wenyewe kwa wenyewe)!


Kwa ukweli usiopingika, serikali yetu haina sababu ya msingi ya kutafuta mchawi wa matukio ya kutisha nchini. Imejiloga yenyewe kwa kutotekeleza ipasavyo wajibu wake wa kusimamia sheria, licha ya kuwa na uwezo wa hali na mali wa kudhibiti matatizo yanayoitafuna nchi.


Rais wa 16 wa Marekani, Abraham Lincoln, alipata kusema; “Nitajitahidi kurekebisha makosa pale itakapothibitika kuwa kweli ni makosa, na nitajitahidi kuyapokea mawazo mapya pale itakapothibitika kuwa ni mapya, na ni ya kweli.”


Serikali ikiri makosa ya kulegea katika kusimamia sheria na kudhibiti uhalifu, ijirekebishe na kupokea mawazo mapya katika kutafuta ufumbuzi wa matatizo yanayoiandama nchi. Tanzania yenye serikali sikivu kwa wananchi wake inawezekana.


 

1119 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!