Nimeipenda kauli ya Mbowe Mbeya

Kwa mara nyingine, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, ameendelea kudhihirisha mng’aro wake katika nyaja ya siasa nchini.

Safari hii, Mbowe amedhihirisha ukomavu wake wa kisiasa wakati akihutubia umati wa wananchi mkoani Mbeya, Alhamisi iliyopita.


Mwanasiasa huyu ametumia nafasi hiyo kuwataka wafuasi wa Chadema kuachana na siasa za vurugu, lakini pia kuepuka kujenga uhasama na vyombo vya dola nchini. Amefafanua kuwa siasa za kiharakati na vurugu zimekuwa zikisababisha chama hicho kueleweka vibaya miongoni mwa jamii.

 

Ameongeza kuwa siasa za chuki na vurugu zimepitwa na wakati, na kwamba sasa ni wakati wa wafuasi wa Chadema kubadili mfumo wa siasa zao ili kukijengea mikakati imara ya kukiwezesha kukubalika zaidi kwa Watanzania.


“Msikubali kujiingiza kwenye uhasama na vyombo vya dola, wala kuingia katika mitego ya kuhatarisha amani…,” amesema Mbowe.


Kwa upande mwingine, kiongozi huyo wa Chadema ametuma salamu kwa vyombo vya dola, kuheshimu haki za kisiasa ili kuepusha malumbano na vurugu zisizo za lazima baina ya vyombo hivyo na wafuasi wa chama hicho.


Binafsi nimeipenda kauli hiyo ya Mbowe, kwani imedhihirisha msimamo wake uliojaa busara, hekima na dhamira njema ya kulinda na kutetea amani ya Taifa letu. Ni ukweli usiopingika kuwa kama kauli hiyo itazingatiwa na wafuasi wa Chadema, itakijengea chama hicho mazingira mazuri kuelekea Uchaguzi Mkuu mwaka 2015.

 

Hii ni mara yangu ya pili kumpongeza Mbowe kutokana na ukomavu wake wa kisiasa. Mwaka jana niliandika makala ya kumpongeza kutokana na majibu yake dhidi ya kauli ya Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (Chadema).

 

Mbowe alisema, “Si sera ya Chadema kuhamasisha kujitenga kwa Ukanda wa Kaskazini. Chama chetu kinahitaji watu kutoka maeneo mengine kushirikiana kuondoa siasa mbaya…”

 

Mwenyekiti huyo wa Chadema alitoa kauli hiyo kuzima jaribio la Nassari, lililotafsiriwa kuwa ni uhamasishaji wa dhana ya ubaguzi wa Watanzania katika matumizi ya rasilimali za madini, ardhi na maeneo ya utalii nchini.

 

Akihutubia mkutano wa hadhara wa wananchi mkoani Arusha uliokuwa na kaulimbiu ya ‘Vua gamba, vaa gwanda’, alitamka kuwa umefika wakati wa Ukanda wa Kaskazini mwa Tanzania kujitenga na kuunda taifa lake huru, kwani umesheheni rasilimali nyingi.


“Tuna utajiri wa madini, maeneo mazuri ya utalii na ardhi ya kutosha kuunda nchi yetu wenyewe. Tunapaswa kutafuta uhuru wetu wenyewe badala ya kuruhusu wengine ambao hawafurahishwi na mabadiliko kuendelea kutuchelewesha,” Nassari alikaririwa akitamka hayo.


Mbunge huyo wa Arumeru Mashariki anadaiwa pia kutoa kauli ya kumpiga marufuku Rais Jakaya Kikwete kutia mguu jimboni humo na Kanda ya Ziwa, akidai maeneo hayo ni himaya ya Chadema!

 

Hata hivyo, mara baada ya kusikia matamshi hayo ya Nassari, Mbowe alisimama na kuyakana mkutanoni hapo na kuwataka wananchi kutoyatafsiri kama ndiyo sera ya Chadema, bali yabaki kuwa ya Nassari binafsi.

Binafsi ninaendelea kuamini kuwa Mbowe ni mtu makini katika masuala ya siasa na uongozi. Ni mwanasiasa mwenye busara na hekima, asiyependa kuona na kusikia amani ya nchi yetu inachezewa.


Nakumbuka pia wakati fulani katika moja ya mikutano yake ya kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka 2005, akiwa wilayani Tarime, Mbowe aliyekuwa mgombea urais, alihimiza sana suala la ulinzi wa amani nchini.


Alifikia hatua ya kuwataka wakazi wa Tarime mkoani Mara wasimchague, kama kwa kufanya hivyo kutasababisha umwagaji damu miongoni mwa wananchi.


“Suala la amani ni muhimu sana kwa Taifa letu, kama mtafikia hatua ya kupigana hadi kumwaga damu kwa ajili ya kutaka niwe rais ni bora msinichague… mimi sitaki kupata uongozi kwa njia ya umwagaji damu,” alisema Mbowe.


Mifano niliyoitoa hapo juu inadhihirisha wazi ukomavu wa Mbowe katika masuala ya siasa na uongozi. Ni mfano mzuri wa kuigwa na wanasiasa wengine nchini. Taifa letu linahitaji viongozi na wanasiasa wa aina ya Mbowe.


By Jamhuri