*Amejenga ghala Chang’ombe, kazi inafanywa kwa siri

*Huyavusha hadi Nairobi kwa kuyaficha kwenye ngoma

Mfanyabiashara mwenye asili ya kiasia, anaendesha biashara ya siri ya kusafirisha mchanga wenye madini kutoka migodini na kufanya uchenjuwaji katika ghala lake lililopo Dar es Salaam.

Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa mfanyabiashara huyo anapata mchanga huo kutoka katika migodi kadhaa iliyopo katika mikoa ya Tabora, Shinyanga na Geita. Kwa sasa jina la mfanyabiashara huyo tunalihifadhi kwa kuwa hatujampata aweze kuzungumzia suala hili.


Ghala lake lipo katika Barabara ya Sanza, Chang’ombe jijini Dar es Salaam; karibu na ghala moja linalotumika kuhifadhi mbolea.


Uchunguzi umebaini kuwa mfanyabiashara huyo amekuwa akiendesha biashara hiyo kwa miaka kadhaa sasa; huku baadhi ya maofisa katika Wizara ya Nishati na Madini wakiwa na taarifa, lakini wamekuwa kimya kwa kile kinachoelezwa kwamba wanalipwa.


Ndani ya ghala ambamo kunaendeshwa shughuli za uchenjuwaji, kuna shimo kubwa ambalo linatumika kuhifadhi mchanga uliokwishatolewa madini.


Chanzo cha habari kimesema kwamba mchanga huo hujazwa katika viroba kutoka migodini, na mara nyingi husafirishwa kwa kutumia magari aina ya Fuso. Inaelezwa kuwa Fuso lenye shehena hiyo huwasili katika ghala hilo kila baada ya wiki moja au mbili. Desemba 8, saa tatu usiku, Fuso lilishusha shehena ya mchanga unaosadikiwa kuwa na madini katika ghala hilo.


Baada ya madini, ikiwamo dhahabu kuchenjuliwa, mfanyabiashara huyo huyasafirisha hadi nchini Kenya kwa kutumia magari na meli.


Madini hayo, pamoja na nyara nyingine, hufichwa ndani ya ngoma ndogo ndogo ambazo nazo zinawambwa katika karakano iliyo karibu na ghala hilo.


“Madini huwekwa ndani ya ngoma, wanapofika kwenye vuzuizi maelezo huwa kwamba ngoma hizo zinapelekwa kuuzwa Mombasa au Nairobi ambako wateja wao wakuu ni watalii. Kwa kuwa kinachoonekana huwa ni ngoma, hakuna ukaguzi mkubwa unaofanywa, hapa pia kodi kuna mazingira ya ukwepaji kodi ya Serikali,” kimedokeza chanzo chetu.


Imeelezwa kwamba mfanyabiashara huyo amejitahidi kupata leseni inayomtambulisha kama mchimbaji mdogo ili kumrahisishia kusafirisha mchanga wenye madini.


“Kwa sasa tunavyozungumza ana leseni kama mchimbaji mdogo wakati ukweli ni kwamba hana mgodi. Mchanga wenye madini anautoa kwenye migodi mikubwa; na hii inatufanya tuamini kuwa huenda amekuwa na uhusiano wa karibu na wenye migodi hiyo au walinzi,” kimesema chanzo chetu.


Habari zaidi zinaeleza kwamba kabla ya kugeukia shughuli hiyo ya madini, mfanyabiashara huyo alikuwa kinara wa kutorosha nyara za Serikali, hasa pembe za ndovu na ngozi za samba kwenda kuziuza nje ya Tanzania, shughuli ambayo hata hivyo, baadaye alilazimika kuiacha baada ya kuhisi anakaribia kugundulika.


Kamishna wa Madini nchini, Mhandisi Ally Samaje, ameiambia JAMHURI kwamba Wizara ya Nishati na Madini, haina taarifa zozote juu ya mfanyabiashara huyo kupewa leseni ya mchimbaji mdogo.


“Najua huyo (mfanyabiashara) anaweza kuwepo, ila huenda akawa ametumia jina jingine kuomba leseni na kuitumia kinyume, ni kosa la jinai. Tukimgundua tutamchukulia hatua mara moja ikiwa ni pamoja na kumfutia leseni,” amesema Samaje.


Duru za uchunguzi zinaonesha kuwa watu maalumu wanaolipwa vizuri na waaminifu wa kutunza siri, ndiyo wanaopewa kazi ya kupakua na kuchenjuwa mchanga wenye madini ghalani hapo nyakati za usiku.


1060 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!