maguZimeanza kujitokeza lawama kwamba Rais John Pombe Magufuli anakwenda nje ya haki za binadamu katika utendaji wake wa kazi, kwa mtindo wake maarufu wa ‘kutumbua majipu’. Baadhi ya watu wanadai kwamba mtindo huo alioubuni Magufuli wa kutumbua majipu unaonekana kuzikiuka haki za binadamu!

 Haijaeleweka ni haki gani wanazozidai watu hao kwamba Magufuli anazikiuka. Ila ningetaka kuwakumbusha kwamba ugonjwa wowote unakiuka haki za maumbile ya binadamu, haijawahi kutokea ugonjwa ukazijali haki za binadamu. Maana ugonjwa huleta maumivu, kitu ambacho tunaweza kusema kwamba ni ukiukaji wa haki za binadamu.

 Kwa hiyo, kwa vile ugonjwa unakiuka haki za binadamu, kuutibu ugonjwa hakuwezi kuzingatia haki za binadamu kwa sababu unasababisha maumivu katika mwili wa binadamu. Na kwa mantiki hiyo, ni lazima kuutibu ugonjwa kulete maumivu pia, lakini ni maumivu ya muda yenye matumaini ya muda mrefu. 

Kwa hiyo, anayesumbuliwa na ugonjwa ni lazima avumilie maumivu ya muda mfupi akiwa na matumaini ya kupata nafuu au kupona kabisa. Ndiyo maana Waswahili wakasema kwamba dawa hulii kunoga. Na dawa chungu ndiyo mara nyingi inayotibu haraka na kwa usahihi zaidi.

 Baada ya maelezo hayo, tunaweza kuona kwamba anachokifanya Rais Magufuli ni kitu chenye lengo jema, kuwaondolea wananchi usumbufu wa muda mrefu kwa kuwaondoa watu wanaosababisha usumbufu huo, tena kuwaondoa kwa muda mfupi bila mjadala.

 Haiwezekani baadhi ya watu, tena walio wachache, wakiwa ni watumishi wa umma wakose ubinadamu kwa kutowatendea haki wananchi walio wengi lakini wao watake kutendewa kinachoitwa ‘haki za binadamu’ wakati wa kuwajibishwa. Hilo ni jambo linaloelekea kwenye uchizi, watu kukosa kutenda haki za binadamu kwa umma wanaoutumikia lakini wao watake kutendewa haki za binadamu wakati wa kuwajibishwa.

Mfano, mtu kaajiriwa mahali fulani kuwatumikia wananchi, mtu huyo anaamua kuiba mali za umma kimakusudi, kwa maana ya kwamba ni mwizi, ila mtu huyo asiwajibishwe kwa madai ya kwamba kwa kufanyiwa hivyo anakuwa hajatendewa haki za binadamu! Ieleweke kwamba mtu wa aina hiyo tayari anakuwa ameuvua ubinadamu. Hiyo maana yake ni kwamba hata haki za binadamu zinazotajwa anakuwa amezivua vilevile, kwa nini aendelee kuhusishwa nazo?

 Rais Magufuli anatumbua majipu yaliyo katika mamlaka yake, katika hilo siwaelewi wanaosema kwamba anakwenda nje ya haki za binadamu wanamaanisha nini. Maana angekuwa anatumbua wale wasiomhusu, kama vile viongozi wa dini na taasisi nyingine zisizohusiana na mamlaka yake basi ningeweza kuiona mantiki ya madai yao.  Lakini madai ya kwamba anawatangaza au kuwatumbulia hadharani wanaotenda maovu kwenye utumishi wao sioni kama yana mashiko. Sababu urais na utumishi wa umma ni kitu cha uwazi, kwa nini maovu yanayotokea kwenye utumishi huo yawe masuala ya siri? Watumishi wa umma ni kwamba mwajiri wao ni umma, sasa iweje wawajibishwe kwa maovu yao bila umma, mwajiri kuelewa kilichowasibu?

 Mbona Rais anapomteua mtu kwenye nafasi yoyote inatangazwa wazi bila kificho na hakuna anayelalamika kuwa kavunjiwa haki za binadamu kwa jina lake kutangazwa kuwa kateuliwa mtu kwenye nafasi ya ukuu wa mkoa, wilaya, balozi nchi za nje na kadhalika? Kwa nini mtu huyo anaposhindwa kuyatekeleza majukumu yake kadiri inavyopaswa asitangazwe hadharani?

 Ikumbukwe kwamba mambo ya aina hiyo, kuyaficha maovu yanayofanywa na watumishi wa umma, na badala yake kuwawajibisha kisirisiri au kutowawajibisha kabisa, au mtu kukosea sehemu moja na kuhamishiwa sehemu nyingine  ili nako akaendeleze uovu wake uleule ndiyo yaliyoifanya nchi yetu kujaa majipu haya ambayo Magufuli kajipa jukumu la kuyatumbua.

Kwa maana hiyo tunapaswa kuelewa kwamba huu ni wakati mwingine kabisa. Ni wakati wa kuitibu nchi yetu na kuiponya kabisa na ugonjwa huo wa kujitakia. Lakini tukianza kuleta madai kama hayo ya kwamba utabibu unaofanyika hauzingatii haki za binadamu ambazo vilevile hazizingatiwi na maradhi husika, basi tutakuwa tumejigeuzia kwenye ule usemi wa ‘mficha maradhi kwa kusudi au kwa kuogopa lawama kifo ndicho kitakacho kuja kuweka kila kitu wazi.’ Kwa nini tusubiri mambo yawe hivyo?

 Utumbuaji wa majipu kwa mtindo wa Magufuli ni mzuri sana, ni mtindo wa kutibu na kuweka kinga sawia. Maana mtu anayetumbuliwa hadharani anawafanya wengine ambao hawajawa majipu kujiepusha na mambo ambayo yanaweza kuwafanya nao kuota majipu. Hiyo ni kinga ambayo inamrahisishia Rais kuendelea na kazi ya kutumbua majipu kila wakati. Inamfanya atibu akiwa ameweka chanjo kama kinga ya majipu ya baadaye.

 Kama alivyosema yeye Rais Magufuli, ni kwamba wale wanaodai kwamba namna yake ya utumbuaji wa majipu inakosa uhalali wa haki za binadamu nao ni majipu ambayo bado hayajamulikwa. Kwa maana hiyo, wakati wao ukifika nao ni lazima watumbuliwe pia. Pengine kwa kulielewa hilo ndiyo maana wanaanza kulalama, wanajua kwamba majipu ni ugonjwa mbaya ambao kutibiwa kwake ni lazima mwenye ugonjwa huo apate maumivu.

Swali ambalo ni rahisi kwa kila mmoja wetu kujiuliza ni la kwa nini anayeelewa maumivu ya kutumbuliwa majipu aendelee kuyafuga majipu? Sababu kwa kadiri inavyoonekana, watu wanayatetea majipu, ni lazima majipu hayo ni ya kufugwa. Isingekuwa hivyo watu wakahangaika kuyatetea wakiyajengea hoza za kuyalinda kiasi cha kusema kwamba utumbuliwaji wa majipu hayo haufuati haki za binadamu.

 Nataka nimshauri Rais Magufuli kwamba asiwasikilize wenye madai hayo ovu, yeye aendelee kutumbua majipu tena akiwa amefumba macho kusudi asiweze kuwaangalia usoni hao wenye majipu na baadaye akawaonea huruma. Ila atakayeona anazo dalili za majipu ni bora akawahi kujitumbua mwenyewe  kwa njia anazozielewa hazitamletea maumivu makali. 

Kwa namna hiyo, mbali na kwamba atakuwa amejisaidia mwenyewe kwa kuyakwepa maumivu ya mtumbuaji mkuu, pia atakuwa amempunguzia na kumrahisishia kazi Rais wetu.

 Nimalizie kwa kusema, Magufuli tumbua majipu bila kuyasikiliza maneno ya watu wenye dalili za majipu. “Mtu dawa halii kunoga, analia kupona tu basi”.

 

prudencekarugendo@yahoo.com

0784 989 512

1459 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!